• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
SHINA LA UHAI: Hatari, tija za mwanamke kujifungua akiwa na umri wa zaidi ya miaka 40

SHINA LA UHAI: Hatari, tija za mwanamke kujifungua akiwa na umri wa zaidi ya miaka 40

NA PAULINE ONGAJI

PINDI baada ya pacha wake watatu kuzaliwa mwezi wa Aprili, Bi Purity Toyian, 42, aligundulika kuugua deep vein thrombosis (DVT) (mgando wa damu unaojiunda kwenye mishipa ya damu mwilini) kwenye mguu wake wa kushoto.

Lakini kwa bahati nzuri, tatizo hili liligundulika mapema na hivyo akaanza matibabu mara moja.

Tukio hili lilitokea kabla ya Bi Toyian kuruhusiwa kwenda nyumbani kufuatia kujifungua kwake.

“Baada ya kujifungua nilikaa siku zaidi hospitalini na mwishowe nilikuwa salama kwenda nyumbani, lakini daktari alitoa masharti makali dhidi ya kusafiri kwa muda mrefu.”

Kisa cha Bi Toyian ni cha kipekee, lakini kulingana na Dkt Saudah Farooq, mwanajinakolojia katika hospitali ya Nairobi West Hospital, wanawake waliozidi umri wa miaka 40 wako katika hatari kubwa ya kukumbwa na changamoto wakati wa kujifungua, hasa pacha.

Kata tamaa

Bi Toyian na mumewe Bw Charles Makau, walikuwa wamekata tamaa ya kupata watoto zaidi, baada ya kujaribu kwa miaka.

Hii ilikuwa kufuatia kuzaliwa kwa binti yao wa pili ambaye kwa sasa ana umri wa miaka minane.

“Mtoto wetu wa kwanza mwenye umri wa miaka 12, anakumbwa na tatizo la utindio wa ubongo (cerebral palsy), na hivyo baada ya mtoto wetu wa pili kuzaliwa, tulionelea haja ya kuahirisha ndoto za kupata watoto zaidi hadi baadaye. Lakini hatukujua kwamba ngoja ngoja yetu ingetuletea shida kwani muda ulikuwa unayoyoma, na hivyo tulipofanya maamuzi ya kuongeza mtoto, sasa tukaanza kukumbwa na ugumu,” aeleza Bw Makau.

Kulingana na Bi Toyian, matatizo ya kushika mimba yalimshangza kwani awali hakukumbwa na changamoto yoyote wakati wa kushika mimba za watoto wao wawili wa kwanza.

“Wasi wasi huu ulinisukuma mwaka wa 2021 kutafuta huduma za mtaalam wa masuala ya uzazi, aliyenishauri kuanza kutumia vijalizo, ambavyo nilivitumia tu mara moja,” aeleza.

Pacha watatu

Oktoba 2022, ngoja ngoja yao ilifikia kikomo kwani Bi Toyian alithibitishwa kuwa na mimba ya pacha watatu.

Licha ya umri wake, asema kwamba, hakuwa na tatizo wakati wa ujauzito, kiwango cha kwamba hakugundua kwamba alikuwa na mimba hadi alipoanza kuugua.

“Nilienda hospitalini na hata nikalazwa nikidhani kwamba nilikuwa mgonjwa, lakini picha za skeni zilithibitisha kwamba nilikuwa mjazito.”

Kulingana naye, kipindi chote cha ujauzito hakikukwa na tatizo japo tu kwa matatizo madogo hapa na pale alipokuwa anakaribia kujifungua.

“Ilikuwa imeratibiwa kwamba afanyiwe upasuaji mwezi Mei 8, lakini akaanza kukumbwa na ishara za kujifungua Aprili 20. Kwa hivyo ilikuwa lazima asafirishwe na ambulenzi kutoka Kajiado hadi jijini Nairobi kwa upasuaji huo,” asema Bw Makau.

Watoto wadogo walizaliwa mapema na hivyo ilikuwa lazima wapelekwe kwenye wadi ya watoto wagonjwa mahututi, ambapo walikaa kwa wiki nne kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani.

“Tokea hapo, hali yao ilikuwa ikifuatiliwa na walikuwa wakilishwa ili kuongeza uzani,” aongeza Bi Toyian.

Kwa kawaida, Dkt Wachira Murage, mwanajinakolojia katika hospitali ya Savannah, jijini Nairobi, asema, kuzaa pacha kuna hatari pasipo kuzingatia umri.

“Tatizo kuu la kuzaa pacha ni mama kushuhudia maumivu ya uzazi mapema. Kuna uwezakano mkubwa wa mama kuanza kushuhudia uchungu wa uzazi kabla ya mimba kutimu wiki 37,” aeleza.

