Makala

MAKALA MAALUM: Madereva wa kike sasa kivutio kipya katika teksi jijini, wanaume pabaya!

May 6th, 2018 3 min read

Na MASHIRIKA

WANAWAKE wameteka biashara ya teksi jijini Nairobi na idadi yao inazidi kuongezeka.  Inakisiwa kuwa jijini Nairobi pekee kuna teksi 12,000 ambazo kwa jumla huzoa mapato ya Sh20 milioni kwa siku.

Madereva wa kike wanasemekana kuwa asilimia tatu pekee lakini wadau wanasema idadi yao inaongezeka kwa haraka.

Sababu kuu ya ongezeko hilo ni visa vya dhuluma na mashambulizi vinavyoripotiwa hususan na wateja wanawake dhidi ya madereva wa kiume.

Vile vile, kumekuwa na ongezeko la kampuni zinazotoa huduma za teksi na ambazo zimechangia kuimarisha mazingira ya kazi, na hivyo kuwavutia madereva wanawake.

Kampuni hizi zinatumia teknolojia ya kisasa kuunda programu za simu (Apps) zinazounganisha madereva na wateja wao, katika mfumo wa e-taxi.

Moja ya kampuni hizo Little Cabs ambayo programu yake inakupa fursa ya kuchagua dereva wa kiume ama kike, imeshuhudia ongezeko mara 13 katika idadi ya madereva wake wa kike kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.

“Tulikuwa na madereva 27 wa kike wa Little Cab tulipoanzisha huduma zetu 2016, sasa wamefika 381. Tunalenga kuwa na madereva 1,000 wa kike kufikia mwisho wa mwaka huu,” alisema Jefferson Aluda, meneja wa mipango wa Little Cabs.

“Watu wengi hudhani kazi ya udereva wa teksi ni ya wanaume pekee lakini mtazamo huo unabadilika. Wateja wetu wanawasifia madereva wa kike; kwamba ni waangalifu sana na hudumisha weledi kazini. Tunatarajia wanawake zaidi kuungana nasi tutakapofanya uteuzi.”

Huku idadi ya kampuni za teksi zinazotumia teknolojia ikizidi kuongezeka, ili kuziba mwanya wa mfumo mbovu wa uchukuzi wa umma jijini Nairobi, idadi ya wanawake wanaosaka ajira za madereva inapanda.

Wanawake hao wanasema kuwa wanavutiwa na ratiba rahisi ya kazi, fursa ya kuchagua mteja wa kubeba na hakikisho la malipo.

“Kuwa dereva wa teksi si jambo ambalo ningeliwazia awali, lakini baada ya kujiunga na kampuni ya teksi inayotumia App kutoa huduma, nimebaini kwamba ni kazi nzuri kwa wanawake,” asema Lydia Muchiri, 29.

“Ni mwafaka, rahisi na salama – bora zaidi kuliko kuketi nyumbani kusubiri misaada,” aliongeza.

Hata hivyo, wanawake bado wanakabiliana na changamoto mbalimbali ili kustawi kiuchumi, kijamii na kisiasa nchini.

Wanachangia asilimia 33 pekee ya wafanyakazi 2.5 milioni walio na ajira za ofisini huku wakimiliki asilimia 1 pekee ya ardhi za kilimo, kwa mujibu wa Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS).

 

Kuimarisha maisha

Kuchipuka kwa apu za teksi kumechangia pakubwa kuwapa wanawake fursa ya kupata ajira na hivyo kuimarika kiuchumi.

Katika miaka mitatu iliyopita, takriban Apps 10 zimezinduliwa kukidhi mahitaji ya tabaka la watu wanaotumia simu za kisasa kusaka huduma mbadala za uchukuzi za bei nafuu na salama.

Madereva wa teksi hulipwa takriban Sh30 kwa kila dakika huku kampuni ikiwatoza ada ya hadi asilimia 25. Licha ya hayo, wanawake wamepongeza kampuni ambazo zimewapa fursa ya kuhudumu kama madereva wa teksi kama vile Uber, Taxify, Little Cabs na Pewin.

