• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
Dogo wa umri wa miaka 10 kuhutubia kongamano la tabianchi la ACS23

Dogo wa umri wa miaka 10 kuhutubia kongamano la tabianchi la ACS23

BONIFACE MWANGI Na WINNIE ONYANDO

KIJANA Nigel Waweru, mwenye umri wa miaka 10, ameteuliwa kuhutubu katika kongamano la mabadiliko ya tabianchi Afrika ambalo litafanyika jijini Nairobi wiki ijayo.

Kongamano hilo linalofahamika kama Africa Climate Summit (ACS23), litaanza rasmi Septemba 4 hadi Septemba 6, 2023.

Wakuu wa Nchi mbalimbali akiwemo mwenyeji Rais William Ruto, watahudhuria.

Haya yanajiri miezi michache baada ya Wizara ya Mazingira kumteua ‘dogo’ Waweru kuwa balozi wa mazingira.

Lakini nia ya mwanamazingira, ustahimilivu na bidii yake ya kuhamasisha watu kuhusu hatari ya kutupa ovyo chupa za plastiki zilizotumika bila uangalifu vilizaa matunda zaidi, baada ya kuwashinda zaidi ya watoto 30 na kuibuka ‘Bw Mazingira Mdogo’.

“Hii ni fursa adimu na matumaini na matarajio yangu ni kwamba watu watapata ujumbe na kukumbatia mabadiliko yanayolenga kuifanya dunia kuwa pahala salama,” kijana Waweru akaambia Taifa Leo kwenye mahojiano baada ya kupata taji hilo.

Hafla hiyo ya siku tatu iliyofanyika katika hoteli ya Weston jijini Nairobi mnamo Jumamosi iliyopita na iliyokuwa na kaulimbiu ‘Tuangamize Uchafuzi wa Mazingira kwa Plastiki’ ilivutia zaidi ya watoto 30 kutoka kaunti zote 47.

Ni hapa ambapo Waweru alifanikiwa kuwashinda wenzake alipoonyesha ubunifu wake – ule wa kutumia chupa za plastiki kupitisha ujumbe wa kuwamasisha umma juu ya hatari ya kutupa plastiki zilizotumika kiholela.

Si hivyo tu, juhudi na ujasiri wake wa kuzuru shule kadhaa kuelimisha wanafunzi wenzake kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira pia ni miongoni mwa maswala yanayomzolea sifa.

Mafanikio haya yalilazimu Wizara ya Mazingira kumjumuisha Waweru kama mmoja wa mahatibu, ambao watahutubia wajumbe katika kongamano hilo.

Safari yake ya uhifadhi wa mazingira ilianza akiwa na umri wa miaka sita pekee alipojionea rundo la taka limeziba mitaro ya majitaka kwenye mtaa wao Nakuru.

“Mafundi wa kuzibua mitaro waliniambia nyingi ya taka hizo huishia kwenye Ziwa Nakuru na kwamba ni hatari kwa samaki na viumbe wengine wanaoishi kwenye maji. Nilisikitika sana,” anakumbuka.

Tangu wakati huo, amekuwa akitazama vipindi vya mazingira vinavyopeperushwa kwenye runinga.

Nigel Waweru, mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Shah Lalji Nangpar Academy Nakuru, ambaye ni balozi wa mazingira wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN). PICHA | RICHARD MAOSI

Wikendi akiwa hajaenda shuleni, hujiunga na wanamazingira kukusanya taka.

“Siku moja nikifanya usafi katika mtaa wa Pipeline katika jiji la Nakuru, wazo lilinikujia kutumia vifuniko vya chupa za plastiki, ambazo zenyewe ni kero, kuziweka kwa vipande vya boksi kueneza ujumbe mzuri,” anasema.

Mwanzoni alimweleza mama yake, Bi Yvonne Anisah, nia ya kuzamia katika masuala ya uhifadhi wa mazingira. Siku za mwanzo, mamake alipuuza wazo hilo.

Ilibidi kijana kumwambia mwalimu wake wa darasa kumuita Bi Anisah shuleni na kumfafanulia wajibu muhimu wa uhifadhi wa mazingira.

Tangu wakati huo, mamake Nigel anamuunga mkono.

Kijana huyo ana ujumbe kama vile ‘Think before you drink’ yaani ‘Fikiri kabla ya kunywa’.

Ujumbe mwingine ni ‘Tukinge mazingira yetu dhidi ya taka za plastiki’.

  • Tags

You can share this post!

‘Simba jike’ wa Kiambu amuonya Wamatangi

Mwanzo mpya

T L