Habari za Kitaifa

Rais Ruto aongoza Wakenya kwa makala ya 61 ya Madaraka Dei

June 1st, 2024 1 min read

NA SHABAN MAKOKHA

RAIS William Ruto anaongoza makala ya 61 ya sherehe za kitaifa za Madaraka Dei katika uwanja wa Masinde Muliro-Kanduyi katika Kaunti ya Bungoma.

Kiongozi wa nchi amewasili uwanjani humo dakika chache kable ya saa nne asubuhi ambapo alianza kwa kupungia wananchi mkono, kukagua gwaride la wanajeshi kabla ya kuwasalimia viongozi na kuketi kwa ajili ya burudani kabla ya kuanza kwa hotuba rasmi.

Maelfu ya Wakenya wamefurika uwanjani Masinde Muliro kwa ajili ya sherehe hizo za mwaka 2024.

Raia walianza kupiga foleni kuanzia saa kumi alfajiri ili kupata nafasi katika uwanja huo wenye uwezo wa kubeba watu 15,000.

Kumetundikwa skrini kubwa za runinga katika sehemu mbalimbali nje ya uwanja huo ili wale ambao hawataweza kuingia uwanjani waweze kufuatilia matukio.

Ni miaka 61 tangu Kenya kuwanza kujikomboa kutoka kwa wakoloni kutoka Uingereza.

Dkt Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua wameonyesha mshikamano sherehe zikinoga.

Baada ya maombi, kumekuwa na burudani aali na sasa kinachosubiriwa ni hotuba kutoka kwa viongozi.