• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
Uongezaji thamani mazao ya kilimo ndio siri ya kuimarisha sekta ya viwanda

Uongezaji thamani mazao ya kilimo ndio siri ya kuimarisha sekta ya viwanda

Na SAMMY WAWERU

MOJAWAPO ya Ajenda Nne Kuu za Rais Uhuru Kenyatta ni kuimarisha na kuboresha sekta ya viwanda nchini.

Huku akisalia na chini ya miezi minane pekee kustaafu, wadau na washirika katika sekta ya kilimo wanahisi atafanikisha lengo lake kikamilifu endapo atatilia maanani kilimo.

Sekta hii ni pana, na inaanzia shughuli za ukuzaji mazao, soko na usindikaji – yaani kuyaongeza thamani.

Kwa kiwango kikuu, viwanda vinategemea mazao mabichi shambani. Mfano, juisi au sharubati, kinywaji kinachotengenezwa kwa kutumia matunda kama malighafi, sauce au paste ya nyanya na pilipili hoho (zile kali), vileo, kati bidhaa nyinginezo…

Kimsingi, sekta ya viwanda inaambatana ama kuenda sambamba na ile ya kilimo.

Njoki Muriuki ni mwasisi wa Kijo’s Garden, mradi wa kuongeza pilipili hoho thamani.

Huunganisha pilipili kwa kutumia viungo asilia kama ndimu, tangawizi, vitunguu saumu, asali na mafuta ya canola, kupata chilli paste.

Paste anayopata, imegawanywa kwa makundi matatu, ndiyo; tamu japo chachu (sweet chilli), ya kadri na chachu (mild chilli) na chachu zaidi – moto (hot chilli).

Malighafi anayotumia Njoki Muiruki kutengeneza chilli paste. PICHA | SAMMY WAWERU

Akisisitiza kwamba hatumii viungio vyovyote vyenye kemikali, afisa huyu mkuu mtendaji wa Kijo’s Garden anadokeza hutumia Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Nchini (KIRDI), kuendeleza shughuli hiyo.

Mbali na mashine za taasisi hiyo ya serikali, vifaa vingine anavyotumia ni grainda ya jikoni, chombo cha kuchanganya kwa kutumia nguvu za umeme (blender) na kipimajoto.

Ni mradi alioanzisha baada ya Kenya kukumbwa na janga la Covid-19 mwaka uliopita, Machi 2020.

“Nimesomea taaluma ya masuala ya usafiri, ambapo nilikuwa nikitafutia abiria wa ndege vyeti vya kuabiri, ndani na nje ya nchi,” afichua.

Njoki ni raibu wa mapishi, na aligeuza ujuzi wake kuwa biashara kutengeza chilli paste.

Hajutii kamwe, kutokana na hatua alizopiga mbele kimaendeleo chini ya kipindi cha muda wa mwaka mmoja pekee.

Mjasirimali huyu anajivunia kuwa miongoni mwa wafanyabiashara, wakulima na wafugaji walioshiriki maonyesho ya siku mbili ya nyama, Nairobi KICC Meat Expo mwishoni mwa mwaka uliopita, 2021.

Licha ya Kijo’s Garden kumwajiri, anasisitiza kwamba ni mradi unaolenga kupiga jeki wakulima.

Aidha, ana zaidi ya wakulima 800 kutoka eneo la Pwani, Ukambani na Kajiado, wanaomsambazia mazao mabichi ya shambani na viungo anavyotumia.

“Hununua moja kwa moja kutoka kwa wakulima, ili kuwainua. Kimsingi, ni njia mojawapo kuwaondolea changamoto zinazochochewa na kero ya mawakala,” afafanua.

Uongezaji thamani mazao mabichi ya shambani anaoendeleza, una maana kuwa yeye ni kati ya waliojituma kuboresha sekta ya kiwanda.

“Vingi vya vifaa ninavyotumia ni vinavyopatikana jikoni. Majiko yetu ni viwanda tunavyoweza kuvigeuza kuwa chanzo cha mapato,” Njoki asema.

Kulingana na Katibu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki – Kenya, Dkt Kevit Desai, haja ipo maslahi ya wakulima kuangaziwa.

Afisa huyu anakiri sekta ya viwanda inategemea kilimo na ufugaji, kwa kiasi kikubwa.

“Asilimia 50 ya viwanda inategemea sekta ya kilimo, mikakati kabambe inapaswa kuwekwa kuiboresha,” Dkt Desai asema.

Mikakati hiyo inajumuisha kuyafanya mazingira ya kilimo kuwa nafuu, kuanzia bei bora ya pembejeo; mbegu, fatalaiza na dawa dhidi ya wadudu.

Kilele cha mazao ya kilimo ni soko, hivyo basi wakulima hawapaswi kuhangaika kuyauza.

Sekta ya viwanda hasa uongezaji thamani mazao mabichi ya shambani, kama anavyofanya Njoki Muriuki ikipigwa jeki na serikali, hii ina maana kuwa mianya ya soko bora itakuwa imelainishwa.

Itakuwa afueni kwa wakulima, na kuwanasua kutoka kwenye minyororo ya mabroka wanaozidi kuwakandamiza bila huruma.

Mahangaiko ya kukosa soko ndiyo yanachangia mazao ya wakulima kuharibikia na hata kuozea shambani.

Ukizuru mengi ya masoko nchini, kama vile Marikiti, Githurai, Makongeni, Wangige, miongoni mwa mengine vitunguu na nyanya zinazotupwa kwa kukosa wanunuzi ndiyo ratiba ya kila siku.

Kwa Njoki mazao kama hayo ni dhahabu, anayoigeuza kuwa pato. Suala la viungo vya mapishi kutupwa, hukera mjasiriamali huyo na anahisi serikali inapaswa kumakinika na kuweka mikakati kabambe kuhamasisha umuhimu wa kuongeza mazao mabichi thamani.

“Sekta ya viwanda ni mazao tunayotoa shambani. Viwanda na kilimo, ni sekta mbili zinazotegemeana na kuenda sambamba,” asisitiza.

  • Tags

You can share this post!

‘Jungle’ Wainaina aeleza jinsi Njonjo...

Faini ya jogoo 3, mbuzi 2 kwa kula uroda na jirani

T L