• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
AKILIMALI: Mitishamba matibabu tosha kwa ng’ombe wake

AKILIMALI: Mitishamba matibabu tosha kwa ng’ombe wake

CHARLES WASONGA na CORNELIUS MUTISYA

NI jambo la kutia moyo sana kuwaona watu wenye ujuzi mbalimbali wakitumia uvumbuzi wa kipekee kutatua shida zinazowakumba katika shughuli zao za kujiletea mapato.

Benson Kyengo mkazi wa kijiji cha Kaewa eneo bunge Kathiani, Kaunti ya Machakos ni mmoja wa watu kama hao.

Ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa ambaye hutumia mbinu mbadala kupambana na maradhi ya mifugo katika jitihada za kuongeza mapato.

Hutumia dawa za miti shamba kutibu ng’ombe wake aina ya Jersey na Freshian badala ya dawa za kisasa za kupambana na maradhi ya mifugo.

Mkulima huyo ambaye, ana shahada ya Diploma katika taalumu ya tiba ya mifugo kutoka Chuo cha Kiufundi cha Kabete, alisema alijipatia mafunzo kuhusu tiba ya kiasili kutoka kwa mzee mmoja, ambaye anabana jina lake, kutoka kaunti jirani ya Kitui.

“Baada ya kuhitimu kutoka chuoni Kabete mnamo 2012, niliamua kutafuta mafunzo zaidi kuhusu tiba za kiasili baada ya kugundua kuwa wafugaji wengine hupendelea dawa za kiasili kuliko dawa za kisasa. Wao husema kuwa dawa za kisasa zimetengenezwa kwa kemikali hatari ambazo huwa rahisi kupenyeza kwenye maziwa,” Kyengo anaeleza.

“Lakini kwa sababu nilikuwa na elimu pevu kuhusu afya ya mifugo, niliamua kutumia upevu huo kufanya utafiti zaidi kuhusu mimea inayoweza kutumia kutengeneza dawa ya mifugo,” anaongeza.

Kyengo, 33, anasema utafiti wake uligundua kuwa matawi ya miti kama vile mpera, ndimu na “wondering jew”, almaarufu ‘’mukengesya’’ kwa lugha ya Kikamba ni tiba kamili kwa maradhi mengi haswa yanayoathiri ng’ombe wa maziwa.

“Dawa ya majimaji iliyotengenzwa kwa mmoja wa “black jack” ama “munzee” kwa Kikamba, pia ni bora zaidi katika kuangamiza kupe na wadudu wengine hatari kwa mifugo.”

“Vile vile, niligundua kuwa dawa za kiasili zilizotengenezwa kutokana na miti kama hii ni kinga dhidi ya maradhi ya ng’ombe wa maziwa. Hii ni kando na mbinu nyingine za kuzuia magonjwa na wadudu, kama vile kudumisha usafi kwenye zizi na kutumia lishe bora,” anaeleza.

Kulingana na Kyengo baadhi ya maradhi yanayoathiri ng’ombe wa maziwa ni kama vile; homa inayosababishwa na kupe, (East Coast Fever), maradhi yanayoathiri miguu na midomo ya ng’ombe (Foot and Mouth Disease), maradhi ya matiti (Mastitis), “Cowpox”, “Listoriosis”, miongoni mwa magonjwa mengi.

“Maradhi hayo na mengine husababisha ng’ombe kukosa hamu ya kula, kupunguza kiwango cha maziwa na hata kifo, na hivyo kumletea mkulima hasara isiyomithilika,’’ asema.

Hivi sasa, Kyengo anamiliki ng’ombe 10 wa maziwa ambapo kila moja huzalisha kati ya lita 20 na 25 za maziwa kila siku.

Bei ya lita moja ya maziwa ni Sh 50 kwa wateja wa kawaida.Hii inamaanisha kuwa, mkulima huyu hutia kibindoni kati ya Sh10, 000 na Sh12,000 kila siku kutokana na mauzo ya maziwa.

Kyengo anasema, wateja wake wakuu ni wamiliki wa mikahawa mjini Machakos, kituo cha kibiashara cha Kathiani na masoko ya karibu kama vile King’atuani, Nzaikoni na Kaviani.

“Wateja wanapenda maziwa yangu kutokana na sababu kwamba mimi hutumia dawa za kiasili kuzuia na kutibu maradhi. Aidha, lishe ambayo mimi hutumia ni ile ya kiasili isiyotengenezwa kwa kemikali,” anaeleza, akiongeza kuwa watu wengi siku hizi hawataki vyakula vyenye kemikali ambazo husababisha maradhi sugu kama saratani.

Kyengo asema alianza ufugaji ng’ombe wa maziwa mnamo 2013 kwa mtaji wa Sh20, 000 pekee alizotumia kununua ndama watano.

Mwaka jana hata hivyo, mkulima huyo alikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa soko la kutegemewa kwa sababu mikahawa mingi ilifungwa kufuatia janga la Covid-19.

“Nilipitia wakati mgumu kwa sababu shule nazo zilikuwa zimefungwa. Lakini sasa naendelea kupata afueni kibiashara maana mambo sasa yameanza kunyooka baada ya serikali kulegeza masharti ya corona na mikahawa kuruhusiwa kuhudumu hadi saa mbili za usiku,’’ asema.

You can share this post!

Vita vikali Afghanstan huku zaidi ya watu 40 wakiuawa

Mkuzaji stadi wa matikitimaji Pwani anayetaka vijana...