• Nairobi
  • Last Updated June 2nd, 2023 9:28 PM
AKILIMALI: Aamini unyunyiziaji huu utaifanya Kenya kupiku TZ kuzalisha vitunguu

AKILIMALI: Aamini unyunyiziaji huu utaifanya Kenya kupiku TZ kuzalisha vitunguu

Na SAMMY WAWERU

KWA muda mrefu, Kenya imekuwa ikitegemea taifa jirani la Tanzania kwa vitunguu vya mviringo (bulb onions) ili kukidhi hitaji la zao hilo nchini.

Hatua hiyo inatokana na uhaba wa vitunguu vinavyozalishwa hapa nchini. Idadi ya wakulima wanaovikuza ni ya chini mno, ikilinganishwa na wateja.

Wakulima waliofanikisha kilimo cha zao hili hata hivyo wanahoji mwanya uliopo unaweza kuangaziwa na kujazwa.

Gedion Makau, ni mkulima wa vitunguu vya mviringo Gishungu, Mai Mahiu, mpakani mwa Kaunti ya Kiambu na Nakuru, eneo ambalo ni kame na anasema muhimu zaidi ni kuzingatia vigezo faafu.

Huku kizingiti kikuu kikiwa uhaba na ukosefu wa maji kwa wakulima wenye nia, Makau anasema yanayopatikana hasa msimu wa mvua yanatosha kuifanya Kenya kujitegemea kuzalisha vitunguu.

Ni mkulima mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika ukuzaji wa vitunguu, na anasifia mfumo wa ‘beseni’ katika kupunguza matumizi ya maji, hasa eneo kame.

Aidha, ni mfumo chipuka ambapo udongo shambani unatengenezwa sawa na umbo la beseni. Miche ya vitunguu inapandwa ndani, na kulingana na Makau kiwango cha maji yanayonyunyiziwa hadi vitunguu kukomaa ni cha chini mno.

“Kimsingi, mfumo wa basin irrigation unapunguza gharama ya maji. Humwagilia mara moja kwa wiki, yanadumu kwa muda na kusalia ndani kunawirisha mimea na mazao kwani hayasambai kwingine,” anaelezea mkulima huyo.

Isitoshe, mfumo wa beseni ni bora katika kufanikisha matandazo (mulching), ili kuzuia uvukizi wa maji jua linapoangaza.

Beseni lina umbo la mstatili au mraba, vipimo vikiwa futi 2 kwa 1.5 ama futi 2 kwa 2. James Mbugua ambaye pia ni mkulima wa vitunguu Mai Mahiu amekumbatia mfumo huo, na anadokeza kila beseni linasitiri wastani wa miche 150.

“Gharama ya kuandaa beseni katika ekari moja ni kati ya Sh6,000 – 8,000,” Mbugua anaiambia Akilimali.

Mbali na kupunguza matumizi ya maji, mfumo wa beseni unasaidia kunawirisha mazao ya vitunguu. Gedion Makau anasema si ajabu ekari moja kuzalisha zaidi ya tani 10, sawa na kilo 10, 000.

Kati ya mwezi Aprili na Julai, vitunguu huwa haba nchini ambapo kilo moja huuzwa zaidi ya Sh100, bei ya shambani. Kulingana na Makau, Julai hadi Novemba hushuka hadi kati ya Sh20 – 40 kwa kilo, kwa sababu ya mazao mengi yanayotoka taifa jirani la Tanzania. Mkulima huyo anaeleza kwamba mwezi Novemba – Machi kilo moja hununuliwa wastani wa Sh50.

“Wakulima wakihamasishwa njia bora kukuza vitunguu, hatutakuwa na upungufu wa mazao. Tutaimarika kimapato kwa kuwahi soko la ndani kwa ndani,” Makau anasema.

Makau aliingilia kilimo cha vitunguu mwaka wa 2000, na kulingana naye Kenya inaweza kuwa mkuzaji mkuu, kwa kile anataja kama “nchi yenye udongo bora na hali bora ya anga kuvizalisha”.

“Kinachoua wengi moyo na kukata tamaa kuendelea kulima vitunguu, ni kukosa kutambua muda unaofaa kuvipanda ili walenge soko bora na lenye mapato ya kuridhisha,” anaelezea, akihimiza wakulima chipukizi kufanya utafiti wa kina, unaojumuisha soko, kabla ya kuingilia kilimo cha vitunguu.

Aidha, vitunguu vina uwezo kuhifadhika hadi kipindi cha miezi sita mfululizo, Makau akifichua kwa sasa ana zaidi ya tani 10 kwenye ghala.

Kulingana na Ngugi Mburu, mtaalamu, vinafanya vyema katika udongo usiotuamisha maji na wenye rutuba. Madau huyo anaelezea kwamba udongo unapaswa kuwa na uchachu wa asidi, pH, kati ya 5.8 – 6.8. “Mfumo bora, katika upanzi ambao umeibuka, ni matumizi ya beseni,” anasema mtaalamu huyo.

Vitunguu vinakomaa baada ya miezi mitano baada ya shughuli za upanzi.

You can share this post!

BIASHARA MASHINANI: Lishe mbovu nusura ifagie sungura wake;...

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 335 idadi jumla...