• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
UJASIRIAMALI: Wadudu kama nzi hivi, kwake dhahabu

UJASIRIAMALI: Wadudu kama nzi hivi, kwake dhahabu

Na PAULINE ONGAJI

KWA watu wengi, huenda wadudu hawana thamani yoyote, lakini hiyo ni kinyume na mtazamo wa Bw Kristian Larsen, mfugaji wa wadudu ambaye kwa miaka miwili sasa ameendelea kuvuna vinono kutokana na biashara hii.

Bw Larsen hasa anafuga Black Soldier Fly (BSF), aina ya wadudu wa jamii ya nzi na ambaye hupatikana katika maeneo ya joto huku asili yake ikiaminika kuwa Amerika Kusini.

Kwa kawaida yeye huvuna viluwiluwi vya wadudu hawa kabla ya kuvikausha ambapo mwishowe bidhaa inayopatikana inayotumika kama kiungo kikuu cha protini katika uundaji wa chakula cha mifugo.

Anafanya hivi kupitia kampuni yake kwa jina NutriEnto, ambapo amekuwa akiuzia bidhaa hii viwanda vya kuunda chakula cha mifugo.

Anaendeleza ufugaji huu katika shamba lake eneo la Karen, jijini Nairobi. Shaba hilo lina sehemu kadhaa ikiwa ni pamoja na kizimba ambapo wadudu hawa hutaga mayai, na kingine cha kulisha viluwiluwi.

“Tunatumia nyumba ya kioo ya kuhifadhi mimea. Kisha unahitaji vizimba vya uzalishaji na vijisanduku ambapo viluwiluwi vinalishwa na kunenepeshwa,” aeleza Bw Larsen.

Utaratibu wote huu wa kuzalisha kiungo hiki cha protini huanza mdudu wa kike anapotaga mayai.

“Kisha mayai hayo yanakusanywa na kuatamizwa na kuangua. Kisha viumbe wadogo walioanguliwa (neonates) wanakua katika awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu ambapo kila awamu huitwa Instar. Kwa ufupi, viumbe walioanguliwa wanakua na kuwa viluwiluwi ambavyo hunenepeshwa kwa kulishwa kwa mchanganyiko wa taka uitwao substrate,” aongeza.

Kulingana na Bw Larsen, taka hii kwa kawaida huwa mchanganyiko wa uchafu wa parachichi na viazi ambavyo huwa vimechachushwa.

“Mimi hukusanya uchafu huu kutoka sehemu mbali mbali jijini Nairobi, ambapo kwa kawaida mchanganyiko huu huwekwa kwenye vifaa vilivyofungwa na kuchachushwa kwa wiki moja. Kuchachusha husaidia kukabiliana na haruufu mbaya.”

Pindi viluwiluwi vinapofikia awamu ya tano, vinavunwa na kukaushwa. Lakini kabla ya kuanza utaratibu wa kuakausha, viluwiluwi hivyo vinatengwa kulingana na rangi ambapo asilimia 80 ya viluwiluwi (vyeupe) huvunwa tayari kukausha.

Kwa upande mwingine viluwiluwi vyeusi ambavo huwakilisha asilimia 20 hurejeshwa kwenye vizimba na kubadilika na kuwa pupa, kisha kubadilika na kuwa wadudu ambao baadaye wataanzisha mzunguko upya kwa kutaga mayai.

Awamu inayofuatia ni kwa viluwiluwi kuanza kukaushwa na kuwa bidhaa ya mwisho ambayo ni kiungo cha priotini. “Utaratibu huanzia kwa kuweka viluwiluwi vilivyovunwa katika kifaa cha kukausha. Kifaa hiki kina uwezo wa kukausha kufikia kilo 300 za viluwiluwi mara moja. Hapa, viluwiluwi hivi hukaushwa kwa joto la nyusi 65 kwa saa moja,” aeleza.

Kulingana na Bw Larsen, uzalishaji wa bidhaa hii huwa tofauti lakini yaweza fikia kati ya kilo 500 na tani moja unusu kwa mwezi. “Wateja wetu hasa huwa waundaji vyakula vya wanyama. Pia sisi huuza moja kwa moja kwa wafugaji wadogo wa kuku na samaki,” aongeza.

Kulingana na Dkt Chrysantus Tanga, mwanasayansi wa utafiti, mpango wa Insects for Food, Feed and Other uses (INSEFF) katika shirika la International Centre of Insect Physiology and Ecology ICIPE, wadudu hawa wa viwango vya juu vya protini kufikia kati ya asilimia 40 na 60. “Aidha, protini yao ni ya bei nafuu kwa asilimia 26%. Hii ni ikilinganishwa na bei ya samaki wa dagaa (omena) ambao hutumika kwa wingi kama chanzo cha protini katika utengenezaji chakula cha mifugo, ambayo huwa kati ya asilimia 40 na 44,” aongeza.

