Makala

MAKALA MAALUM: Nyandarua yalemewa na visa vya mauaji na kujitia kitanzi

November 14th, 2019 3 min read

Na WAIKWA MAINA

MAKABURI matatu katika lango kuu la shamba na nyumbani mwa Bi Margaret Wambui yamesalia kuwa kumbukumbu ya majonzi ya kuwapoteza mwanaye na wajukuu wawili.

Bado uchungu anao wa kuelewa mawazo gani yalipelekea mwawawe kuwauwa wanawe kwa njia ya kuwakatakata kinyama kabla ya kujitoa uhai kwa kujonyonga. Hilo, anasema, haliwezekani wala kueleweka.

Familia ya Bi Wambui pia inasema mauaji hayo ni jambo ambalo hawakuwahi kuwaza lingewafika.

Unyama huu ulitokea katika kijjiji cha Mwisho wa Lami, eneo Bunge la Ol Kalou, Nyandarua, wakati mwendeshaji bodaboda Kelvin aliwachinja wanawe wenye umri wa miaka sita na minane, kisha akajinyonga chumbani mwake.

Vifo hivyo vimemuacha Bi Wambui mpekwe, wala hamna sauti ya kumfariji jinsi alivyozoea kabla ya wingu la hofu kumfika.

Bi Margaret hajasahau jinsi alivyowapikia wajukuu wake kuwasimamia kufanya kazi ya ziada waliyopewa shuleni, kuwaosha na kuwapeleka chumbani mwa baba yao kwa malazi.

“Mwanangu Kelvin alikuwa mtu wa bidii ya kuwatunza wanawe. Mara nyingi alichelewa kazini na kufika usiku wa manane na aliwapenda sana wanawe. Nami nilikuwa kama mama mlezi kwa wajukuu wangu,” akasema Bi Margaret.

Tangu vifo hivyo tatanishi zaidi ya miezi mitatu iliyopita, Bi Margaret hajaamua kubomoa chumba cha Kelvin kinachomkumbusha machungu.

Na anapopambana na hali yake, familia na majirani katika kijiji cha Mawingu wako hali hiyo hiyo baada ya familia mbili tofauti kuwa na mkasa wa mauaji ambapo wazee wa boma waliwaua kinyama wake zao na kisha kujitoa uhai.

Moja ya familia hizi ni ile ya Bw Justice Ndung’u aliyemkatakata mkewe Monicah Muthoni kabla ya kujinyonga, na ile ya Bw Samuel Kamakia, mwalimu mstaafu aliyejifungia chumbani na kukiteketeza na wakaungua yeye na mkwewe Veronicah Wanjiru.

Katika kijiji cha Jua Kali mjini Ol Kalou, chumba cha kukodi walimoishi wanafunzi wa chuo cha uuguzi bado hakijapata mteja zaidi ya miezi miwili tangu wanafunzi huyo kujitoa uhai kwa njia ya kunywa sumu chumbani.

Bw Joshua Mbogo, jirani, asema kuwa wateja wanaepuka chumba hicho baada ya kupata fununu kuwa mwanafunzi alijitoa uhai humo ndani na hivyo kukifanya chumba kuwa eneo la uhalifu.

Kamishna wa Kaunti ya Nyandarua, Bw Boaz Cherutich anakiri kuwa visa vya kujitoa uhai vimekuwa kitendawili ambacho serikali kuu na ile ya kaunti zinajaribu kutegua.

Bw Cherutich asema kuwa zaidi ya watu 43 wameripotiwa kujitoa uhai katika muda wa mwaka mmoja.

Linalowapa viongozi na wakazi kiwewe ni jinsi mauaji haya hutekelezwa, ambapo anayekusudia kujiua huwaua kwanza jamaa wake wa karibu wakiwemo watoto na mke.

Dalili

Katika visa vyote, marafiki na familia wanasema walikuwa wameona dalili na mabadiliko ya tabia kwa waathiriwa, lakini wakakosa kutilia mabadiliko haya maanani, kabla ya kuua na kujiua.

Katika visa hivi, waliokusudia kujiua waliishi maisha ya upwekwe wakijifungia chumbani kwa masaa mengi na wakitumia mbinu zote kuepuka kutangamana na familia na marafiki

Bi Wambui na Bw Josphat Mugo, mjombake kelvin na rafiki wa dhati Samuel Kang’ethe walikiri kuona mabadiliko haya kwa marehemu Kelvin lakini hawakutilia maanani hadi kisa kikatokea.

“Alitumia masaa mengi kitandani hadi kuisahau kazi aliyopenda. Mara nyingi nililazimika kumkumbusha na kumshawishi aende kazini,” akaelezea Bi Wambui.

Anasema kuwa mwanawe marehemu Kelvin alikuwa na matatizo ya ndoa baada ya mkewe kumtoroka, lakini Kelvin alionekana mtulivu na mpole.

Mamake Kelvin anaamini ni katika utulivu huu ambapo mwanawe alipanga mauaji ya wanawe wawili na pia kujitoa uhai.

“Aliwaita wajukuu wangu kutoka kwa jirani wetu ambapo walicheza na wenzao, akawafungia ndani ya nyumba na kisha akawakatakata kama mboga,” akaelezea Bi Margret huku akijikakamua kuyafungia machozi.

Nako katika kijiji cha Captain ambako Bw Kamakia waliungua na mkewe baada ya kutia kiberiti nyumba yao, kibarua wao wa muda mrefu pia anakumbuka kuona dalili za upweke majuma kadhaa kabla ya Bw Kamakia kuyatekeleza mauaji.

“Awali, mwajiri wangu aliamka mapema kuwasimamia wafanyikazi na hata kutangamana nao kwa njia ya urafiki. Lakini alianza kuamka akiwa amechelewa na kuutumia muda mwingi chumba cha malazi na hakuonekana kujali chochote,” akadai Bw Gitau Njeri.

Mtaalamu wa afya Dkt Jorum Muraya alizitaja dalili walizoonyesha waliotekeleza mauaji na kujitoa uhai kama tatizo la akili kutokana na mawazo mengi wasio na jibu lake.

“Dalili za matatizo ya akili kutokana na mawazo ni kujitenga kutoka kwa familia na marafiki na mtu kukosa au kusahau kutimiza majukumu yake. Ni dalili ambazo jamaa na marafiki wanaweza kuzitambua mapema na kuchukua hatua kuzuia kupoteza maisha jinsi hii,” akasimulia Dkt Muraya.