• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Abdul Haji afuata nyayo za waliorithi jamaa zao kisiasa

Abdul Haji afuata nyayo za waliorithi jamaa zao kisiasa

Na NYAMBEGA GISESA

ALIPOWEKA maisha yake hatarini kwa kuingia ndani ya Jumba la Kibiashara la Westagate, Nairobi, 2013 kuokoa watu waliokwama huku wakati wa shambulio la kigaidi, Abdikadir Haji, maarufu kama Abdul Haji, hakujua kuwa kitendo hicho kingebadilisha maisha yake.

Picha ya Abdul akiwa ameinua bastola huku akiwasaidia waliokwama katika jengo hilo, haikumwezesha tu kupata tuzo kutoka kwa rais pekee, bali imeimsaidia kupata baraka za wazee kama anayefaa kuwa Seneta wa Kaunti ya Garissa.

Wazee walisema kuwa baba huyo wa wasichana wanne, ndiye aliyekuwa mwenye ujasiri zaidi miongoni mwa wale waliotaka kujaza nafasi hiyo iliyosalia wazi kufuatia kifo cha babake, Seneta Yusuf Haji, mnamo Februari 15.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inatarajiwa kumtawaza Haji kama mshindi wa kiti hicho kwani kufikia Alhamisi hakukuwa mgombeaji mwingine ambaye alikuwa amewasilisha stakabadhi zake akitaka kushiriki katika uchaguzi huo mdogo.

Alhamisi ilikuwa siku ya mwisho kwa wagombeaji kuwasilisha stakabadhi hizo kwa afisi za IEBC mjini Garissa kuidhinishwa kwa uchaguzi huo ambao umeratibiwa kufanyika Mei 18, 2021.

“Baada ya kupokea karatasi za uteuzi kutoka kwa mgombeaji mmoja pekee, nimewasilisha habari hiyo kwa makao makuu ya IEBC ili tume ifanye uamuzi,” Afisa Msimamizi wa uchaguzi kaunti ya Garissa Hussein Gure akaaambia Taifa Leo.

Bw Gure alisema amekamilisha kazi yake kama Afisa Msimamizi wa Uchaguzi kwani hakutakuwa na uchaguzi mdogo baada ya mgombeaji huyo kukosa wapinzani.

Haji anakuwa mwanasiasa wa tatu kuchaguliwa bila kupingwa katika uchaguzi mdogo baada ya Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi.

Kufuatia kifo cha babake Moses Mudavadi- aliyekuwa Waziri mwenye ushawishi mkubwa katika serikali ya marehemu Rais Daniel Moi- mnamo 1989, Bw Mudavadi alichaguliwa bila kupingwa kama mbunge wa Sabatia kuchukua nafasi ya babake.

Mnamo 2014, Bw Kuria pia alichaguliwa bila kupingwa wakati mpinzani wake mkuu, Bw Kiarie Kamere wa chama cha New Democrats, alipojiondoa kutoka uchaguzi mdogo wa Gatundu Kusini.

Uchaguzi huo mdogo ulitokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Joseph Ngugi Nyumu.Katika kaunti ya Garissa ambapo siasa za ukoo huwa na usemi katika chaguzi, Bw Haji amefaulu kupata uungwaji mkono kutoka kwa wazee wote kutoka koo kubwa.

Mnamo Jumanne, mwana huyo wa marehemu seneta alikutana na jopo la wazee wanaoheshimika zaidi, ‘Samawadhal Sagaales’ katika makazi yake mjini Garissa.

“Wazee wa ukoo wana wajibu mkubwa katika kuleta amani na uwiano miongoni mwa jamii. Ilikuwa ni furaha yangu kutambua baraka, hekima na tajriba ya wazee,” Haji akasema baada ya kukutana na wazee hao.

Bw Haji alipata uidhinishwaji kutoka wa koo za Abduwak, Aulihan na Abdalla kwamba ndiye anayefaa kuchukua nafasi ya babake kama seneta. Koo hizo tatu zina ushawishi mkubwa katika siasa za Garissa.

Bw Haji aliidhinishwa na IEBC Jumanne kuwania kiti hicho baada ya kuwasilisha karatasi zake za uteuzi kwa Afisa Msimamizi wa Uchaguzi kaunti ya Garissa Bw Gure katika Chuo Anuai Kitaifa cha North Eastern.

