Makala ya spoti- Pema Ladies FC

Makala ya spoti- Pema Ladies FC

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

HUWA ni jambo la kawaida kwa baadhi ya wachezaji wa soka hapa nchini kupewa majina ya wachezaji wanaosifika kulisakata soka la hali ya juu katika mataifa yanayotambulika kutoa wachezaji hao maarufu.

Kumezoeleka kutolewa majina ya wachezaji maarufu na kupewa wale ambao wanafananishwa nao huko ng’ambo. Kwa kawaida, majina hayo hupewa wanaume wanaocheza vizuri kwa kuwalinganisha na wanasoka hao wenye majina makubwa.

Lakini katika mji wa Mwatate uiloko Kaunti ya Taita Taveta kuna mwanasoka mwanamke anayecheza kabumbu la hali ya juu ambalo mashabiki wenyewe wanamlinganisha na kumpa jina la mchezaji maarufu wa Barcelona na Argentina, Lionel Messi.

Mwanadada huyo, Agnetta Mchana mwenye umri wa miaka 22 amebandikwa jina la Messi kutokana na jinsi anvyowachachafya mabeki wa timu pinzani kwa chenga na kufunga mabao mengi kwa timu yake ya Pema Ladies FC.

Agnetta aliyemaliza masomo ya kidato cha nne mwaka 2018 katika shule ya Ngami Secondary iliyoko eneo la Bura Mission, alionyesha kipaji cha uchezaji wake kwenye mechi ya ufunguzi ya timu yake ya Pema Ladies ilipoibebesha kapu la magoli Nyika Queens FC kwa mabao 8-0.

PICHA/ABDULRAHMAN SHERIFF

Katika mchezo huo uliochezwa uwanja wa Mwatunge mwishoni mwa wiki iliyopita, Messi huyo aliweza kuifungia timu yake mabao matano kati ya hayo manane na amepania kuhakikisha anamaliza Ligi ya Kaunti ya Tiata Taveta ya soka ya wanawake akiwa mshindi wa ‘Kiatu cha Dhahabu’.

“Nimepania kuhakikisha naibuka mfungaji bora kwani najiamini naweza kupambana na timu yoyote na kutamba. Ninataka kuwa mchezaji wa kuaminika na hata kuchaguliwa kuichezea timu ya taifa ya Harambee Starlets,” akasema Agnetta aliyewaomba wateuzi wa timu hiyo wafike kumuona.

Kwake anaamini timu yake hiyo ya Pema Ladies itaweza kuibuka washindi wa ligi hiyo ya kaunti na kuweza kupanda ngazi hadi Ligi ya jimbo la Pwani. “Nina hamu niisaidie timu yangu tupande kwani tukicheza ligi za juu tutaweza kuonekana,” akasema.

Agnetta anataka kuendeleza kipachi cha uchezaji afikie kucheza soka la kulipwa Ulaya. Yeye ni shabiki mkubwa wa straika wa Ureno, Ronaldo lakini kwa klabu anaipenda zaidi Manchester United ya England.

Kocha wa Pema Ladies FC, Peter Kinuthia anasema mbali na Agnetta, ana wachezaji mahiri ambao wakiendelea kucheza mechi za ligi ya kaunti, wataonekana na huenda hata klabu za Ligi Kuu zikawataka kuwasajili.

Wachezaji wengine wa timu hiyo ni nahodha Fatuma Musa, Susan Mtheu, Harriet Mutuku, Christine Mutua, Jesca Ndambi, Dorah Mwang’ombe, Morin Akinyi, Everlyne Akinyi, Agnes Wachia, Rodah Mwambi, Agnes Mchana, Agnes Mwachika, Mary Mwangemi na Sarah Mwikamba.

Kocha Kinuthia ameambia Taifa Dijitali kuwa changamoto kubwa waliyonayo ni ukosefu wa udhamini na akaomba wahisani wajitokeze ili kuwasaidia wasichana ambao wana nia ya kuinua vipaji vya ili watambulike na kucheza soka la kulipwa miaka ijayo.

“Wanasoka wangu wana moyo wa kutaka kuendeleza vipaji vyao ili wapate kuonekana na maofisa wa benchi la ufundi la Starlets ili nao wapate kuvaa jezi ya taifa leo,” akasema mkufunzi huyo mwenye nia ya kuipeleka timu yake hiyo hadi ligi kuu.

Nahodha Fatuma Musa anasema wameanza kwa ukali na watamaliza kwa makala zaidi. “Tuna imani kubwa kuwa tutatamba katika kila mechi tutakayocheza kwani tumelenga kuibuka washindi wa ligi hii,” akasema.

Katika mechi yao hiyo ya ufunguzi ya ligi ya kaunti hiyo ya Taita Taveta, wafungaji wengine waliotinga nyavu ni Everlyne Akinyi aliyefunga mabao mawili na Agnes Wachia akafunga bao moja.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Mbunge atilia shaka nyumba za Buxton ujenzi wazo ukiendelea...

WANDERI KAMAU: Waliopigania ukombozi wasipuuzwe