Makala

MAKALA MAALUM: Ubandikaji wa kope bandia ndilo gumzo kuu katika mitaa kwa sasa

August 17th, 2019 3 min read

Na HALIMA GONGO

WAHENGA waliponena ukiona vyaelea ujue vimeundwa, huenda walikuwa wamebashiri mtazamo wa mwanamke wa kisasa.

Urembo unaojidhihirisha miongoni mwa wanawake wengi siku hizi, huwa umewaingiza gharama kubwa na muda mwingi.

Mojawapo ya aina ya urembo ambao ni gumzo la mtaa sasa hivi, ni ule wa kope bandia.

Ubandikaji kope bandia umeshamiri si jijini Nairobi pekee, bali ulimwengu mzima kwa jumla.

Wanawake wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za kukuza kope zao na pia kubandika kope bandia, ili kuimarisha urembo wa macho yao.

Lakini baadhi yao wamedhurika baada ya kubandika kope hizo. Inasemekana waathiriwa walitumia gundi isiyo bora walipobandika kope hizo.

Kulingana na wataalamu wa urembo, tatizo ambalo limewakumba wengi linatokana na gundi inayotumika.

Huenda ikawa gundi inayotumika haifai ngozi ya mlimbwende au gundi ile imeshika sana na hivyo wakati wa kutoa inasababisha zile kope halisi kung’oka. Pia madhara kwenye macho yanaweza kutokana na utumizi wa bidhaa ambazo ni duni au bandia.

Zipo picha ambazo zimekuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii na ambazo zimezua mjadala kuhusu urembo wa kubandika kope bandia. Picha hiyo inaonyesha jinsi mwanamke huyo alivyodhurika baada ya kubandikwa pope.

Kulingana na mtaalamu wa kubandika Kope katika saluni ya Lintons, Bi Samira Kavinya huenda ikawa msichana huyo alidhuriwa na gundi kwenye macho yake, kwa sababu gundi inayotumiwa kubandikia kope hizo huwa na madhara kwa baadhi ya watu.

“Kabla hatujamweka mtu hizo kope, huwa tunashauri kwanza afanyiwe vipimo na hiyo gundi. Tunaweka hiyo gundi katika sehemu ya karibu na macho, kijitone kidogo tu. Tunaangalia kama inamuumiza au la. Iwapo inaonyesha athari zozote kwenye ngozi, hatuitumii. Tunatumia gundi aina nyingine,” akasema Bi Kavinya.

Mtaalamu huyo anasema kwamba gundi inayotumiwa haifai kugusa ngozi ya mtu, na kwamba wataalam wa urembo huwa makini sana wakati wa kubandika kope hizo. Mtu anayetaka kurembeshwa kope huwa anashauriwa kutumia vifaa vya kubandikia kope na kuepuka kuvishika kutumia mkono.

Kope huchukuliwa na kuchovywa kwenye gundi kisha kubandikwa kwenye sehemu ya juu ya kope halisi.

“Haifai na inasisitizwa kuwa mtu asishike kope kwa mkono, ili kuepukana na kuingiza uchafu na pia kuathiri jicho. Unajua mikono yetu huwa inabeba uchafu wa kila ina. Unaweza kudhani kuwa kwa kuzishika kope hizo kwa mikono unafanya vizuri, kumbe unayaumiza macho,” akasema Bi Kavinya.

Sababu hasa ya kuziweka kope bandia ni kuongeza ujazo na pia urefu wa kope na kumfanya mtu apendeze zaidi.

Mwanamke anayetaka ulimbwende anashauriwa kutunza kope zake kila siku kama anavyozitunza nywele zake, iwapo anataka kuimarisha afya na urembo wa macho.

Bi Kavinya anasema kuwa, mtu anapaswa kuziosha kope kutumia sabuni yake maalum (Conditioner) ambayo huwekwa kwenye pamba kisha na kusafisha. Usafi kwenye kope huzisaidia kukua na pia humsaidia mtu kuepuka magonjwa ya mara kwa mara kwenye macho.

“Unafaa kuosha kope zako na conditioner maalumu ambayo huwa inapatikana. Unaiweka kwenye kitambaa kisafi kisha unajisafisha taratibu kwenye jicho moja na unarudia kwa jicho la pili. Pia yafaa uzipake mafuta yanayosaidia kuzifanya zikue kwa haraka,” akasema.

Maskara ni mojawapo ya vipodozi ambavyo wanawake wengi hujipaka ili kuzifanya kope zao zionekane nadhifu na ndefu. Unapochagua maskara unapaswa kuzingatia lengo unalotaka kutimiza kwenye kope zako. Iko maskara ambayo husaidia kope zionekane ndefu. Ipo maskara mabayo huzifanya kope zionekane zimejaa au nene.

Pia kuna maskara ambayo huzifanya kope zisishikane na hii ni aina ya maskara ambayo haiwezi kutoka kwenye kope hata inapooshwa na maji inajulikana kama Water proof Mascara, mara nyingi aina hii hutumiwa na warembo wapohudhuria tamasha mbalimbali au wanapokwenda kufanya mazoezi.

Manufaa ya karatasi

Karatasi inayobandikwa chini ya macho kabla kope hazijaanza kubandikwa, ina manufaa kwenye jicho mbali na kulinda gundi kutiririka kwenye sehemu ya chini ya jicho.

Karatasi hii husaidia kuondoa weusi chini ya macho na pia kuondoa uvimbe ambao hutokea chini ya macho wakati mtu amechoka au amekosa usingizi kwa muda.

Kuna aina nyingi ya kope. Zipo kope ambazo hubandikwa moja moja kama kope hizi hupendwa sana na wengi kwani huwa na muonekano wa kupendeza zaidi kushinda kope zote.

Aina nyingine ya kope ni kope za kushikana ambazo mlimbwende pia anaweza kujibandika akiwa nyumbani.

Macho katika urembo ni kiungo muhimu ambacho huleta mvuto wa kipekee na wa aina yake, na ndio maana wanawake wengi huongeza vikorombwezo aina aina kwenye macho yao ili yawe na mvuto zaidi.