• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 4:34 PM
Namna ya kuandaa nyama ya mutura kulika msimu wa Krismasi

Namna ya kuandaa nyama ya mutura kulika msimu wa Krismasi

NA LABAAN SHABAAN

KATIKA barabara ndogo mkabala na Barabara Kuu ya Thika Superhighway hatua chache tu kutoka eneo la Bypass kuelekea mtaa wa Gatong’ora eneobunge la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, kuna vibanda vingi vya kuuzia mutura lakini kibanda chake Benjamin Mutua huwa na foleni kubwa ya wateja.

Mwandishi huyu alipokutana na Bw Mutua mnamo Jumatano jioni akiuza mutura kwa wapitanjia wa Sunrise Estate, mfanyabiashara huyo alisema siri yake ni kuandaa mutura hadharani watu wasimdhanie vibaya.

Wengi wanaoogopa mlo huo, anasema, wamechukulia kwa uzito habari zilizoenea kuwa huenda mutura hujazwa nyama za paka, mbwa ama punda waliochinjwa.

Mkabala na kibanda chake Bw Mutua, kuna bucha ambayo ni chanzo cha malighafi ya kuandaa mutura.

Bw Mutua anaambia Akilimali kuwa katika kipindi hiki cha shamrashamra za Krismasi na Mwaka Mpya, anaweka zingatio katika kuandaa mutura ambao wateja wake wakila watajisikia wamekula nyama choma.

“Ng’ombe akishachinjwa kwa utaratibu unaokubalika, sisi huchukua utumbo na kusokomeza ndani nyama kutoka kwa sehemu ya paja ambayo huwa tayari imesagwa, kisha kutia viungo kama chumvi, dania na kitunguu kilichokatwakatwa vizuri,” akaeleza Bw Mutua.

Akaongeza: “Tunaandaa mutura hadharani ili wateja waone na kutuamini kuwa sisi ndio mabingwa katika kuchoma mutura tamu.”

Mfanyabiashara wa mutura Benjamin Mutua akiuza mlo huo kwa wateja katika mtaa wa Gatongora ulioko Ruiru katika Kaunti ya Kiambu mnamo Desemba 20, 2023. PICHA | LABAAN SHABAAN

Kwa kawaida bei ya mutura imesalia pale pale, kumaanisha Bw Mutua huuza mutura kwa angalau Sh20 kila kipande anachokata ambacho saizi yake wateja wameshazoea.

“Hii Krisimasi kama huwezi kumudu kununua nyama, basi mutura utakuwa mbadala maridhawa kwa sababu tunakata vipande vya nyama ya mapaja ya mbuzi ama ng’ombe na kutumia kuandaa,” akajanjarusha Bw Mutua.

Baada ya kuandaa mutura kwa kuweka viungo vyote vinavyohitajika kwenye utumbo wa ng’ombe uliosafishwa ukatakata, Bw Mutua hutumbukiza kwenye dumu la supu lililoinjikwa mekoni ili supu hiyo iive.

Mfanyabiashara wa mutura Benjamin Mutua akiuza mlo huo kwa wateja katika mtaa wa Gatongora ulioko Ruiru katika Kaunti ya Kiambu mnamo Desemba 20, 2023. PICHA | LABAAN SHABAAN

Hatua itakayofuata ni kuchoma mutura hadi maji maji yakauke ambapo mlo huu utakuwa tayari kuliwa.

Wateja wake aghalabu huambatanisha mutura kwa supu inayogharimu Sh10 kwa kikombe.

“Nikila mutura bei ya Sh50 kwa supu kikombe kimoja, nitahesabu nimekula chajio na kilichobaki ni kulala na kuamkia siku nyingine,” akasema mteja mmoja akieleza ni njia yake ya kula nyama wakati gharama ya juu ya maisha imekuwa donda sugu siku za hivi karibuni.

  • Tags

You can share this post!

‘Ground’ mbovu waziri Linturi naye akidai...

Kang’ata atia breki utoaji wa Sh4,000 kwa kila mimba...

T L