• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 4:55 PM
Hajuti kamwe kuuza makabeji sokoni Kongowea

Hajuti kamwe kuuza makabeji sokoni Kongowea

NA CHARLES ONGADI

MTAFUTAJI hachoki na akichoka keshapata, ndivyo ilivyo kwa Elijah Kailikia Kithela,34, mfanyabiashara wa mboga aina ya kabeji katika soko maarufu la Kongowea, Mombasa.

Ijapo si mkulima, Kithela maarufu kama ‘Mwananchi’ ameondokea kuwa maarufu kwa uuzaji wa makabeji, biashara ambayo imebadilisha maisha yake maradufu.

“Nilitoka katika familia ya walalahoi nikija Mombasa kusaka maisha ila kutokana na bidii na kujituma,nimeweza kubadilisha maisha yangu na familia,” asema mwanafunzi huyu wa zamani wa Chuo cha Kiufundi cha Mombasa.

Kwa sasa Kithela ni kati ya wafanyibiashara katika soko kuu la Kongowea ambao wameshikilia biashara ya kuuza makabeji na soko zingine katika kaunti jirani za Kilifi na Kwale.

Kithela, mzaliwa wa Igembe Kaskazini, kijijini Nkandone, alisomea Shule ya msingi ya Naathu kisha Shule ya Upili ya Muthuati na kumaliza mwaka wa 2012.

Kulingana na mfanyibishara huyu, juhudi zake za kuendeleza masomo yake katika Chuo cha Kiufundi cha Mombasa (TUM), ziligonga mwamba, baada ya wazazi wake kushindwa kumlipia karo kutokana na maisha ya uchochole iliyowazonga kipindi hicho.

“Niliamua kusaka maisha Mombasa baada ya kuwacha masomo yangu na kujitosa katika biashara ndogo ndogo kujikimu kimaisha na pia kuwasaidia wazazi wangu,” aeleza.

Kithela anaiambia AkiliMali kwamba aliamua kujitosa katika kazi ya kuwauzia wafanyibiashara miraa na wakati huo huo kuwabebea mizigo yao punde ilipowasili sokoni.

Katika juhudi hizo, anasema alifaulu kujiwekea akiba ya Sh161,000.

Hapo, aliamua kutumia hela hizo kama mtaji wa kuanzishia biashara ya duka eneo la Bamburi, Kisauni Mombasa.

Hata hivyo, Kithela anasema mwaka wa 2013 aliamua kuuza duka lake baada ya biashara yake kuanza kuyumbayumba na kuelekea Eldoret kujaribu bahati yake katika biashara tofauti ya kuuza miraa na aina tofauti ya vinywaji.

Lakini mambo yakamwendea segemnege na kuamua kurudi Mombasa kujaribu tena bahati yake sokoni Kongowea.

Wavyele wanasema kuvunjika kwa mwiko siyo mwisho wa kusonga ugali, licha ya pandashuka zilizomkabili Kithela, aliamua kuajiriwa kama muuzaji kabeji na Steven Nderu aliyekuwa maarufu katika biashara ya kuuza mboga hizo sokoni Kongowea.

Kwa mujibu wa Kithela, hapo ndipo ilikuwa mwanzo mpya ya maisha yake ya mafanikio katika biashara kwani alisoma mbinu kibao ya kufaulu katika biashara ya makabeji kutoka kwa mwajiri wake.

“Hapa nilitangamana na wafanyibiashara watajika wa mboga na matunda kutoka bara na nikaamua kuwachana na kazi ya kuajiriwa ili kujaribu bahati yangu katika biashara ya makabeji,” asimulia Kithela.

Alijipiga moyo konde na kutumia akiba aliyokuwa nayo ya Sh100,000 kununulia mboga kutoka kwa wakulima shambani na kuwauzia wafanyibiashara katika soko la Kongowea.

Anakiri kwamba katika jaribio lake la kwanza alipata hasara ya Sh30,000 lakini akajikokota na kuendeleza juhudi zake pasina kuchoka.

Kithela anafichua kwamba ilipofika mwaka wa 2018, biashara yake ilianza kunoga akinunua makabeji kwa wingi kutoka wakulima wa maeneo ya Naivasha, Nyandarua, Subukia na maeneo mengine.

“Nilipata wateja kutoka maeneo mengine katika Kaunti za Kilifi na Kwale waliofika sokoni Kongowea kila asubuhi kuchukua mali yao. Kutokana na uaminifu na uadilifu nikaangukia oda ya kuuza mboga katika kambi ya Jeshi ya Wanamaji iliyoko Mtongwe, Mombasa,” afichua mfanyibiashara huyu mkakamavu.

Kutokana na faida aliyojirundika, Kithela asema aliweza kupanua zaidi juhudi zake kwa kuanzisha biashara ya hoteli na duka katika maeneo tofauti Mombasa mbali na kuwajengea wazazi wake nyumba kwao Meru.

Aidha, anafichua kwamba kati ya changamoto anazokabiliana nazo katika biashara yake ni baadhi ya wateja wake ambao pia ni wafanyibiashara kutoroka bila kulipa deni.

“Kuna baadhi ya wateja wangu ambao pia ni wafanyibiashara katika soko mbali mbali hapa Pwani ambao ninawapatia mboga kwa ahadi ya kulipa baada ya kuuza ila wanaamua kutotimiza ahadi ya kulipa hivyo kuyumbisha biashara yangu,” asema.

Tatizo lingine ni kipindi cha mvua ambapo mara nyingi mboga zinaponyeshewa huharibika na kuweka hasara kwa mfanyibiashara.

Hata hivyo, Kithela anasema siri kuu katika biashara ni kujituma na kutokata tamaa huku akiwashauri vijana kutosubiri kuajiriwa bali kuwa wabunifu katika kila wanaloamua kufanya kwa mafanikio yao ya baadaye.

  • Tags

You can share this post!

Waraibu wa biashara ya mapenzi walalamikia mipira inayotoka...

Madai watu walilipwa kuhudhuria maadhimisho ya Jamhuri Dei...

T L