• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
ZARAA: Wakulima wapiga mabroka chenga

ZARAA: Wakulima wapiga mabroka chenga

Na SAMMY WAWERU

KATIKA mazingira ya mtaa wa kifahari wa Runda, na pembezoni mwa barabara ya Kiambu yenye shughuli nyingi inayounganisha Kaunti ya Kiambu na jiji la Nairobi, ni soko la wakulima la Nairobi.

Nairobi Farmers Market kama inavyotambulika, si kama masoko ya kawaida ambayo mazao mbichi ya shambani na bidhaa hupitia mikononi mwa madalali, yaani mawakala.

Ni la kipekee, wamiliki wa maduka wakiwa wakulima halisi, hatua inayosaidia wanunuzi kutangamana nao ana kwa ana.

Mhudumu wa duka moja katika Nairobi Farmers Market, Runda; soko linalomilikiwa na wakulima kutoka sehemu mbalimbali za nchi, akionyesha mazao mabichi ya shambani. PICHA | SAMMY WAWERU

Likiwa na jumla ya maduka 30 yanayouza kila aina ya mazao, limeondoa mahangaiko wanayopitia wateja kutafuta mazao na bidhaa bora.

Kenya, hasa kutokana na kuendelea kupanda kwa gharama ya maisha, ongezeko la hivi majuzi la bei ya mafuta ya petroli likizidisha ugumu, bei ya chakula ni ghali.

“Hapa Kenya, takwimu zinaonyesha gharama ya chakula ni ya juu mno, nyakati zingine ikikwea hadi asilimia 40 ya mapato jumla ya familia,” Jeff Mundia Meneja wa soko hilo asema, akielezea haja ya kushusha gharama hiyo.

Nchi kama vile Amerika, kila familia hutumia karibu asilimia 5 ya mapato jumla katika chakula.

Mundia huendesha mojawapo ya duka, The Farm Outlet ambayo huuza mazao ya shambani, ya familia yake yanayokuzwa katika Kaunti ya Tharaka Nithi.

Aidha, hulima matunda aina ya mapapai, karakara, ndizi, avokado na matikitimaji. Vilevile, hukuza malenge, nyanya, vitunguu na miwa. Mazao mengi yanayouzwa katika duka lake yanatoka shambani mwao.

“Mengine hununua kutoka kwa wakulima, hususan tusiyokuza,” Mundia anasema.

Anaiambia Akilimali kwamba sababu ya kuanzisha Nairobi Farmers Market, ilitokana na mahangaiko ambayo familia yake awali ilikuwa ikipitia kutafutia mazao soko.

Anakumbuka, Machi 2018 walikuwa wamezalisha zaidi ya kabichi 60,000 jitihada kutafutia mazao hayo soko zikigeuka kuwa kitendawili.

“Mawakala na wanaohusishwa na masoko waliishia kutia mfukoni kiwango kikubwa cha mapato,” Mundia anakadiria hasara waliyopata.

Ni kutokana na changamoto hizo, waliamua kutathmini njia mbadala kufikia wanunuzi.

“Tuliibuka na wazo kuleta pamoja wakulima waliopitia mahangaiko sawa na yetu, tuwe tukitangamana moja kwa moja na wateja,” asema.

Walitoa mapendekezo katika mitandao ya kijamii; WhatsApp na Facebook, wakihimiza walioridhishwa na mpango huo kujisajili. Mundia anasema majibu waliyopita, wengi waliridhia wazo la kuanzisha soko.

“Tuligundua changamoto ziliwiana, na wakulima walihitaji suluhu,” adokeza. Ujenzi wa soko hilo ulianza 2019, na kukamilika mwishoni mwa mwaka uliopita.

Joyce Gichana, na dadake pacha mzawa, Ruth Wakonyo, 24, wanamiliki duka, Jorujo Fresh Veggies, linalouza mazao kutoka shamba la wazazi wao lililoko eneo la Ruai, Nairobi.

Ruth Wakonyo (kulia – mwenye koti la buluu) na dadake pacha mzawa Joyce Gichana, wanamiliki duka, Nairobi Farmers Market, la kuuza mazao ya shamba la wazazi wao wanayokuza eneo la Ruai, Nairobi. PICHA | SAMMY WAWERU

Katika shamba lenye ukubwa wa ekari 30, hulima nyanya, pilipili mboga za rangi tofauti (hoho), vitunguu, matango na celery-kiungo kinachofanana na dhania.Hutumia maji ya kisima kuendeleza kilimo-biashara.

“Kando na kilimo katika eneo tambarare, tuna vivungulio 12 vilivyoko katika ekari mbili na nusu,” Joyce afichua.

Wawili hao na ambao wamekuwa wakitafutia mazao yao soko, hata hivyo wanasema haijakuwa rahisi kufanikisha shughuli hiyo, huku wakiridhia kuzinduliwa kwa Nairobi Farmers Market.

“Hata ingawa huwa tunasambazia masoko mengine, ni bora zaidi kuuzia mazao katika duka letu,” Ruth aeleza, akisema kila siku hupata fursa ya kipekee kutangamana na wateja na kuelewa mahitaji yao.

Mkabala mwa duka la mabinti hao, ni la Tevin Mutugi, Granary Food Store, analomiliki kwa ushirikiano na babake.

Huuza nafaka ambazo hukuza katika shamba lao lenye ukubwa wa ekari 20, Kaunti ya Meru. Hulima kunde, maharagwe aina tofauti, mbaazi na njahi.

“Tulianza na aina saba ya nafaka na sasa tunauza zaidi ya 30,” Mutugi asema, akiridhia soko hilo kusaidia kufikia wateja walaji wa nafaka.

Granary Food Store pia huongeza mazao thamani.

Mbali na mazao mabichi na bidhaa za shambani, soko hilo la aina yake pia huuza ya mifugo, kama vile maziwa, mayai, samaki na nyama.

“Husambaza maziwa kwa watu binafsi na mamia ya taasisi kama vile shule na hoteli,” anasema Jeremy Muthomi, mhudumu wa Home Deliveries Centre.

Blossoms and Beehives, ni duka jingine ambalo jukumu lake ni kuuza asali.

Kulingana na Dorah James, mfanyakazi, lililianza kama jaribio kuona iwapo wakazi wa Nairobi wanaenzi asali.

“Wengi wanageukia asali, hasa kipindi hiki taifa na ulimwengu unahangaishwa na janga la Covid-19 ili kuongeza virutubisho mwilini. Mbali na kuuza asali kwa wateja rejareja, pia huuza kijumla,” Dorah asema.

Mmiliki wa duka hilo ambalo pia huongeza asali thamani kwa kutumia viungohai mbalimbali, ni mfugaji wa nyuki Kaunti ya Pokot Magharibi na Baringo.

Uongozi wa soko hilo unasema uko tayari kushirikiana na wawekezaji wengine katika sekta ya kilimo-ufugaji-biashara, kuboresha wakulima na wateja kupata mazao bora.

You can share this post!

Ugaidi: 6 wafa, 33 wakiumia Uganda

Mkazi adai hakimiliki za ‘Bottom up’

T L