• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
Wanamazingira waingiwa na wasiwasi mikoko ikifa Kitangani

Wanamazingira waingiwa na wasiwasi mikoko ikifa Kitangani

NA KALUME KAZUNGU

WATUNZAJI na wanaharakati wa kuhifadhi mazingira katika Kaunti ya Lamu wanazidi kukuna vichwa kufuatia kufeli mara kadhaa kwa juhudi zao za kupanda, kukuza na kurejesha mikoko kwenye eneo la Kitangani ambalo msitu wake uliharibiwa zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Eneo hilo la Kitangani tangu jadi lilikuwa likitambulika kuwa miongoni mwa maeneo ya Lamu ambayo yana ukwasi tele wa msitu wa mikoko.

Aidha hali ilianza kwenda segemnege mnamo 2011 wakati mchanga uliochimbwa chini ya bahari kwenye kivuko cha Mokowe kuelekea kisiwani Lamu ulipotupwa eneo hilo la Kitangani.

Shughuli iliyotekelezwa ya kuchimba mvunguni mwa Bahari kwenye kivuko cha Mokowe kuelekea kisiwani Lamu ni hatua iliyonuiwa kuongeza kina cha maji baharini ili kuwezesha vyombo vya usafiri wa majini, ikiwemo boti, mashua na meli kupita bila wasiwasi wa kugonga miamba na kusababisha ajali na maafa baharini.

Ni kutokana na kugeuzwa kwa Kitangani kuwa jaa la kutupa mchanga na changarawe za baharini ambapo hali hiyo ilibadilisha kabisa hadhi ya eneo hilo kwani maelfu ya mikoko iliishia kuangamia, hivyo kuiacha sehemu kubwa kuwa jangwa.

Kwa karibu miaka 12 sasa, juhudi zimekuwa zikiendelezwa na serikali na mashirika mbalimbali ya mazingira katika kurudisha hali shwari na ya asili ya Kitangani bila mafanikio.

Kulingana na Afisa wa Shirika la Kuhifadhi Mazingira la Wetlands International, Kaunti ya Lamu, Shawlet Cherono, kizungumkuti kinachozingira eneo la Kitangani ni kwamba kila mara miche ya mikoko inapopandwa eneo hilo haijafaulu kumea au kukua hadi kufikia ukubwani.

Afisa wa Shirika la Kuhifdhi Mazingira la Wetlands International, Kaunti ya Lamu, Bi Shawlet Cherono akizungumzia juhudi zilizopigwa katika kujaribu kurejesha mikoko iliyoharibiwa eneo la Kitangani, Kaunti ya Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Hali hiyo ni kizingiti kikuu katika kuziba kijangwa cha Kitangani na kubadili sehemu hiyo kuwa  msitu kama ilivyotambulika zamani.

Bi Cherono anasema kufuatia hali hiyo, mashirika ya mazingira, likiwemo Wetland International hivi karibuni yamekaribisha watafiti tofautitofauti, hasa wale wa kuchunguza uchachu wa mchanga (pH) na mengineyo katika kupeleleza hali ya mchanga wa Kitangani na kubaini ni nini hasa kinachostahili kufanywa kufaulisha juhudi za upanzi na ukuzaji wa miti sehemu hiyo.

Afisa huyo alisema miongoni mwa yaliyojitokeza na kusababisha miche kutomea ni jinsi ambavyo vyanzo vya maji yanayoelekezwa Kitangani wakati bahari ikifura au mvua kunyesha vilikuwa vimezibwa na mchanga uliokusanywa pale wakati wa uchimbaji wa kibvuko hicho cha Mokowe kuelekea Lamu mwaka 2011.

Bi Cherono alieleza kwamba ni kutokana na kuziba kwa vyanzo hivyo vya maji, ambapo kila mara maji yalipofika Kitangani hayakuwa yakitoka kwa urahisi.

“Hiyo ilizua tatizo, ambapo oksijeni inayotumika katika kukuza mimea ilitatizwa kusambaa. Hali hiyo ilipelekea eneo hili kukosa uwezo wa miche kukua. Twashukuru kwamba baada ya utafiti kufanywa, tayari tumeondoa mchanga unaotatiza maji kuingia na kutoka eneo hili. Hata harufu mbaya iliyokuwepo kwa sasa imeanza kupungua na tuko na imani kwamba mwishowe juhudi zetu za kupanda mikoko na kurejesha msitu wa Kitangani zitafaulu,” akasema Bi Cherono.