Charles Makau na mkewe Purity Toyian wakibeba pacha wao watatu nyumbani Lower Kabete mnamo Juni 3, 2023. PICHA | EVANS HABIL

Aidha, kulingana na Dkt Murage, tatizo la kijusi kukua vyema tumboni (fetal growth restriction) pia hushudiwa sana.

“Hali hii hutokea ambapo mtoto tumboni hakui katika kiwango cha kawaida. Hii yaweza sababisha watoto kuzaliwa mapema au wakiwa na uzani wa chini.”

Pia, aongeza kwamba huenda tatizo la placenta abruption pia huenda likashuhudiwa.

“Hii ni hali ya dharura ambapo mji hujiondoa kwenye ukuta wa uterasi kabla ya mtoto kuzaliwa. Aidha, kuna uwezekano wa kukumbwa na shinikizo la damu wakati wa ujauzito.”

Kwa ujumla, Dkt Saudah anaeleza kwamba, japo hatari hizi za kiafya na zingine zinahusishwa na ujauzito wa pacha pasipo kuzingatia umri, wanawake waliozidi miaka 40, wamo katika hatari kubwa.

“Kwa mfano, shinikizo la damu huongezeka wakati wa ujauzito ikiwa uko katika miaka ya 40, na hii yaweza geuka na kuwa maradhi ya kudumu.”

Kwa hivyo, hii inamaanisha nini kwa wanawake wanaoamua kuanza familia baada ya kutimu miaka 40?

Tafiti zimeonyesha kwamba visa vya wanawake waliozidi miaka 40 kuzaa pacha hasa hapa barani vinaendelea kuongezeka.

“Takwimu uliwenguni zinaonyesha kwamba uwezekano wa mwanamke kuzaa pacha huongezeka hadi kufikia miaka 43, kabla ya kupungua tena anapopita umri huu. Kwa wanawake chini ya miaka, uwezekano wa kushika mimba ya pacha ni asilimia 0.3. Kwa upande mwingine, uwezekano wa wanawake kati ya miaka 25 na 34 kubeba pacha ni asilimia 1.4, huku kwa wanawake kati ya miaka 34 na 39, uwezekano huo ukiwa asilimia 3, na asilimia 4 kwa wanawake walio katika miaka ya arubaini,” aeleza Dkt Saudah.

Kulingana na mtaalamu huyu, kuna baadhi ya nadharia zinazoeleza baadhi ya masuala ambayo huenda huchochea hili miongoni mwa wanawake wa umri huu. Moja yazo, asema, ni mayai kujihifadhi.

“Kutokana na sababu kuwa ubora wa mayai hupungua umri unavyozidi kuongezeka, kuna uwezekano wa wanawake hawa kutoa mayai mara mbili. Kwa kiwango fulani, mzunguko hautabiriki baada ya miaka 40, na hivyo, kuna baadhi ya miezi ambapo mayai hayatatolewa, ilhali miezi mingine yatatolewa mara kadhaa.”

Matumizi ya dawa

Kulingana na Dkt Saudah, pia matumizi ya dawa za kuimarisha uwezo wa kuzaa ni sababu ingine ambayo huongeza visa hivi.

“Hii ni ambapo teknlojia ya kusaidia kutungisha mimba ART inatumika. Hii huhusisha matumizi ya dawa za kumeza au kudungwa ili kuchochea nyumba za mayai kutoa zaidi yai moja, na hivyo huenda zikatoa mayai mawili au matatu kulingana na dozi unayopokea au hali ya mhusika.”

Aidha, asema, mhusika anaweza fanyiwa utaratibu wa urutibishaji wa in vitro fertilization (IVF), ambao kwa kawaida huhusisha kuhamisha zaidi ya yai moja lililorutubishwa hadi kwenye yuterasi ya mhusika.

“Ikiwa wanahamisha zaidi ya yai moja, basi kuna uwezekano wa kushika mimba ya pacha,” aeleza.

Kwa hivyo, Dkt Saudah asema, huku idadi ya wanawake wanaoamua kuchelewa kupata watoto kwa sababu za kitaaluma ikiendelea kuongezeka, hii inamaanisha kwamba tutaendelea kushuhudia ongezeko la idadi ya wanawake zaidi ya miaka 40 wanaojifungua mapacha.

Na japo wataalam wanaonya kuhusu hatari zinazohusika hapa, kwa upande mwingine, wanakiri kwamba kuna manufaa kwa mwanamke kuzaa akishatimu miaka 40.

“Kwa kawaida, wakati huu mwanamke amekomaa kustahimili changamoto zinazoambatana na uzazi, kama vile mzigo wa kifedha. Pia, wakati huu, kuna uwezekano mkubwa kwamba mwanamke amefaya utafiti wake vilivyo na ana tajriba ya uzazi kwa sababu huenda una watoto wengine,” aeleza Dkt Saudah.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume ataka arudishiwe mkono wake uliokatwa miaka 16...

Brown Mauzo atangaza kutengana na Vera Sidika

T L