MAKALA MAALUM: Reli ya Nanyuki-Nairobi kufufua uchumi wa eneo la Mlima Kenya

NA JOSEPH WANGUI

“Reli hiyo itapunguza unyanyasaji wa wakulima wadogo na kufanya mazao yao ya shambani kufika sokoni kwa haraka. Viwanda ambavyo vilifungwa kama kiwanda cha kahawa cha Kenya Planters Coffee Union (KPCU) vitapata nafasi ya kurejelea biashara. Miji kama ya Sagana na Karatina itakuwa mikubwa kupanuka kiuchumi,”
asema mkulima wa mchele na mfanyabiashara kutoka kaunti ya Kirinyaga Bw Muriithi wa Kanga’ra.

MPANGO ya magavana wanane wa eneo la Mlima Kenya kufufua reli ya kutoka Nanyuki hadi Nairobi umeibua matumaini mengi miongoni mwa wakazi, ikiwa ni pamoja na ukuaji wa kiuchumi na uboreshaji wa biashara.

Jumuiya ya wanabiashara na viwanda imesifia mpango huo na kueleza kwamba hatua hiyo itaunda nafasi za ajira na kufungua nafasi za biashara hadi katika nchi jirani ya Ethiopia.

Kiongozi wa jumuiya ya wanabiashara wa kaunti ya Laikipia, Bw Francis Gitonga, alisema mradi huu utabadilisha mji wa Nanyuki na kuufanya ‘bandari ya nchi kavu’.

Hata hivyo, ameomba magavana hao kuimarisha reli hiyo na kuifanya ya kisasa (Standard Gauge) wala si tu kuifufua kwa kuirekebisha.
Anasema wanabiashara pamoja na wakulima ndio wamelengwa kunufaika na mradi huo zaidi.

“Pia reli hiyo itaokoa fedha za serikali kwa ajili ya kutengeneza barabara na kuvutia wawekezaji kuelekea maeneo mengine ya ndani ya nchi si tu Nairobi pekee. Muda na gharama ya usafiri ni sababu za kuzingatia katika biashara yoyote”, anasema Bw Gitonga.

Amewaomba magavana kuboresha reli hiyo kwa kusaka ujuzi kutoka nchi zilizoendelea kama Uchina, Marekani na Uingereza.

“Sekta za utalii na ujenzi zitafaidika pakubwa kutokana na mradi huo ukikamilika. Serikali ya taifa inapaswa pia kuunga mkono wazo la magavana hao na pia kuzipa serikali za kaunti fedha zaidi,” anasema Bw Gitonga.

Serikali za kaunti ya Nairobi, Kiambu, Murang’a, Kirinyaga, Nyeri, Laikipia, Nyandarua na Isiolo mwaka jana zilikubaliana kutenga Sh25 bilioni ili kufufua njia hiyo ya reli yenye urefu wa kilomita 240 kutoka Nairobi hadi Nanyuki. Kisha baadaye wanapania kuiendeleza hadi Isiolo.

Kaunti hizo zilianza kwa kuchanga Sh100 milioni kila mmoja na kuelekeza fedha hizo kwenye mradi huo.

Waziri wa Biashara na Uwekezaji katika Kaunti ya Nyeri Bi Diana Kendi asema mipango bado inaendelea huku akithibitisha kwamba serikali hizo zishaanza kuchanga hela husika.

Mkulima wa mchele na mfanyabiashara kutoka kaunti ya Kirinyaga Bw Muriithi wa Kanga’ra amefurahia wazo hilo la magavana na kusema kuzinduliwa kwa usafiri wa reli kutaleta manufaa kwa jamii ya Mlima Kenya.

Bw Kang’ara asema kuwa reli hiyo itapunguza unyanyasaji wa wakulima wadogo na kufanya mazao yao ya shambani kufika sokoni kwa haraka.

 

Viwanda kufufuka

“Viwanda ambavyo vilifungwa kama kiwanda cha kahawa cha Kenya Planters Coffee Union (KPCU) vitapata nafasi ya kurejelea biashara. Miji kama ya Sagana na Karatina itakuwa mikubwa kupanuka kiuchumi,” anasema Bw Kang’ara ambaye pia ni Mkurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maji ya Tana Athi

Anaongeza kuwa sekta za kilimo kama chai, kahawa, macadamia na kilimo cha mboga huenda zikanufaika kwa njia kubwa kwa kuwa mazao ya kilimo kwa sasa husafirishwa kwa kutumia malori.

“Usafirishaji bidhaa kwa reli utatufaa sana. Tutakuwa na watu wanaofanya kazi Nairobi na kuishi vijijini kwa sababu gharama na muda wa kusafiri utapungua,”anasema Bw Kang’ara.

Simon Wachira akivuna kahawa katika shamba lake eneo la Kiamwathi, kaunti ya Nyeri Agosti 28, 2017. Picha/Maktaba

Anatazamia zaidi kwamba kutakuwa na nafasi za ajira katika maeneo ya stesheni za abiria za reli na kuwa vijana watapata kazi za upakiaji wa bidhaa za kusafirishwa.

