• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
Wito kwa walioambukizwa HIV wajitokeze waziwazi kuepusha maambukizi ya mama hadi kwa mtoto

Wito kwa walioambukizwa HIV wajitokeze waziwazi kuepusha maambukizi ya mama hadi kwa mtoto

NA ALEX KALAMA

WADAU wa afya katika Kaunti ya Kilifi wameelezea hofu yao, baada ya maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama hadi kwa mtoto kupanda mwaka huu wa 2023.

Akizungumza na wanahabari mjini Kilifi, mratibu wa afya ya uzazi Bw Kenneth Miriti alieleza kuwa maambukizi hayo yanapanda kutokana na kuongezeka kwa akina mama wenye umri mdogo ambao wanajifungua wakiwa wangali shuleni na huogopa kujitokeza waziwazi wanapogundulika kuugua Ukimwi.

“Watu ambao wameathirika sana ni wale matineja na akina mama ambao hawajapitisha umri wa miaka 24 lakini wanaugua Ukimwi. Huwa wanaogopa kujitokeza waziwazi kwa sababu ya unyanyapaa katika huo umri,” akasema Bw Miriti.

Alieleza kuwa ni kawaida siku hizi kumuona msichana ambaye amepatikana na virusi lakini hataki kuelezea ama hataki kujulikana katika jamii kwamba ana HIV, hivyo basi hawezi akampatia mtoto wake dawa vizuri na hawezi akafuatilizia kliniki.

Kulingana na idara ya afya ya uzazi Kaunti ya Kilifi, visa 30 vimeshuhudiwa kufikia Juni 2023, kipindi cha miezi minane pekee ikisajili watoto watano ambao wamepata maambukizi kutoka kwa wazazi wao.

“Katika ngazi ya kitaifa, takwimu zinaonyesha kwamba tuko na asilimia 11.2 kama nchi ya Kenya, lakini Kaunti ya Kilifi tuko chini kidogo tukiwa na asilimia 8.3 na hilo ni jambo zuri la kuonyesha kwamba maambukizi si mengi sana hapa ikilenganishwa na maeneo mengine ya nchi,” akasema.

Alisema kwamba cha kusikitisha ni kuwa mnamo Septemba 2023 walipata visa vitano vya maambukizi kwa mwezi huo mmoja.

“Tusipoweka mikakati, tunaweza kuwa na maambukizi zaidi kwa sababu hilo ni kuonyesha kwamba maambukizi yanaenda juu,” alisema Bw Miriti.

Hata hivyo, idara hiyo imedokeza kuwa tayari serikali imeanza kupambana na hali hiyo kwa kuwatumia akina mama washauri waliopitia hali sawa na hiyo ili kuhakikisha akina mama wanaoishi na HIV wanamlinda mtoto kutokea akiwa mimba na hata anapojifungua.

  • Tags

You can share this post!

Mlalamishi aokolewa kukwepa genge linalohusishwa na...

Kuria sasa atania kaunti za Mlima Kenya akizitaka zipunguze...

T L