• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 5:55 PM
Kijana aliyeunga listi ya ‘40 under 40’ ashirikiana na chuo kikuu kuanzisha kiwanda cha biskuti za samaki

Kijana aliyeunga listi ya ‘40 under 40’ ashirikiana na chuo kikuu kuanzisha kiwanda cha biskuti za samaki

NA MAUREEN ONGALA

CHUO Kikuu cha Pwani katika Kaunti ya Kilifi kimesifu aliyekuwa mwanafunzi wa chuo hicho kwa kuunga listi ya ’40 Under 40′ katika maswala ya Uchumi wa Baharini jijini Nairobi.

Maafisa wakuu katika chuo hicho cha Pwani walimlaki Bw Frank Thoya katika sherehe ya kukata keki iliyofanyika katika chuo hicho.

Bw Thoya kutoka kijiji cha Tezo katika eneobunge la Kilifi Kaskazini alikuwa mshindi miongoni mwa maelfu wa vijana baada ya kuwasilisha na kuupa umaarufu mradi wake wa biskuti za samaki. Alisema ni njia moja ya kutatua changamoto ya utapiamlo miongoni mwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano katika Kaunti ya Kilifi.

Bw  Thoya alifuzu na kutunukwa cheti cha shahada ya Sosholojia mnamo Novemba 23, 2023.

Kulingana na  Profesa wa Sayansi za Jamii na Maendeleo katika Chuo Kikuu cha Pwani Halimu Shauri, alisema kuwa tuzo hiyo imeweka chuo cha Pwani katika ramani ya nchi na dunia nzima.

Akizungumza na Taifa Jumapili baada ya kumpkoea Bw Thoya katika chuo hicho na kusherekea ushindi wake Prof Shauri alisema kuwa ushindi huo ni dhihirisho kuwa vijana katika maeneo ya changamoto humu nchini wana uwezo wa kuwa bora licha ya changamoto wanazokumbana nazo.

“Jamii ya  Chuo Kikuu cha Pwani tuna furaha kubwa kwa sababu mwanafunzi wetu aliwakilisha mradi bora zaidi na ametuweka katika ramani na kuonyesha kuwa pia Kilifi inaweza kutoa kitu ambacho kinaweza kikachangia suluhu ya matatizo ya dunia,” akasema.

Profesa Shauri alieleza kuwa safari ya Bw Thoya kutafuta kuongeza elimu katika chuo hicho ilikuwa yenye changamoto lakini yenye ubunifu.

“Amekuwa na changamoto katika kuendeleza na kufikisha hatima masomo yake ikiwemo ukosefu wa karo, mahitaji ya kimsingi lakini hakuvunjika moyo na aliweza kuendeleza fikira na mawazo yake na kuendeleza kipaji chake. Ubunifu wake unaweza kuwa mdogo lakini ukiangalia kwa undani utapata kuwa katika mradi wake ameweza kuhusisha taaluma tofauti tofauti,” akasema.

Profesa huyo alisema kuwa ubunifu huo ni kielelezo mwafaka kwa vijana wote kuwa watafanikiwa katika kila jambo licha ya safari yenye changamoto nyingi.

“Bw Thoya amehusisha taaluma ya kilimo ambapo anatumia muhogo ambao ni kiungu chake muhimu katika biskuti hiyo na pia maswala ya baharini kwa kutumia samaki. Biskuti hii inachangia katika kutimiza malengo ya ruwaza ya 2030 ya kupigana na njaa na kuhakikisha lishe bora,” akasema.

Prof Shauri anatoa wito wa serikali ya kitaifa na zile za kaunti kuangazia na kuwainua kiuchumi na pia kiteknolojia vijana wote walioshiriki katika mashindano hayo hususan vijana 40.

Alieleza masikitiko yake kuwa licha ya kuwa na ubunifu huo, serikali haikujitokeza kumshika mkono mwanafunzi huyo.

