• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Vifaabebe kwa watoto wachanga huwacheleweshea uwezo wa kuongea, wanasayansi wasema

Vifaabebe kwa watoto wachanga huwacheleweshea uwezo wa kuongea, wanasayansi wasema

NA MARY WANGARI

HUKU wanasayansi wakionya dhidi ya matatizo ya kiafya yanayosababishwa na mazoea ya kuwaruhusu watoto kuwa na muda mwingi wakitazama vifaa vya kielektroniki kama vile simu, TV, tarakilishi na vinginevyo, James ambaye ni baba wa watoto wawili anafahamu fika athari zake.

James na familia yake changa walipomkaribisha mtoto wao wa kiume miaka sita iliyopita, walijawa na furaha isiyo na kifani. Malaika huyo mchanga ndiye waliyehitaji kukamilisha familia yao changa.

Wazazi hao pamoja na binti yao kifunguamimba, walisubiri kwa hamu na ghamu kusherehekea kila hatua ya mwana wao kuanzia tabasamu lake la kwanza litakalochanua usoni mwake, atakapojua kuketi, kutembea na zaidi kutamka neno lake la kwanza!

Kadri mtoto wao alivyozidi kukua ndivyo walivyogundua alipenda sana kutazama runinga na simu za wazazi wake ambapo angeangua kilio endapo yeyote angejaribu kubadilisha kipindi chake cha vibonzo.

“Alikuwa anapenda kupindukia kituo cha Cocomelon, hasa wimbo wa ‘Baby Shark doo doo’. Ungempokonya simu au kubadilisha kipindi chake kwenye mtandao wa Youtube alikuwa analia sana usiweze kumtuliza,” anasimulia James.

Mtoto wao alipofikisha umri wa miaka mitatu kipindi cha janga la Covid-19 mnamo 2020, ndipo walipoanza kuona yote hayakuwa shwari.

Hali kwamba James alikuwa kipindi hicho akifanya kazi na Daughters of Charity Thigio, shule maalum ya watoto walemavu, ilifanya iwe rahisi kwake kugundua dalili za kuchelewa kuzungumza au tawahudi (autism).

Taasisi hiyo huwatunza watoto wanaougua tawahudi au walio na matatizo ya kuchelewa kuzungumza.

“Niligundua mwanangu ana tatizo na maendeleo yake ya kuzungumza mnamo 2020 wakati wa janga la virusi vya corona. Alikuwa anaelekea miaka mitatu,” anasimulia.

“Hakuwa anaitika jina lake lilipoitwa, macho yake yalikuwa hayatazami mtu moja kwa moja, alikuwa anacheza pekee yake hata wakati dada yake au watoto wa jirani walipokuwa karibu. Angepanga vifaa vyake vya kuchezea kwenye foleni moja sambamba na alikuwa anamwita kila mtu mama alipohitaji usaidizi.”

Wazazi walijaa na hofu huku mikakati ya kufunga shughuli zote, usafiri na hata shule kutokana na janga la Covid-19 lililotikisa dunia, ikiwatonesha kidonda zaidi.

“Tulizidiwa na wasiwasi. Haingewezekana kupata mtaalam wa kumfanyia vipimo vya kimatibabu. Wataalam katika Taasisi ya Elimu ya Walemavu Nchini (KISE) walikuwa wamefunga kutokana na virusi vya corona. Hatungeweza kusafiri katika Hospitali ya Gertrude au hata Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) ambapo nilikuwa nimeshauriwa na mwalimu wa walemavu kazini. Marufuku ya kusafiri ilinizuia,” anaeleza.

Babu na nyanya walijawa na wasiwasi kuhusu hali ya mkujuu wao kuchelewa kuongea huku wakitamani kuzungumza naye lakini waliitia moyo familia hiyo wakiwakumbusha kwamba “kila mtoto ni tofauti na mwenzake na hukua kwa njia tofauti vilevile.”

Hata hivyo, jinamizi kuu lilikuwa kukabiliana na marafiki na wanajamii kwa jumla jinsi James na familia yake walivyobaini kwa mshtuko mkubwa.

Baadhi ya marafiki kwa hekima au kukosa hekima waliamua kuisuta familia hiyo ambayo tayari ilikuwa imezongwa na mafadhaiko.

“Nilichelea kuwaeleza marafiki zangu kuhusu kilichokuwa kinaendelea kwa sababu wengi wao walinipuuzilia mbali wakisema, ‘ni kwa sababu huzungumzi na mtoto wako, huwa hauruhusu mtoto wako atoke nje kucheza na mengine mengi. Sikuwa na nguvu wakati huo ya kusikiza shutuma au matamshi hasi yoyote.”

Kwa sadfa, marafiki zake wawili walikuwa wanapambana na masaibu sawa na yake kuhusu watoto wao kuchelewa kuzungumza na hili lilimfariji walipoungana kuhimizana.

