Makala

MAKALA MAALUM: Kipusa wa kwanza kutoka jamii ya Lembus kushiriki mashindano ya ulimbwende

November 19th, 2019 3 min read

Na SAMUEL BAYA na PHYLLIS MUSASIA

WAKATI Rose Jerotich, mwenye umri wa miaka 26 alipoitwa mbele ya wazee wa jamii ya Lembus kuwasalimia wakazi mjini Eldama Ravine, Kaunti ya Baringo, aliinuka kwa madaha na kupungia mkono umma kisha akakiendea kipaza sauti.

Wazee kutoka jamii hiyo ya Lembus, mojawapo ya jamii ndogo za Wakalenjin, walikuwa wamekutana katika kituo hiki cha biashara kusherehekea baada ya mahakama kuu jijini Nairobi kuwaorodhesha kama jamii inayotambuliwa kuwa miongoni mwa jamii za Wakalenjin.

Jukwaani, Bi Jerotich aliwasalimia wazee hao kwa lugha asilia kisha baadaye akawaeleza dhamira ya kuwapo kwake mahali hapo.

“Niko hapa kuwasalimu kama jamii yangu ya Lembus. Mimi ndiye mshindi nambari mbili wa mashindano ya mwaka huu ya kumtafuta mrembo wa jamii ya Wakelenjin. Nina furaha kwamba hatimaye jamii yetu ya Lembus iliwakilishwa katika mashindano ya ulimbwende huko Nairobi,” akasema.

“Ila ninataka kuwafahamisha kwamba pia nina mradi wa kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum katika shule yao ya Simotwet ambayo iko katika kaunti hii ya Baringo,” akasema.

Baada ya kuwahutubia wakazi na kushangiliwa, Bi Jerotich alielekea katika uwanja wa karibu wa Eldama Ravine ambako kulikuwa na mashindano ya soka yaliyoshirikisha timu za mtaani.

Kwa muda, alionekana akisherehekea mchezo huo na vijana kando ya uwanja huo na alionekana kuwa kivutio kila alipofika.

Tulitaka kufahamu umaarufu wa msichana huyu na safari yake ya kupambana na maisha katika jamii hiyo ya watu wachache.

“Nilizaliwa mwaka wa 1993 katika eneo hili la Eldama Ravine. Kama tunavyojua hili ni eneo ambalo wakaaji wake wengi ni wale wa kutoka jamii ya Lembus. Kwa miaka mingi hatukuwa tumejulikana kama jamii ila tulichaganywa tu katika jamii kubwa ya Wakalenjin,” akasema katika mahojiano yetu.

Mashindano ya kumsaka mlimbwende wa jamii ya Kalenjin yalifanyika mapema mwaka 2019 katika hoteli ya Weston iliyoko jijini Nairobi.

Bi Jerotich, ambaye kwa sasa ni mwanafunzi anayesomea somo la Kiingereza na Fasihi katika Chuo Kikuu cha Egerton, kitivo cha Nakuru Mjini, anaambia ukumbi huu kwamba ilikuwa heshima kubwa kwa jamii ya Lembus kushiriki katika mashindano yake kwa mara ya kwanza.

“Mimi ninatoka katika jamii ya Lembus Inotti na ninashukuru kwamba hatimaye tumepata hadhi ya kujulikana kama jamii kamili,” akasema.

Ila masimulizi yake yanatia moyo maadamu yanaeleza jinsi bidii inavyoweza kumfanya mtu afaulu maishani. Alianza kwa kuuza mboga aina ya mnavu (managu) katika kijiji cha kwao Sigor hadi kufikia sasa ambapo ana ushawishi mkubwa miongoni mwa vijana wa jamii hiyo.

“Nilimaliza masomo yangu ya sekondari mwaka wa 2013 na kupata alama ya C+.

Hata hivyo, kutokana na ukosefu wa karo nilibakia nyumbani kwa miaka mitano mpaka 2018 ambapo nilijiunga na Chuo Kikuu cha Egerton. Na sababu ilikuwa moja tu; wazazi wangu hawakuwa na fedha za kunilipia karo,” akasema katika mahojiano na Taifa Leo.

Ili kukabiliana na hali ngumu za kimaisha, kati ya mwaka wa 2014 na 2015 aliamua kuanzisha duka dogo la kuuza nguo katika kijiji hicho na alisema alifanya hilo kwa bidii kubwa ili kufanikiwa kimaisha.

“Huo muda haukuwa mzuri sana kwa sababu nilizoea kuzunguka katika vijiji vya Sigor na Kewangoi nikiuza mboga zangu aina ya managu. Maisha yalikuwa magumu lakini nilivumilia kwa sababu nilijua kila kwenye wingu jeusi kuna mwangaza hapo mbele,” akasema.

Bi Jerotich, mbali na kuibuka mshindi nambari mbili, kwa sasa pia ni msemaji wa kutia ari hasa kwa watu wanaolemewa na ugumu wa maisha. Juhudi zake hizi huzielekeza katika shule na mihadhara mingine ya umma.

Aliwezaje?

Je, aliwezaje kupata fursa ya kushiriki katika mashindano hayo ya ulimbwende ambayo hapo awali, hayakuwa katika fikra zake.

“Siku moja nilikuwa katika mtandao wa kijamii na hapo ndipo nikaona tangazo limewekwa likitangaza kuhusu mashindano hayo jijini Nairobi. Mashindano yenyewe yalikuwa yameandaliwa na wakfu wa jamii ya Wakalenjin wanaoishi Ulaya ila mapato yake yalikuwa yatumiwe kuzisaidia jamii zinazoishi nchini,” akasema.

Alisema kwamba kupitia kwa mwito wa kutaka kushirikisha jamii, aliamua kujihusisha katika mashindano hayo na akaibuka mshindi nambari mbili, jambo ambalo anasema hadi leo bado haaamini lilivyomtokea.

“Mashindano yalikuwa na lengo moja tu. Kuinua jamii ya Wakalenjini humu nchini ingawa waliopanga mashindano hayo ni Wakalenjin wanaoishi katika mataifa ya nje,” akasema.

Bi Jerotich alisema kuwa ingawa ushindi wake huo ulimwezesha kupata sifa na hadhi miongoni mwa wanajamii, hatua hiyo alisema ilikuwa ya kihistoria kwa sababu jamii hiyo haikuwahi kushirikishwa awali katika mashindano ya hadhi hiyo.

“Ni mwanzo mpya kwa jamii ya Lembus kwa sababu hata baada ya kukubalika kama jamii rasmi kwa sasa, macho yote sasa yanaangazia juhudi ambazo tunafaa tufanye kama jamii kuendeleza utaamduni na malengo yetu kama Lembus,” akasema katika mahojiano yetu.

Aliwataka vijana kujibidiisha na kutafuta riziki kwa njia halali na vilevile wajiepushe na madhara ambayo yanaweza kuwarudisha nyuma kimaisha na kukatisha matumaini yao.