• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Hii ni kwa wanaonyonyesha na inawabidi kuenda kazini

Hii ni kwa wanaonyonyesha na inawabidi kuenda kazini

NA MAUREEN ONGALA

MSHIRIKISHI wa maswala ya afya ya uzazi katika Kaunti ya Kilifi Bw Kenneth Miriti amewahimiza akina mama wanaofanya kazi wawe wakikama na kuyahifadhi maziwa ili watoto wao wapate chakula hicho muhimu.

Bw Miriti alizungumza na wanahabari afisni mwake katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kilifi huku wakijumuika na nchi nyingine kuadhimisha wiki ya kunyonyesha ulimwenguni. Ilikuwa ni wiki jana.

Alisema kuwa serikali ya kaunti ya Kilifi inaendelea kufanya hamasisho kwa akina mama ambao wanafanya kazi kuhusu umuhimu wa kuwanyonyesha watoto hata baada ya ile miezi mitatu ya likizo wanayopatiwa wanapojifungua.

“Hamasisho huhitajika sana kwa sababu kila mara kuna wakati mama atahitaji mtu wa kukaa na mtoto akiwa kazini na tunawaambia kuwa sio lazima watoke kazini ama waende na watoto kazini lakini anaweza kuyakama maziwa na kuweka katika chombo safi ili mtoto aweze kupewa anapohitaji,” akasema.

Bw Miriti alisema hata hivyo kuna manufaa mengi iwapo mtoto atanyonya matiti ya mamake ikiwemo kuimarisha uhusiano kati ya mama na mtoto na pia kama njia ya kupanga uzazi.

Wakati huo huo, Bw Miriti pia aliwahimiza akina mama ambao wana maziwa mengi ama wamepoteza watoto wao kukama maziwa na kuwapa watoto wengine ambao pengine akina mama wamefariki ama hawako karibu.

“Hii ni tabia ambayo haijakumbatiwa sana nchini lakini mataifa mengine yanaendeleza kama njia mojawapo ya kuwapa watoto maziwa ya matiti. Bora mama awe hana magonjwa, jambo la muhimu ni kwamba tunawahimiza akina mama kutumia kikombe na kijiko ili kuepusha magonjwa ya kuharisha na hata vifo,” akasema.

Bw Miriti alisema kuwa katika kaunti ya Kilifi, akina mama wakubwa kiumri huwanyonyesha watoto ambao wamefiliwa na mama zao.

“Nyaya hao huchukua mtoto na kumweka kwenye titi na akianza kuvuta maziwa yanaanza kutoka, na hii ni tabia ambayo inafanyika sana Kilifi,” akasema.

Alisema watawapa kipaumbele wafanyikazi katika idara ya afya katika hospitali kubwa saba za kaunti hiyo ambapo watajengewa sehemu za kunyonyoshea watoto wao.

“Tunataka kuwapa wafanyakazi wetu nafasi nzuri ya kuwanyonyesha watoto wao hata wakiwa kazini kwa afya bora ya watoto,” akasema.

Alisema kuwa takwimu za kitaifa zinaonyesha ya kwamba asilimia 52 ya wanawake ambao wanafanya kazi hawana nafasi ya kunyonyesha watoto kwa miaka miwili, kipindi ambacho kinafaa.

“Tunaweza kutatua changamoto hii kupitia kwa hamasa kwa akina mama ambao wanafanya kazi na pia kuwa sehemu maalum za kufanyia kazi wakiwa na watoto wao,” akasema.

Kulingana na Bw Miriti, hatua hiyo pia itatatua changamoto ya lishe bora ambapo wazazi wengi hawawezi na pia serikali ya kaunti haiwezi kumudu kununua tembe hizo kwani ni ghali.

Idara ya afya imehakikisha kuwa imeweka jumbe kuhusu umuhimu wa kunyonyesha katika hospitali wakilenga kuwafikia akina mama wengi ambao wanaenda kliniki zao.

Bw Miriti alisema serikali ya kaunti inalenga kushirikiana na shirika la UNICEF miongoni mwa wadau wengine kuwapa mafunzo hayo wamiliki wa sehemu za kuwalinda watoto mchana na shule za chekechea pia kuwa na sehemu za kunyonyesha watoto hao katika kila kituo.

Aliwataka wanaume kuwa karibu na wake zao wanapowanyonyesha watoto ili kuimarisha uhusiano kati ya mama na mtoto.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Ulanguzi wa dawa za kulevya ulifanya mzungu kunitema

CHARLES WASONGA: Matamshi ya Ruto, Raila yasivuruge...

T L