“Mmoja wetu aliyejiweza kifedha alikuwa anamlipa mtaalam wa kuzungumza kuja kwake mara kwa mara. Yule mwingine alilazimika kusafirisha familia yake kuishi kijijini ambapo mwanawe angetangamana na watoto wengine baada ya maji kuzidi unga kwenye ploti walimokuwa wakiishi. Tuliungana sote ambapo tulikuwa tukishauriana.”

Huku akiwa amepania kuwa ni sharti mwanawe azungumze sawa na watoto wengine, James alijitosa kwenye utafiti na kujaribu karibu kila mchanganyiko wa sawa na mbinu alizoshauriwa bila kujali gharama yake.

“Nilisaka kwenye Google jinsi ya kurekebisha hali ya kuchelewa kuzungumza ambapo niligundua mbinu kwa jina Kanuni ya Nemechek. Inahusu kununua baadhi ya viungo kama vile mafuta safi ya mzeituni, mafuta ya samaki na vinginevyo. Tiba hii ilipendekezwa na daktari raia wa Amerika na alikuwa anauza bidhaa kwenye mtandao wa Amazon.”

“Niliagizia na kulipa zisafirishwe hadi Kenya. Ulikuwa mchakato ghali lakini nilikuwa tayari kutumia hela zangu zote wakati huo.”

Hata baada ya kujitolea hivyo, mwanawe alikataa kunywa mchanganyiko huo wa dawa kwa sababu “ilichukiza mno.”

Baada ya kutaabika akitafuta suluhu, mmoja wa wafanyakazi wenzake alimshauri ampeleke mwanawe kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya kitaaluma katika KNH au Gertrude.

Alifuata ushauri huo ambapo mtoto wake alifanyiwa vipimo na mtaalam wa mazungumzo katika Hospitali ya Gertrude na kupatikana na tawahudi inayotokana na mitandao (virtual autism).

Kwa mujibu wa tabibu huyo, mwanawe haukuwa na tawahudi bali alikuwa ameathiriwa na tawahudi kimtandao kutokana na kutumia muda mwingi akitazama runinga alipokuwa mchanga.

“Alitushauri kupunguza muda anaotumiwa kutazama runinga, tarakilishi, simu au vifaa vinginenvyo vya kielektroniki na tumpeleke kijijini ambapo angecheza na watoto wa rika lake. Hatua hiyo ilizaa matunda na waliporejea mjini, mke wangu akaanza kuhudhuria vipindi maalum vya tiba ya mawasiliano pamoja naye, kusoma alfabeti, rangi, majina ya wanyama, samani na kadhalika. Matokeo yalikuwa ya kufariji mno.”

Shule vilevile ilichangia nafasi muhimu na punde si punde, siku waliyokuwa wakisubiri kwa hamu na ghamu iliwadia! Mtoto wao alianza kuzungumza na kutangamana na wenzake.

Japo mwanzoni matamshi yake yalikuwa na kigugumizi na hayakueleweka, yalisikika kama wimbo mtamu na kuvutia furaha riboribo kwa familia yake.

“Alianza kuzungumza kwa sentensi kamili baada ya kujiunga na PP1 alipohitimu umri wa miaka minne. Kuna siku angerejea nyumbani na kutusimulia jinsi mwalimu wake alivyowaeleza walale au waimbe wimbo waliofunzwa shuleni.”

“Kisha alianza kuwa na tabia ya kuongoza sala kabla ya chakula. Mwanzoni haungeweza kuelewa chochote ila “Kwa jina la baba, na la mwana na la Roho Mtakatifu’ kwa sababu ilikuwa shule ya Kikatoliki.”

“Tulikuwa tunafunga macho yetu tu kwa utiifu na kumpa nafasi ya kusema mambo yake kisha tunajiunga naye kufanya ishara ya msalaba mwishoni,” anasimulia tabasamu likichanua usoni mwake.

Ingawa mtoto huyo huzungumza kwa kigugumizi mara kwa mara ambapo huhitaji mtu kuwa na subira kuelewa anachosema, hali kwamba anaweza kujieleza na hata kusimulia hadithi, inawajaza wazazi wake na bashasha isiyo kifani.

“Ujuzi wake wa kutangamana kijamii umeimarika zaidi kushinda hapo mbeleni alipokuwa mpweke. Hali hii imebadilika tangu alipoanza kwenda shuleni. Ana marafiki watatu: Kamau, Mburu na Maxwell anaosimulia kuwahusu kila arejeapo nyumbani. Ana adui vilevile, mvulana kwa jina Njoroge, anayemtaja kama mvulana mbaya sana. Sina hakika ni kipi Njoroge alimfanyia.”

“Anawajua pia jamaa wake wote wa familia ya karibu na baadhi ya jamaa wa mbali.”

James anawakilisha idadi inayozidi kupanda ya wazazi wanaohangaika kulea watoto wanaochelewa kuzungumza na kukomaa kijamii.

