• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
ZARAA: Nyasi maalum inayopatia wafugaji matumaini tele

ZARAA: Nyasi maalum inayopatia wafugaji matumaini tele

NA LABAAN SHABAAN

JOSEPH Mwangi, Burton Githaiga na John Karia ni wataalamu wa uhandisi, sheria na mazingira mtawalia ambao walikutanisha bongo zao na kuanza kilimo ila mwanzo wao nusura uwakatishe tamaa kwa jinsi walivyoumizwa na madalali.

Kabla ya kukuza malisho ya mifugo kama vile nyasi ya super napier grass, brachiaria na sweet potatoe vines, wataalamu hawa walijihusisha na kilimo cha vitunguu saumu na french beans ila walipata mapato duni wakilaumu kupunjwa na mabroka.

Mwangi, Githaiga na Karia ni wakurugenzi wa Kampuni ya Maximum Milk Production Solution Afrika (MMPS), iliyoasisiwa mwaka wa 2019 na sasa wanasambaza malisho ya mifugo kote nchini kwa juhudi zao wenyewe.

MMPS inajulikana sana miongoni mwa wakulima kwa sababu imevuma na kuvuna wakulima wapya wa nyasi maalum ya Napier.

“Super Napier Grass hunawiri haraka sana na mche mmoja hukupa mashina arubaini huku ekari moja ikisheheni miche 4, 500 wakati wa upanzi,” Mwangi anaeleza.

“Uzuri wa nyasi hii ni kuwa mkulima hupalilia mara mbili tu baada ya kupanda na baada ya mavuno hakuna kupalilia sana kwa kuwa homoni za kuwezesha kukua kwa Super Napier hufanya nyasi hii kutoathiriwa na magugu tena,” anaongeza.

Mwangi anasifia kilimo hiki akisema hupata mavuno kila baada ya siku 30 hadi 60 kutegemea na hali ya hewa.

Shambani humu, Super Napier hukomaa miezi miwili hadi mitatu baada ya kupandwa. “Nyasi hii maarufu Pakchong 1 hustahimili hali tofauti za anga na hakuna sehemu ambapo sijaiuza Kenya.” “Sasa tunauza miche sana ila siku za usoni tunatazamia zaidi kuuza malisho ya mifugo,” asema Mwangi.

Ili kufikia soko na kuvumisha mazao yanayokuzwa Thika, Kaunti ya Kiambu na pia Kigumo, Kaunti ya Muranga katika mashamba ya ekari zaidi ya 60, maafisa wasimamizi wamebuni mikakati kabambe ya usambazaji na makuzi.

Mkurugenzi wa MMPS, John Karia, ashika baadhi ya mashina ya Pakchong 1 yaliyo tayari kuuzwa kama miche. PICHA | LABAAN SHABAAN

Kila mkurugenzi wa kampuni hii ana majukumu yake ili kutekeleza malengo yao. Karia husaidia kutathmini mazingira bora ya kilimo na kusimamia oparesheni naye Githaiga hujihusisha na masuala ya kisheria na mauzo.

“Sisi husambaza bidhaa zetu kwa wateja kote nchini kutumia mashirika ya kusafirisha mizigo,” Githaiga anaambia Akilimali.

“Aghalabu tunatangaza kazi yetu kupitia mitandao ya kijamii hasa Facebook. Kwa siku tumeratibu kutuma zaidi ya jumbe 1,000 kutumia wafanyakazi 13 walioajiriwa hapa,” Mwangi anadokeza.

Mwanamazingira John Karia, anaeleza kuwa azimio lao kubwa, mbali na kupata tija, ni kuwezesha wakulima wafugaji kuzalisha maziwa na nyama kwa pesa gharama ya chini ili kuimarisha faida wanayopata.

Kwa Mujibu wa Karia, kampuni yao huandaa warsha mbalimbali na wakulima nchini ili kuwaelimisha kuhusu nyasi hii maalum kama njia yao ya kukuza mtandao wa soko.

Karia anasema kuwa soko lao limepanuka sana ndani ya miaka minne iliyopita huku Mwangi akisema kuwa kulingana na tathmini yao, wamefikia asilimia tatu tu ya soko na wangali na kazi kubwa ya kuliimarisha.

  • Tags

You can share this post!

Jaji ajiondoa kusikiliza kesi ya ufisadi

MITAMBO: Mtambo unaosaidia wakulima kufunga vitita vya nyasi

T L