Makala

MAKALA MAALUM: Mafumbo, vijembe na matumizi ya jumla ya vazi la leso Uswahilini

January 2nd, 2020 3 min read

Na MISHI GONGO

MIPASHO ni sehemu ya utamaduni wa wanawake wengi maeneo ya Pwani ya Afrika Mashariki.

Kwenye sherehe za ngoma kama vile muziki wa Taarabu, nyimbo zinazoporomoshwa na watribu huwavutia wanawake wengi, sio tu kwa kuwa midundo ya muziki kuwakosha nyoyo zao, bali hasa maneno yanayotamkwa.

Kwa mfano Mwaka 2004 Jokha Kassim akiwa na kundi la Zanzibar Stars aliimba wimbo ‘Unalo Lilokukaa na Roho’.

Kibwagizo chake kilikuwa hivi:

Lo hasidi, fisadi mkubwa, utakufa nacho kijiba cha roho,

Kinakupekechaa, ndani kwenye moyo,

Utazikwa naayo, roho mbaya na chooyo,

Utamuona hivi hivi, mwana wa mwenzioo.

Wimbo huu kila ulipoimbwa, baadhi ya wanawake walionekana wakikonyezana au kutabasamu, ikiwa na maana kuwa kulikuwa na ujumbe uliopitishwa kumsimanga mwanamke mwengine.

Nyimbo za Khadija Kopa kama vile ‘Mfunge Kamba Mumeo’, ‘Mjini Chuo Kikuu‘, ‘Mwanamke Mambo’, zinaangazia zaidi mashairi ya vijembe, maarufu kama Rusha Roho.

Lakini si Taarabu pekee bali hata vazi maarufu la mwambao lijulikanalo lama khanga au leso.

Leso ni vazi lenye umuhimu mkubwa kwa wanawake wa Pwani. Si ajabu kuona wanawake wamezivaa leso katika sherehe na hata wanaposhinda nyumbani.

Ni fahari ya mwanamke aliyeolewa kumiliki gora nyingi za leso, kwa sababu huonyesha matunzo bora kutoka kwa mumewe.

Leso ni kitambaa kilichotengenezwa na pamba, chenye umbo la mstatili, kilichorembwa kwa maua na semi au methali za Kiswahili zinazotuma ujumbe.

Mwanamke baada ya kuvaa nguo, hujifunga leso moja kiunoni na nyingine hujifunika kichwani kwa kujisitiri.

Kulingana na mtafiti wa mila na tamaduni za Kiswahili, Bi Hamira Saidi, leso hutumika kutuma ujumbe, rasilimali kwa wanawake, kuonyesha msichana ametoka utotoni na kuingia katika utu uzima miongoni mwa shughuli zingine.

Alieleza kuwa leso ni vazi la kihistoria katika pwani ya Kenya. Inaaminika kuwa zililetwa na wareno katika Pwani ya Afrika mashariki kwenye visiwa vya Unguja, Pemba na Mombasa katika karne ya 19.

“Leso ni rasilimali kwa mwanamke, ni kawaidi kwa mwanamke kumiliki zaidi ya gora 500, anapokumbwa na matatizo ya kifedha huuza leso hizo kujipatia fedha,” alisema Bi Saidi.

Aidha alisema maandishi ya leso hutumika kupongeza, kuonyesha shukrani au hata kugombana.

“Mwanamke anaponunua leso hutazama maandishi ili kuwasilisha ujumbe anaotaka kumpa mtu. Leso za mwanamke aliyejifungua au mzazi huwa na jumbe za kongole kwa mfano Karibu mgeni, Asante mama kwa malezi na kadhalika,” akasema Bi Saidi.

Alieleza kuwa wanawake wa Kiswahili au Pwani walipendelea kufumbana kutumia jumbe za leso.

“Wanawake wangeweza kutuma ujumbe bila kuzungumza kufuatia maneno yaliyoandikwa kwa kanga aliyovaa,” alisema Bi Saidi.

Bi Saidi pia alieleza kuwa baada ya msichana kuvunja ungo, alipelekwa kwa shangazi yake ambaye angemfundisha majukumu yake katika jamii na mambo ambayo hapaswi kufanya.

“Watoto wa kike kati ya siku zake saba za hedhi, alifundishwa mapishi, kujistiri, kuhudumia familia kisha baada ya mafunzo hayo angepewa gora za leso ambazo alistahili kujifunga kama sitara wakati yuko nyumbani,” akaeleza mtafiti huyo.

Kwa wanandoa, Bi Saidi alisema mwanamke angekunja leso miundo mbalimbali kutuma ujumbe kwa mumewe.

“Wanawake walikuwa na haya au aibu, maneno mengine ilikuwa ni vigumu kuyatamkia mumewe. Anapokuwa kwa hedhi mwanamke angekunja leso umbo la pembe tatu kisha kuweka katikati ya kitanda ili kumtaarifu mumewe,” akasema.

Leso hutengenezwa kupitia kitambaa laini, hivyo ni murua kwa kulalia wakati wa joto.

Maandishi kwenye leso huwa na ujumbe mzito. Picha/ Hawa Ali

“Kinyume na sasa, mwanamke aliyeolewa alipaswa kulala na leso katika mila za Waswahili,” akasema mtafiti huyo.

Hutumika katika kushikia mtoto aliyezaliwa ili kumuepusha na kushikwa na mafua au nzio.

“Leso ni kitambaa baridi na laini ambacho hakitoi nyuzi kama vitambaa vyengine vinavyotumika kubebea mtoto. Nyuzi zile huletea mtoto mafua, na ugumu wa kitambaa hukwaruza ngozi ya mtoto na kumpa harara mwilini,” alieleza.

Aidha hutumika katika shughuli za kuoshea maiti. Na pia kutofautisha kati ya jeneza la mwanamke na mwanamume.

Bi Saidi alieleza kuwa japo matumizi ya leso kwa sasa yamebadilika bado zina umaarufu mkubwa Pwani.

“Watu wa sasa hutumia leso kushona nguo kudumisha utamaduni wa Wapwani. Mabibi harusi hutia vipande vya leso kutukuza utamaduni,” alisema Bi Saidi.

Aidha katika sherehe kama mikutano, harusi na shughuli zenginezo leso hutumika katika kupamba majukwaa.

Bi Nuru Juma mkazi wa Mombasa alieleza kinyume na miaka ya nyuma ambapo methali na semi za Kiswahili zilitumika, leo hii watu hutumia maneno ya Sheng ilimradi kuvutia wateja wa umri mbalimbali.

“Leo hii si ajabu kuona leso imeandikwa kwa Kiingereza au sheng. Kwa mfano No one but you, au Ukinidelet wenzako wanidownload,” Bi Nuru akasema.

Wanaotunga maandishi ya leso wamekuja na mbinu hiyo ili kuvutia vijana.

Bi Nuru aliwaonya wanawake dhidi ya kununua leso au kuvaa bila kuchunguza jumbe zilizoandikwa.

“Kama mwanamke kuna watu unaowaheshimu kwa mfano mama mzazi au mavyaa. Kuvaa leso zenye jumbe za kejeli au kukonyeza ni ukosefu wa adabu,” alieleza.