Kutokana na aliyopitia binafsi, hachelei kuwapa motisha wazazi wengine wanaopambana na changamoto kama hizo ushauri wake mkuu ukiwa “kufungua moyo na kuwa na nia thabiti.”

“Usikubali kuteseka pekee yako. Usiogope hukumu au unyanyapaa. Fungua moyo. Huenda kuna wazazi wengine wanaopitia masaibu sawa na unayopitia. Ukizungumza, watu watatoa suluhu unazoweza kujaribu.”

“Jambo la pili, usilaze damu tu ukisubiri mtoto wako azungumze. Kuwa na nia thabiti kuhusu maendeleo yao ya kuwasiliana, wasomee vitabu, jiandikishe kuhudhuria vipindi vya matibabu ya mawasiliano na pia uwapeleke katika shule au vituo ambapo wanaweza kutangamana na watoto wengine.”

Akiwa amepatiwa mshawasha na mwanawe, James alianzisha tovuti, Themonterabbi.com anayotumia kusimulia safari ya familia hiyo tangu mwanzo hadi mtoto wao alipopata nafuu ikiwemo vidokezo kuhusu jinsi ya kukabiliana na hali ya watoto kuchelewa kuzungumza.

Katika kizazi hiki cha maendeleo kiteknolojia, ni muhali kujitenga kutokana na vifaa vya kielektroniki.

Iwe ni bembea za kuwafanya watoto walale, kutuliza vilio visivyo na kikomo au tu kuwashughulisha watoto wachanga na vibonzo na nyimbo za chekechea huku wazazi wakifurahia angalau dakika chache za kujiliwaza, malezi kidijitali yamegeuka kipenzi cha wengi.

Wanasayansi, hata hivyo, wanaonya kuwa huenda unaathiri uwezo wa mtoto wako kuzungumza na kukua kwa kumruhusu muda mwingi usiodhibitiwa kutazama au kucheza na vifaa vya kielektroniki akiwa angali mchanga.

Kuwaruhusu watoto wachanga katika miezi yao ya mwanzoni kutazama runinga, vipakatalishi, simu, michezo ya video na vinginevyo huenda kukawasababisha kuchelewa kuzungumza na kukomaa, kwa mujibu wa watafiti katika Chuo Kikuu cha Tohoku, Japan.

Ripoti hii imejiri huku mataifa yakijitahidi kujikwamua kutokana na athari za Covid-19 zilizolemaza shughuli kote duniani ikiwemo marufuku za usafiri na shule kufungwa.

Matokeo yake yalikuwa idadi kubwa ya watoto waliolazimika kutumia mudas wao mwingi ndani ya makazi yao ama wakitazama au kucheza na vifaa vya kielektroniki.

Wataalam hao walichunguza vitoto vichanga 7,000 kwa miaka minne kati ya 2013-2017 waliogawanywa kwa idadi sawa ya wavulana na wasichana.

Walitathmini miondoko yao ya mwili, mguu, mkono pamoja na mawasiliano mathalan uwezo wa kuelewa, kutamka na kigugumizi.

Isitoshe, wataalam walichunguza ujuzi maalum wa miondoko ya mwili kama vile kusogesha kidole na mkono, kucheza na vifaa vya watoto, kujifuna na kusuhisha matatizo.

Uwezo wa watoto kutangamana kijamii na kibinafsi hususan kucheza na watoto wengine, vifaa vya kuchezea, kucheza kivyao, vilevile ulichunguzwa.

Kupitia dodoso, wazazi walitakiwa kueleza kiasi cha muda wanaoruhusu watoto wao wachanga kucheza na kutazama vifaa vya kielektroniki.

Matokeo yaliashiria matatizo ya kutangamana kijamii na kibinafsi ikiwemo changamoto za miondoko maalum kwa watoto wachanga wanaotumia muda mwingi kwenye vifaa vya kielektroniki wanapohitimu umri wa miaka miwili.

Walipofikisha miaka minne, dalili hizo za kuchelewa kuzungumza na kukomaa zilififia zilionekana kufifia.

Hata hivyo, ujuzi wa kuzungumza ulionekana kuimarika pakubwa vifaa vya kielektroniki vilipotumiwa kwa kusudi la kuwaelimisha watoto.

Wataalam wanashauri wazazi kuchagua vipindi vya hali ya juu vyenye matini ya elimu kabla ya kutambulisha mitandao ya kijamii kwa watoto wao wenye umri kati ya miezi 18-24.

“Katika kizazi cha leo cha dijitali na vifaa vya kielektroniki, ni muhali kudhibiti muda unaotumiwa kutazama vifaa vya kielektroniki. Kutumia vipengee vya kielimu kupitia utambulishaji na kupunguza baadhi ya vifaa vya kielektroniki vinavyohusishwa na kuchelewesha ukomavu huenda kukawa na manufaa,” anaeleza mtaalam kwa jina Dkt Taku Obara.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Bei ya mafuta yapaa juu zaidi

Ruto haonekani kukoma kuvizia wabunge wa upinzani

T L