• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 12:43 PM
Aibu taulo za hedhi zilizotumika zikitapakaa mitaani Nairobi

Aibu taulo za hedhi zilizotumika zikitapakaa mitaani Nairobi

NA SAMMY WAWERU

MAJAA ya taka mitaa mbalimbali Kaunti ya Nairobi yamegeuzwa kuwa tupio la sodo zilizotumika, hali inayoibua wasiwasi kuhusu usalama wa mazingira kiafya.

Hali hiyo pia inashuhudiwa kandokando mwa barabara, hasa maeneo yasiyo na miundomsingi ya utupaji taka.

Kufuatia uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali katika mtaa wa Roysambu, Zimmerman, Githurai, Mwiki, Mathare, Kahawa West na mitaa mingineyo Thika Road hali imekuwa mbaya zaidi kiasi cha sodo zilizotumika kutapakaa.

Evanson Chege, mkazi Githurai 44 anasema siku za hivi karibuni bidhaa hizo za hedhi zimeonekana kuongezeka.

“Zinahatarisha usalama kiafya wa mazingira,” anasema.

Cha kushangaza zaidi, baadhi zinatupwa zikiwa wazi hata bila ya kufungwa.

Ni jambo ambalo kulingana na wenyeji wa mitaa iliyoathirika, inatishia kusababisha mlipuko wa maradhi.

Baadhi ya maeneo hayo yamekuwa yakiandikisha visa vya Homa ya Matumbo na Kipindupindu.

“Si ajabu kuona taulo za hedhi zimetupwa kwenye mitaro ya majitaka, ambayo pia mifereji ya maji imepitia,” akasema Daisy Kanyua, mkazi Zimmerman.

Nepi ya mtoto iliyotupwa njiani mtaani Zimmerman, Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

“Mtaa wa Mwiki, kando na miundomsingi mbovu na duni ya majitaka, kero ya sodo kutupwa kiholela inatuhangaisha,” akateta Martin Omondi.

Mbali na taulo za hedhi, nepi za watoto zilizotumika pia zinatupwa kiholela.

Baadhi ya makazi, watu wamegeuza nyuma ya ploti kuwa ‘majaa’.

Serikali ya Kaunti ya Nairobi, kupitia mashirika ya kibinafsi imeweka mikakati ya ukusanyaji taka ambazo hupelekwa katika majaa yaliyotengewa shughuli hiyo.

Henry Wanjiku, ni mmoja wa wahudumu wa ukusanyaji taka Nairobi na anasema shughuli hiyo hufanyika kila wiki.

Ni jukumu la kila mmiliki wa nyumba au landilodi kuhakikisha wapangaji wake taka zinakusanywa, Henry anaambia Taifa Leo Dijitali.

“Mfano, sisi hutoza Sh200 kila nyumba na taka zinakusanywa kila wiki,” akasema.

Aidha, kuna wafanyakazi wanaotawanya taka kuhakikisha kila kilichotupwa kinaenda kinapofaa.

Halmashauri ya Kitaifa Kuhusu Mazingira (Nema), ndiyo imetwikwa jukumu kuhakikisha mazingira ni salama.

Hali ya taulo za hedhi na nepi za Watoto zilizotumika kutapaa mitaani Nairobi, inaibua maswali kuhusu utendakazi wa Nema.

  • Tags

You can share this post!

Mapenzi ya mzazi: Baba akubali kupoteza maisha mwanawe...

Good Hope moto kwa Mvita ligini

T L