Hata hivyo, mkulima wa chai na mfugaji wa ng’ombe wa maziwa eneo la Othaya Kaunti ya Nyeri anakosoa serikali hizo za Kaunti.

Bw Easu Kioni anasema mradi huo haustahili kupewa kipaumbele katika mipango ya Magavana.

Alisema mradi huo una athari ndogo za kiuchumi na kwa maisha ya wakazi wa eneo hilo la Mlima Kenya.

Anasema Magavana hao wanane wanapaswa kulainisha utendakazi wao na kuipa kipaumbele miradi ya barabara za vijijini katika wilaya zao.

Pia anawahimiza kushawishi serikali kuu kuharakisha ujenzi wa barabara kuu ya Thika-Nanyuki-Isiolo au kufadhili ujenzi huo kwa kutumia zile Sh25 bilioni wanazopangia kuchanga.

 

Taarifa muhimu

“Wakazi na umma hawakuhusishwa kabla ya magavana kutangaza mradi huo. Wananchi wanatakiwa kuwa na taarifa kuhusu ni bidhaa gani itakuwa ikibebwa kutoka eneo hili kwa kutumia njia ya reli ambayo haiwezi kubebwa kwa kutumia barabara zilizopo,” anasema Bwana Kioni.

Bw Kioni ambaye pia alikuwa mshauri wa usalama wa Rais mstaafu Mwai Kibaki, alisisitiza kuwa mradi huo hauna umuhimu kwa sasa.

Anasema kwamba kutumika kwa reli ya Nanyuki ambayo ilijengwa na serikali ya ukoloni mwaka wa 1913 kulipunguka hatua kwa hatua tangu miaka ya 1990 baada ya wakazi kukubali usafiri wa barabara.

Anasema kulikuwa na malalamishi kwamba kusafiri kwa gari la moshi kulichukua muda mrefu. Baadaye sehemu kadhaa za reli hiyo zilianza kuharibiwa na kuporwa.

Magavana wanapanga kuzindua reli ya Nanyuki na kuiunganisha na ukanda wa Lamu Port-South Sudan-Ethiopia Transport (LAPSSET).

Bw Kioni anashauri Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, mwenzake wa Nakuru Lee Kinyanjui na Francis Kimemia wa Nyandarua kwamba badala ya kushughulika na reli hiyo ya Nanyuki, washawishi ujenzi wa barabara ya kilomita 52 inayounganisha kaunti hizo tatu kupitia hifadhi ya Wanyamapori ya Aberdare.

“Barabara ya Aberdare itakuwa na ufanisi mkubwa wa kiuchumi kwa wakazi wa kaunti hizo tatu kuliko reli. Pia itapunguza muda na umbali wa kusafiri kutoka Nyeri hadi Kinangop na Nakuru”, anasema Mr Bw Kioni.

Seneta wa zamani wa kaunti ya Nyeri Bw Mutahi Kagwe, kwa upande wake, anakumbatia wazo la magavana hao lakini anatilia shaka uwezo wa serikali za kaunti kupata fedha za kujenga reli.

 

Hazina uwezo

“Serikali za kaunti kivyao hazina uwezo wa kukopa hela nje ya nchi na haziwezi kujenga reli. Njia ya reli ya Nairobi-Isiolo si gharama kidogo kama inavyodhaniwa. Kaunti husika ziko sehemu ambayo ina milima na ukweli ni kwamba wakazi wanataka reli ya kusafiri kwa haraka wala si ile ya zamani,” anasema Bwana Kagwe.

“Hebu tuwe wakweli, reli ya kisasa ya kiwango cha Mombasa-Nairobi inayojulikana kama SGR ilitumia Sh325 bilioni. Je, unadhani serikali ndogo zina uwezo huo?”auliza Bw Kagwe.

Anahimiza kuwa serikali za kaunti husika zihimize serikali kuu izindue reli ya Nanyuki lakini wasielekeze fedha wanazopata kwa mradi huo.

“Njia ya reli ya Nairobi-Isiolo itakuwa ya manufaa sana ikiwa itafanywa ya kisasa. Ukarabati tu ni jambo la muda mfupi na kupoteza muda na raslimali.Inapaswa kuwa mradi mpya,” anasema Bw Kagwe.

Aliongeza kwamba serikali hizo za kaunti hazistahili kuachilia huduma nyingine na kuelekeza fedha katika mradi huo.

Kwa upande mwingine, Mbunge wa Tetu Mwangi Gichuhi anasema Wabunge wa eneo la Mlima Kenya walikubaliana kuanzisha kundi la kushughulikia mambo ya kiuchumi ya jamii ya Mlima Kenya na kufanya kazi pamoja na magavana.

Wabunge hao walifanya uamuzi huo baada ya mkutano katika hoteli moja mjini Thika.

“Tulikubaliana kwamba tunapaswa kudai haki yetu kama eneo la kati la taifa. Tunafuatilia miradi mingine kama ujenzi wa mabwawa, barabara pamoja na umoja wetu kama jamii,”  alisema Bw Gichuhi.

Habari zinazohusiana na hii