“Serikali ina wajibu kwa sababu haya mafanikio yote nikimjua Frank wakati ana changamoto anakuja tunaongea na kujadiliana  vipi atatoka na kupitia wapi. Serikali haikuweza kujitokeza kwa nguvu kuonyesha ya kwamba inaweza msaidiua kijana ambaye ana ubunifu mkubwa,” akasema.

Prof Shauri alisema kuwa ubunifu huo utatoa ajira kwa vijana wengine.

“Mbali na kutoa ajira na kutoa chakula kwa jamii, serikali haijamwezesha kwa sababu wazo hili la ubunifu ni kubwa na linaweza likaleta mabadiliko miongoni mwa vijana na kutoa natija kwa serikali kupitia mapato ya kodi ,” akasema.

Kwa upande wake Bw Thoya, alielezea furaha yake na kusema kuwa ilikuwa safari ndefu ikizingatiwa kuwa alikuwa anashindana na takriban watu 6,777  na kati ya hao, ni vijana 40 peke yao ambao walihitajika.

Bw Frank Thoya akiwa na uteo wa papa ili kuwauzia wateja. PICHA | MAUREEN ONGALA

Alishukuru kampuni ya Nation Media Group (NMG) kupitia shirika la John Walker kwa kufadhili mashindano hayo na kusema tuzo hiyo ni ya Chuo Kikuu cha Pwani na jamii pana ya Kaunti ya Kilifi.

“Majaji walichagua wakapata vijana 500 bora na wakaendelea kuchuja na kuwapata 40. NaMshukuru Mungu kwa sababu amewezesha mashindano hayo kufanyika na nikaonyesha ubunifu wangu kwa taifa na ulimwengu,” akasema Bw Thoya.

Kijana huyo alidokeza kuwa anaendeleza mazungumzo na Chuo Kikuu cha Pwani ili kujenga kiwanda cha kuoka biskuti hizo katika chuo hicho.

“Kiwanda hiki kitatoa nafasi za ajira kwa jamii ya Kilifi ili wafanyakazi waweze kujimudu maishani,” akasema.

Bw Thoya alikuja na uvumbuzi huo baada ya kufanya utafiti wa changamoto ya utapiamlo katika Kaunti ya Kilifi, hali inayochangiwa pakubwa na kiwango kikubwa cha umaskini miongoni mwa wanajamii.

Utafiti wa  Kenya Demographic and Health Survey 2014 uliorodhesha kaunti ya Kilifi nambari ya tatu ikiwa na asilimia 39.1 katika viwango vya utapiamlo na kudumaa. Kaunti nyingine kwenye orodha hiyo mbaya zilikuwa ni Kitui na Pokot Magharibi miongoni mwa watoto wa umri chini ya miaka mitano.

Idadi ya watoto walioathirika na utapiamlo na kudumaa nchini ilikuwa asilimia 26.

Bw Thoya alijiunga na chuo hicho cha Pwani mwaka wa 2017 .

Hapo mwanzo, Bw Thoya alijihusisha na biashara ya kurembesha mandhari ya kufanyia sherehe mbalimbali ili kujilipia karo.

Biashara hiyo ilikuwa imenoga lakini janga la ugonjwa wa Covid-19 likaiathiri pakubwa baada ya serikali kupiga marufuku sherehe na mikusanyiko ya aina yoyote nchini kuzuia au kupunguza kusambaa kwa ugonjwa huo.

Hapo awali Bw Thoya alikuwa anauza samaki aina ya papa.

Alijiita ‘The papa man’ kwani alikuwa anazungusha bidhaa hiyo katika ofisi kadhaa na maboma ya wakazi vijijini.

Muda ulivyozidi kusonga na biashara kunoga, Bw Thoya aliamua kutafuta njia ya kuongeza thamani kwa biashara yake ya samaki na akaamua kutengeneza biskuti za samaki.

  • Tags

You can share this post!

Polisi anayedaiwa kumvunja mwanakijiji mikono kwa kukataa...

Mpiga picha aliyeponea kifo kwa moto kanisani Kiambaa 2008...

T L