Ukiondoa ada ya kampuni, mafuta na kukodisha gari, madereva wanaohudumu kwa saa 12 kila siku hupokea takriban Sh60,000 kila mwezi, duru katika sekta zasema.

Faridah Khamis, mzazi wa pekee wa watoto watano, aliamua kuwa dereva wa e-taxi Februari mwaka 2017 baada ya kuhimizwa na dereva mmoja wa kiume.

“Ingawa malipo yako chini na lazima nifanye kazi saa 12 kwa siku – watoto wangu wakiwa shuleni na usiku wakiwa wamelala – ni afadhali kuliko kazi za ofisi za siku hizi,” alisema mama huyo mwenye umri wa miaka 36 kando ya gari lake aina ya Mazda Axela.

 

Usalama

“Vile vile, ni salama kwa wanawake. Mimi ndiye huamua wakati wa kufanya kazi, ni wapi nitakapoenda na wateja nitakaobeba. Ningekuwa dereva wa teksi za kawaida ingenilazimu kuwa barabarani wakati wote ili kusaka wateja. Kupitia apu ya simu mimi huwapata wateja kwa urahisi nikiwa nyumbani kwangu.”

Madereva hao wa kike huchagua wateja ambao maelezo yao ni mazuri, na hukubali tu kubeba wateja wanaoenda maeneo yaliyo na watu wengi.

Kampuni zao pia huwafuatilia kupitia GPS na apu zao ziko na pahali pa kubonyeza wakihisi wamejipata katika hatari.

Maafisa wa Uber, kampuni nyingine inayotumia teknolojia kutoa huduma za teksi, wanasema programu hizo za simu za kisasa ni fursa nzuri ya kiuchumi kwa wanawake hususan katika mataifa yanayoendelea kama Kenya.

“Apps kama za Uber zinasaidia kuondoa vizingiti vinavyowazuia wanawake kushiriki kikamilifu katika ukuzaji uchumi,” msemaji wa Uber kanda ya Afrika Mashariki, Bi Janet Kemboi, alisema.

“Vizingiti hivi ni pamoja na ubaguzi wa kijamii, hatari za usalama, kutengwa kifedha na kidijitali na ugumu wa kupata magari pamoja na mali nyingine.”

Licha ya mazingira kuimarika na sekta kushuhudia ongezeko la madereva wa kike, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za ubaguzi na dhuluma.

Kama vile ugumu wa kukodisha magari kwa sababu ya dhana potovu kwamba wanawake si madereva wazuri na usumbufu wa wateja wanaume walevi.

 

Usumbufu

Kwa sababu nambari zao za simu zinapatikana kwa urahisi kwenye apu za teksi, wanawake madereva husumbuliwa na simu za “kuwajulia hali’ kutoka kwa wateja ambao wanataka uhusiano wa kimapenzi.

Vile vile, wanakabiliwa na dhana kwamba wao ni makahaba kwa sababu ya kuvalia maridadi, kufanya kazi usiku na kufanya kazi ya “wanaume”.

Hata hivyo, wanawake hao wanasema changamoto hizo si za kila siku na kwamba kufanya kazi kama dereva wa teksi kumewafanya baadhi kuota maono ya kumiliki magari yao binafsi ya teksi – ya wateja wanawake zinazoendeshwa na madereva wanawake.

“Kuna hitaji la madereva wa teksi wa kike. Wateja hupongeza mienendo na weledi wetu. Baadhi yao hutuambia kwamba magari yetu ni salama na safi zaidi kuliko ya madereva wanaume,” akasema Muchiri.

“Tunajivunia kazi yetu. Sisi si duni kuliko wale wanaofanya kazi za ofisi. Magari yetu ndiyo ofisi zetu na tunaamini kwamba tunapoingia ndani ya gari lazima tuwe weledi.”

(Makala yametayarishwa kwa hisani ya Thomson Reuters Foundation).