MAKALA MAALUM: Kero ya wakazi kugeuza makaburi ya umma majaa ya taka Mombasa

MAKALA MAALUM: Kero ya wakazi kugeuza makaburi ya umma majaa ya taka Mombasa

Na WINNIE ATIENO

KATIKA Kaunti ya Mombasa, wafu hawalali pema kwani makaburi yamegeuzwa majaa ya takataka.

Makaburi ya umma ya Kongowea na Manyimbo yametekwa na watupaji takataka ambao hawajali kuhusu hitaji la kuheshimu safari ya mwisho ya maisha ya binadamu.

Familia ambazo zilizika jamaa wao katika makaburi hayo wanalalamika kwani wameshindwa kuvumilia uchungu wanaopitia kila mara wanaposhuhudia jinsi makao ya mwisho ya wapendwa wao yamenajisiwa.

Katika makaburi ya Kongowea, wafanyabiashara pia wamegeuza sehemu hizo ziwe za kuuzia bidhaa ambazo hutandazwa juu ya makaburi.

“Soko limejaa, mnataka niuze wapi bidhaa zangu? Ambieni serikali ya kaunti itupe nafasi sokoni kama hawataki tuuzie hapa. Lazima tutafute riziki,” akasema mmoja wa wafanyabiashara hao, Bi Jane Sawe. Bi Sawe ambaye huuza nguo alisema haogopi uwezekano wa kuwepo majini makaburini kwani ashazoea.

Kando yake, kuna mwenzake ambaye amejenga nyumba juu ya makaburi matano. Anadai kuwa hakufahamu hapo ni makaburini wakati aliponunua kipande hicho cha ardhi.

“Nilitapeliwa nikanunua ardhi hii katika miaka ya tisini. Niliamua kujenga nyumba lakini baadaye nikaiuza. Nilishindwa kuishi kwa nyumba hiyo kwani nilikuwa na hofu tele,” akasema, akiomba asitajwe jina gazetini.

Inasemekana kuwa zamani sehemu iliyokuwa imetengwa na serikali kutumiwa kama makaburi ilikuwa kubwa lakini watu wakaanza kunyakua ardhi hadi sasa ambapo takataka zimejaa.

Inahofiwa ikiwa hakuna hatua zitachukuliwa kuhifadhi sehemu hizo, huenda baadaye ardhi yote ikanyakuliwa ikiwemo sehemu ambazo watu walizikwa.

Wakati tulipozuru eneo hilo, tulikuta baadhi ya watupaji taka wakiendeleza shughuli zao huku kukiwa na watu wanaosubiri kuchakura ili wapate mali wanzoweza kuuza.

Bw Benson Wamali ambaye ni mtaalamu wa mazingira alitaja hali hiyo kuwa ya hatari na inayoweza kusababisha maradhi kwa binadamu.

“Kuchanganya miili ya wafu na takataka za nyumbani kutasababisha janga Mombasa. Hufai kutupa aina yoyote ya takataka makaburini. Hiyo si sehemu ya kutupa takataka,” akasema.

Bw Wemali ambaye aliwahi kuwa afisa wa Mamlaka ya Kuhifadhi Mazingira Kitaifa (Nema) alishangaa kwa nini serikali ya kaunti imeruhusu watu waendelee kuchafua sehemu hizo.

“Kuna sehemu zilizotengwa kwa matumizi ya kutupa taka, mbona watu wanaruhusiwa kufanya hivyo makaburini? Ulimwenguni kote, makaburi ni sehemu zinazotunzwa na wananchi pamoja na serikali,” akasema.

Alitoa wito kwa serikali ya kaunti inayoongozwa na Gavana Hassan Joho ichukue hatua haraka kuhusu suala hilo.

Hata hivyo, alishauri pia wananchi hasa Wakristo ambao ndio hutegemea sana maeneo hayo kwa mazishi waungane kuyatunza jinsi wafanyavyo Waislamu na Wahindi.

Bw Bruno Mahoka, 65, ambaye alizika jamaa zake wanane katika makaburi ya Kongowea alisema ameshindwa hata kutambua sehemu alikowazika kwa sababu kote kumejaa taka.

“Kila mwaka huwa naja hapa Novemba 2 kwa kumbukumbu ya jamaa zangu lakini nahofia mwaka huu utakuwa tofauti kwa sababu ya taka hizi. Nimeshindwa kupata makaburi ya jamaa zangu wanne,” akasema katika mahojiano na Taifa Leo.

Bw Mahoka alisema ametafuta usaidizi katika afisi nyingi za serikali lakini hali yazidi kuwa mbaya.

“Baadhi ya makaburi yameharibiwa na malori ambayo huleta taka hapa. Siku hizi huwa wanachoma taka na tunahofia moto waeza kuathiri miili iliyozikwa chini,” akaeleza.

Bi Sheila Machika, mkazi wa Kongowea alisema alishindwa kupata kaburi la kakake aliyezikwa mwaka wa 2016.

“Nilikuja hapa haraka niliposikia kuna tingatinga imeharibu makaburi mengi. Kama tungekuwa na pesa tungesafirisha mwili wa kakangu hadi kwetu Kakamega lakini sisi ni masikini. Ni bora tuambiwe kama sasa sehemu hii ni jaa la takataka ili tukae tukijua hivyo,” akasema kwa masikitiko.

Hali si tofauti katika makaburi ya Manyimbo.

“Tunafaa kuheshimu wafu. Kile tunachoshuhudia Mombasa kinasikitisha,” alasema Bw Paul Opiyo, mkazi wa Tudor.

Hayo yametokea wakati ambapo serikali ya Kaunti ya Mombasa ingali inakumbwa na changamoto kubwa kuhusu utupaji wa taka.

Katika mitaa mingi eneo hilo, taka hutupwa ovyo kwa vile hakuna sehemu maalumu wala mfumo mahususi kusimamia shughuli hiyo.

Waziri wa Mazingira, Kawi na usimamizi wa Taka, Dkt Godfrey Nato alisema hivi karibuni uchafu wote utaondolewa na ua kujengwa makaburini.

You can share this post!

Kalonzo arai Raila awe mgombea mwenza wake uchaguzini 2022

Biden ataka bunge kukinga wanaoshindwa kulipa kodi