Dkt Tanga asema kwamba wakati huu ambapo nchi nyingi zinauza maharagwe ya soya (ambayo pia ni chanzo kikuu cha protini ya chakula cha mifugo) kwa bei ya juu, huenda bei ya chakula cha mifugo ikaongezeka, na mwishowe kuathiri bei ya bidhaa za wanyama.

“Huenda wadudu hawa wakawa suluhu kwa tatizo hili. Hii ni kwa sababu mzunguko wao wa uhai ni mfupi sana kufikia kati ya mizunguko 9 na 10 kwa mwaka, ikilinganishwa na mizunguko ya wanyama au mimea. Kumbuka kwamba wadudu hawa huzalisha vyema kufikia kati ya mayai 500-900 kwa mpigo mmoja,” aongeza.

Kwa upande wa usalama, Dkt Tanga asema, wadudu hawa hawana madhara kwa binadamu kwani hawabebi maradhi wala kung’ata kwa sumu.

“Zaidi ya yote utaratibu wa ukaushaji ili kupata bidhaa ya mwisho ni muhimu kwani hapa ndipo maradhi na uchafu mwingine unaondolewa. Lakini pia wadudu hawa wana uwezo wa kuondoa bakteria wenyewe,” asisitiza Dkt Tanga.

Lakini mbali na kuunda bidhaa za protini, Bw Larsen asema kutokana na ufugaji huu, wamekuwa wakiuzia wakulima wengine mayai.

“Kwa wiki moja tunaweza uza kufikia gramu 150 ya mayai. Kwa sasa tuna wateja wa tano kutoka Karatina, Thika, Juja na Kenol.”

Aidha, baada ya kuvuna viluwiluwi, uchafu uliosalia kutokana na chakula chao hutumika kama mbolea. “Baada ya kuutoa, unaachwa nje katika kifaa kikubwa kwa wiki moja, ili vimeng’enyovipate muda wa kufanya kazi. Aidha, kufanya hivyo huizuia isiunguze udongo wa juu,” aeleza Larsen.

Kulingana na Dkt Tanga, mbolea inayotokana na wadudu hawa huimarisha rotubea kwenye udongo. Mbolea hii imefanyiwa majaribio na kuonekana kuimarisha mazao ya mimea kama vile maharagwe na sukuma wiki, ikilinganishwa na ile ya kemikali.

Kwa sasa, Bw Larsen asema kwamba wao huwapa wakulima mbolea hii, ambapo kwa upande mwingine wao huiuza kwa kati ya Sh20 na Sh100 kwa kilo.

Anasema kwamba kinachowaweka upeoni ni kwamba wamepokea mafunzo kutoka kwa ICIPE na Chuo Kikuu cha Wageningen, Uholanzi, na hivyo wanafuata mbinu za kisasa.

Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba hawakumbani na changamoto. Anasema changamoto kuu ni ufadhili hasa ikizingatiwa kwamba hii ni fani mpya. “Aidha kuna suala la kuzalisha bidhaa hii kwa wingi ili kutosheleza mahitaji ya viwanda vya kuunda vyakula vya mifugo, kupata mchanganyiko ufaao wa kulisha wadudu hawa, vile vile kujua uwiano ufaao.”

Lakini anasisiza kwamba japo ufugaji wa wadudu hawa ni jambo mpya, anaendela kutiwa moyo na mahitaji mengi mingoni mwa wateja wao, kumaanisha kwamba kuna fursa ya kukua katika sekta hii.

Baada ya kurejea nchini mwaka wa 2015 kutoka nchini Australia ambapo alikuwa ameendea kusomea kilimo biashara na ufugaji wa samaki na wanyama wengine wa majini, aligundua kwamba asilimia 80 ya bidhaa za protini za kuunda chakula cha wanyama zilikuwa zikiagizwa kutoka nje. “Asilimia iliyosalia ilikuwa kutoka kwa samaki wa dagaa (omena) ambao idadi yao katika Ziwa Victoria imeathirika pakubwa.”

Kwa hivyo alipoanzisha kampuni ya NutriEnto mwaka wa 2019, madhumuni yake yalikuwa kuleta bidhaa mbadala kwa soko, mpango uliofanikishwa na ufadhili wa $1500, aliopokea kutoka kwa Hazina ya Rockefeller Foundation.

“Awali nilijaribu kufuga samaki lakini tena singeweza kabiliana na samaki wa bei rahisi waliokuwa wakiingia nchini. Hili lilikuwa tatizo hasa ikizingatiwa kwamba chakula kilikuwa ghali.”

Kwa sasa, kampuni ya NutriEnto ina wafanyakazi wanne, na Bw Larsen asema wameanzisha mpango wa kusaidia wakulima wanaotaka kuanzisha mashamba yao. “Aidha, sisi husaidia wakulima kukausha viuwiluwi vyao pindi baada ya kuvuna.”

You can share this post!

Waliopokea mafunzo ya ugaidi kupewa ushauri nasaha

LEONARD ONYANGO: Itabidi Mudavadi akubali wadhifa wa...

T L