Afisa huyo hata hivyo aliitaka jamii kuwa mstari wa mbele katika kusaidia juhudi za kupanda na kupanua msitu wa mikoko si Kitangani pekee bali pia maeneo mengine mengi ya Lamu ambapo mikoko imevunwa.

Ikumbukwe kuwa mikoko ni kitega uchumi kwa familia zaidi ya 30,000 za Lamu ambazo tangu jadi hutegemea pakubwa uvunaji na uuzaji wa miti hiyo.

Katika miaka ya 1980s, Lamu ilivuma sana kwa kuendeleza biashara ya uuzaji wa mikoko mataifa ya Warabuni kabla ya biashara hiyo kusitishwa kwa hofu kwamba huenda ingemaliza misitu hiyo na kusababisha athari za mazingira.

“Ningeiomba sana jamii, serikali na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali kushirikiana nasi katika kurudisha hadhi ya Kitangani na maeneo mengine ya Lamu ambayo mikoko yake imeharibiwa. Tukishirikiana tutashinda,” akasema Bi Cherono.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Huduma za Misitu nchini (KFS), kaunti ya Lamu ni eneo lenye asilimia kubwa zaidi ya msitu wa mikoko kote nchini.

Maafisa wa Sirika la Huduma za Misitu nchini (KFS) wakipanda mikoko katika sehemu mojawapo ya Kitangani, Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Karibu asilimia 65 ya msitu wa mikoko nchini hupatikana Lamu.

Kwa upande wake aidha, Mwenyekiti wa Miungano ya Kijamii ya Kutunza Mikoko, Kaunti ya Lamu, Abdulrahman Aboud alitaja mikoko kuwa mimea muhimu eneo hilo.

Bw Aboud alitaja mikoko kuwa fahari ya Lamu kutokana na kwamba nyumba nyingi za eneo hilo zimejengwa kupitia mti wa mkoko.

Aliahidi kuendeleza kampeni kabambe miongoni mwa wanajamii katika kupiga jeki juhudi zinazofanywa kupanua msitu wa mikoko kote Lamu.

Alishikilia kuwa watu wa Lamu ni wangwana ajabu kwani tayari wamekuzwa na kuelimishwa kuhusu jinsi ilivyo muhimu kwao kuhifadhi mikoko.

“Utapata kwamba wakazi wa Lamu endapo watakata mkoko mmoja, wao huishia kupanda karibu kumi. Hilo limesaidia sana kuiweka Lamu katika hadhi ya juu linapojiri suala la kuhifadhi mikoko. Karibu familia 30,000 eneo hili zinategemea kukata mikoko, kuuza na kujipatia riziki, kusomesha watoto, kugharimikia matibabu ya hospitali nakadhalika. Hivyo kila mja hapa ana wajibu binafsi wa kuhifadhi miti hiyo ili tuendelee kufaidi milele,” akasema Bw Aboud.

Mbali na kujengea nyumba, mikoko pia imesifiwa mno kwa utengenezaji wa fenicha, boti, mashua, jahazi na matumizi mengine.

Bi Hafswa Saidi Tola aliishukuru serikali kupitia KFS na mashirika yasiyo ya kiserikali, ikiwemo Wetlands International, W.W.F Kenya na makundi ya kijamii ambayo yametoa mchango mkubwa katika kurekebisha misitu ya mikoko iliyoharibiwa na kuendeleza utajiri mwingi wa msitu huo Lamu.

Alieleza kufurahishwa kwake na juhudi za kila mara zinazoendelezwa Kitangani kuona kwamba fahari ya zamani ya eneo hilo ya kuwa na msitu wa mkoko inarejeshwa.

“Nina imani kwamba ipo siku Kitangani itabadilishwa kutoka hali ya sasa ya ujangwa na kuwa msitu mkubwa. Isitoshe, kuna maeneo mengine kama vile Njia ya Ndovu huko Kililana, Manda Titan a Kipungani ambayo yako katika hali mbaya kwa kukosa mikoko baada ya kuvunwa na kuendeleza biashara ya mikoko. Natumai juhudi zinazoendelezwa Kitangani pia zitaelekezwa kwenye sehemu hizo nyingine,” akasema Bi Tola.

  • Tags

You can share this post!

Karen Nyamu: Ninaomba Mungu abadili ajenda ‘mume wangu’...

Kisanga polo akilaumu kahaba kwa kumzima nguvu za kiume...

T L