• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
SHINA LA UHAI: Ongezeko la taka za kielektroniki tishio kwa afya na mazingira

SHINA LA UHAI: Ongezeko la taka za kielektroniki tishio kwa afya na mazingira

NA PAULINE ONGAJI

HUKU ulimwengu ukiendelea kushuhudia ustawi mkuu wa teknolojia, kwa upande mwingine, maendeleo haya yamesababisha uzalishaji mkuu wa taka za kieletroniki (e-waste).

Taka hizi zinahusisha bidhaa za kieletroniki zisizohitajika tena au zinazokaribia kikomo cha kipindi cha matumizi.

Zinahusisha kompyuta, vipakatalishi, simu za rununu na vifaa vingine vya kielektroniki nyumbani, kama vile televisheni na friji.

Mwaka wa 2019, tani milioni 53.6 za taka za aina hii zilizalishwa duniani kote, na takwimu hizi zinaendelea kuongezeka.

Kulingana na Mpango wa Mazingira wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UNEP), kiwango hiki kinatarajiwa kuongezeka maradufu kufikia mwaka wa 2050, ikiwa hatua za dharura hazitachukuliwa.

Kulingana na Bw Kevin Lunzalu, mwanaekolojia wa baharini, taka za kieletroniki zina athari kuu za kiafya na kimazingira, na kuongezeka kwake ni tishio kwa uhai wa wanyama na binadamu, vile vile usalama wa kimazingira.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Kituo cha Vifaa vya Umeme na Elektroniki (WEEE) Bonface Mbithi akizungumza kuhusu mpango wa urejelezaji wa taka za kielektroniki kwenye warsha awali mtaani Utawala, Nairobi. PICHA | FRANCIS NDERITU

Ni suala hili lililomsukuma Bw Bonface Mbithi kuanzisha kampuni ya Waste Electrical and Electronics Equipment (WEEE) Centre, inayohusika na utengenezaji upya bidhaa za kielektroniki.

“Kampuni hii inayoendesha shughuli zake katika mtaa wa Mihango, Kaunti ya Nairobi, imekuwa ikitengeza upya taka za kieletroniki kama vile kompyuta zilizoarabatiwa na kutolewa kama msaada kwa taasisi za masomo,” aeleza Bw Joseph Oliech, msimamizi wa miradi katika kampuni ya WEEE Center.

Kwa upande mwingine, vifaa vilivyoharibika huvunjwa kisha sehemu zake kama vile plastiki, kebo, chuma, motherboard na betri zinaondolewa.

Kituo cha kusaga plastiki

Hapa kuna kituo maalum cha kusaga plastiki zilizokusanywa kutokana na taka hizi, ambapo vidonge vinavyopatikana baada ya utaratibu huu hutumika kutengeza bidhaa kama vile nguzo za ua.

“Aidha, bidhaa nyingine hatari kama vile zebaki, risasi na kemikali zinazopakwa kwenye vifaa ili kuzuia kuungua au kupunguza kasi ya kuenea kwa moto (flame retardants), zinaondolewa kwa utaratibu na njia salama,” aongeza Bw Oliech.

Kampuni hii pia inashughulikia kemikali hatari zinazopatikana kwenye vifaa va kieletroniki.

Kwa mfano, kuna karakana maalum ya kuunda upya aina mbali mbali za betri, na kuondoa elementi zenye thamani, kwa matumizi mapya.

“Betri huwa na kemikali na aina kadha wa kadha za chuma zenye sumu, na hivyo zinapotupwa kiholela, husababisha madhara kwa mazingira, maji na udongo,” aeleza Bw Oliech.

Zile bidhaa ambazo haziwezi tengezwa upya, kama vile motherboard na sehemu za friji, zinasafirishwa hadi Ulaya ambapo kuna mbinu za kisasa za kukabiliana na aina hii.

Kwa sasa kampuni hii hushughulikia kati ya tani 20-25 za taka za kieletroniki kila mwezi, ambapo katika harakati hizi, kampuni hii inazuia hatari na athari kuu za kiafya na kimazingira, sasa na siku za usoni.

Nchini Kenya, ni asilimia moja pekee ya tani 51.3 za taka za kieletroniki zinazozalishwa kila mwaka, ambazo hutengezwa upya.

Duniani, takriban asilimia 20 pekee ya taka hizi hutengezwa upya, na kulingana na UNEP, zilizosalia hutupwa kiholela.

Kulingana na Bw Lunzalu, taka za kieletroniki hazivunjiki kwa urahisi, na hivyo endapo hazitashughulikiwa kwa njia inayofaa, zinasababisha hatari kubwa kwa afya na mazingira.

Kulingana na Sammy Simiyu, mtaalamu wa masuala ya kiafya, kuwa wazi kwa viwango vikubwa vya uchafu unaopatikana kwenye taka za kieletroniki kwa sasa unajitokeza kupitia maradhi mbali mbali.

Kwa mujibu wa Shirika la Afa Duniani (WHO), uchafu unaotokana na taka za kieletroniki umehusishwa na madhara ya kiafya kama vile uharibifu wa sehemu za mwili kama vile ubongo, ini, figo na mifupa.

Hatari ni kubwa kwa watoto

Kulingana na wataalam, kwa watoto wadogo, hatari ni kubwa hata zaidi kwani miili yao midogo hufyonza sumu kutoka kwenye taka hizi kwa kasi, ilhali sumu hii huondoka kwenye mfumo wa mwilini polepole. Kwa mama mjamzito, kemikali hizi zina athari za kudumu kwa afya ya mtoto tumboni. Baadhi ya athari ni pamoja na mtoto kuzaliwa akiwa amekufa au kabla ya wakati kutimia.

Madhara mengine kwa afya ya watoto ni pamoja na mabadiliko ya shughuli za mapafu, athari kwenye mfumo kupumua, mabadiliko ya shughuli za kikoromeo na ongezeko la hatari ya kukumbwa na baadhi ya maradhi ya kudumu kama vile kansa na maradhi ya moyo.

Lakini kando na athari kwa afya, taka hizi pia zinasababisha uharibifu mkubwa kwa mazingira.

Sumu

Kulingana na Bw Lunzalu, taka hizi za kieletroniki zinapokuwa wazi kwa joto, huzalisha kemikali hatari na kuziachilia hewani.

“Kisha kemikali hizi zenye sumu hupenyeza kwenye udongo na kuingia kwenye maji ya ardhini na baharini, na hivyo kuathiri afya ya wanyama na mimea,” aeleza Bw Lunzalu.

Aidha, kulingana na mtaalam huyu, chuma hatari kama vile risasi, cadmium, thallium, arsenic, na beryllium zinazotokana na taka hizi na kupenyeza kwenye udongo, huingia kwenye mimea na hivyo kusababisha uharibifu sio tu kwa mimea, bali pia madhara ya kiafya kwa wanyama watakaoila.

  • Tags

You can share this post!

Mhubiri atupwa ndani kwa kupatikana na chang’aa

Barabara zote zaelekea Nyayo warembo wa Harambee Starlets...

T L