Aliandamana na viongozi kadha, miongoni mwao akiwa Gavana wa Garissa Ali Koran, Naibu Gavana Abdi Dagane, Mbunge wa Ijara Sophia Abdinoor, aliyekuwa Gavana wa Garissa Nathif Jama, aliyekuwa Naibu Gavana wa Garissa Abdullahi Hussein na madiwani kadhaa.

Kabla ya hapo, alikuwa amepata uungwaji mkono kutoka kwa chama cha ODM baada ya kukutana na kushauriana na naibu kiongozi wa chama hicho Gavana wa Mombasa Hassan Joho. Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto pia kiliahidi kumuunga mkono kwa kutodhamini mgombeaji katika uchaguzi mdogo.

Bw Haji, ambaye ni mfanyabiashara, alijulikana kwa mara ya kwanza wakati wa shambulio la kigaidi katika jumba la kibiashara la Westgate, katika mtaa wa Westlands, Nairobi mnamo 2013.

Aliingia ndani ya jengo hilo kumwokoa kakake mkubwa Noordin Haji, sasa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP), ambaye ni miongoni wa waliokwama katika jengo hilo baada ya shambulio hilo lililotekelezwa na wafuasi wa kundi la Al Shabaab.

Mfanyabiashara huyo, ambaye amekuwa akifanya mazoezi ya kulenga shabaha eneo la Athi River, aliwaokoa watu kadha kutoka jengo hilo, wakiwemo watoto.

Bw Haji, mwanamume mwingine, ambaye hakutambuliwa, na maafisa watatu wa polisi, wakiwa na bunduki aina ya AK47, waliingia ndani ya jumba hilo la kibiashara na kuwaokoa watu waliokuwa wamejificha ndani ya mkahawa wa Java, wakihofia maisha yao.

Ni miongoni mwa watu waliofika katika eneo la tukio kwanza, hatua iliyomfanya kuchukuliwa kama mmoja wa mashujaa katika mkasa huo.Baada ya kuchaguliwa bila kupingwa, Bw Haji sasa anajiunga na orodha ya wale waliorithi viti vya kisiasa kutoka kwa jamaa zao, mtindo unaoendelea kujenga familia za kisiasa.

Katika uchaguzi mdogo eneobunge la Msambweni mwishoni mwa mwaka jana, Feisal Bader, mpwaye aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo Suleiman Dori, alishinda na kumrithi kwenye kiti hicho.

Bader ambaye pia amekuwa meneja wa afisi ya hazina ya eneobunge la Msambweni tangu 2013, aliwania kiti hicho kama mgombea huru, japo alifanyiwa kampeni na wanasiasa wa mrengo wa Tangatanga, ambao ni wandani wa Dkt Ruto.

Katika uchaguzi wa useneta wa Machakos wiki jana, mgombeaji wa Wiper Agnes Kavindu Muthama, ambaye ni mkewe (waliotengana) aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnston Muthama, alichaguliwa kuchukua mahala pa Seneta Boniface Kabaka, aliyefariki Desemba 15 mwaka jana baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Kabla ya seneta Kabaka kiti hiki kilikuwa kimeshikiliwa na Johnson Muthama.Vile vile, katika uchaguzi mdogo wa Bonchari, Kisii, chama cha UDA kimemdhamini Bi Teresa Bitutu, mkewe aliyekuwa mbunge wa eneo hilo John Oyioka.

Uchaguzi huo mdogo umeratibiwa kufanyika mnamo Mei 18, 2021.Marehemu gavana wa Bomet Joyce Laboso, alimrithi dadake Lorna Laboso kama mbunge wa Sotik mnamo 2008.

Lorna alifariki katika ajali ya ndege katika eneo la Enoosupukia, Narobi.Naye Bi Beatrice Kones alichaguliwa kwa mara ya kwanza kama mbunge kufuatia kifo cha mumewe, aliyekuwa Waziri Kipkalya Kones katika ajali hiyo hiyo iliyomuua Lorna Laboso.Hii ni mifano michache tu ya watu ambao wamewahi kurithi viti vya kisiasa vilivyoshikiliwa na jamaa zao waliofariki.

You can share this post!

Pasaka chungu kwa wakazi wa kaunti tano

Askofu ataka serikali ichanje Wakenya wote