• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 7:55 AM
AKILIMALI: Mwalimu mwenye bidii ya mchwa ashauri vijana kutafuta njia za kujiajiri

AKILIMALI: Mwalimu mwenye bidii ya mchwa ashauri vijana kutafuta njia za kujiajiri

Na HAWA ALI

SIKU zote kilio cha vijana wengi wanaohitimu elimu ya chuo kikuu nchini kimekuwa ni ukosefu wa ajira.

Kwa kuwa ndoto ya wengi ni kupata kazi, makazi bora, magari na hata fursa za kufanya anasa, ukosefu wa ajira umekuwa kikwazo kikubwa cha kutimiza ndoto walizonazo.

Kimsingi, mawazo na mtazamo kuhusu maisha wakiwa vyuoni, huwa tofauti na hali halisi wanapohitimu masomo.

Wengi hubaki wakizunguka na bahasha zenye barua ya maombi ya kazi kwenye ofisi mbalimbali ama kutuma maombi ya kazi mitandaoni bila mafanikio na hivyo kuishia kulalamikia ugumu wa maisha.

Mwalimu wa Shule ya Upili ya St James Kianjai, Meru, Sebastian Mbae anasema alianza kufikiria kujiajiri tangu akiwa Kidato cha Kwanza.

“Kwa sababu nilikulia kijijini hivyo nikajifunza kushona viatu, nilipoanza kidato cha kwanza niliamua kuwa mshona viatu vya wanafunzi wenzangu,” anasema.

Tangu hapo Mbae akajulikana kwa jina la mshona viatu.

Wanafunzi wote walioharibikiwa na viatu walikimbilia kwake naye hakuwaangusha kwani alitumia vyema siku za mwisho wa wiki kutengeneza viatu na kujipatia chochote.

Baada ya safari ndefu ya kuishi kwa shida kama mtoto anayetoka familia masikini, sasa Mbae ni msomi wa shahada ya digrii, huku akiwa njiani kuanza masomo ya shahada ya pili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Nje ya taaluma ya ualimu, Mbae ni mkulima hodari wa mazao ya mboga na matunda.

Aliamua kukuza mboga za kienyeji kama vile managu, terere, mchicha na kadhalika kwa sababu ya virutubisho vingi mwilini.

“Ninapenda sana vyakula asilia kwa sababu ya kinga kuu ya mwili, zikiwemo mboga za kienyeji,” alidokezea Akilimali shambani mwake Kianjai, Tigania Magharibi.

Siku zote Mbae alitamani kuwa mwalimu wa shule ya upili, na alitamani sana kuwa mwalimu wa Bayolojia na Kilimo, hivyo akaamua kusomea taaluma hiyo.

Alifuzu mwaka 2015 na kuajiriwa katika baadhi ya shule za kibinafsi kabla ya kuajiriwa na Tume ya Kuajiri Walimu nchini (TSC).

Kwa kuwa alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliobahatika kupata mkopo wa elimu ya juu (HELB), maisha yake yalikuwa mepesi kidogo.

“Sikuwa muoga wa kujaribu, nilipopata mkopo wangu kwa mara ya kwanza nilichukua baadhi ya fedha nikazitumia kama mtaji,” anasema.

Wakati huu hakuendelea kushona viatu. Akiwa mwaka wa kwanza chuoni, alianzisha biashara ya viatu vya mitumba na nguo akiwauzia wanafunzi wenzake.

“Biashara yangu iliongezeka siku hadi siku, nikapata faida kubwa iliyoniwezesha kununua shamba katika kijiji cha Uringu, Meru,” anasema.

Shughuli zake za biashara chuoni hazikumzuia kutia bidii masomoni kwani aliibuka mmoja wa wanafunzi bora.

“Ukiniuliza niliwezaje kufanya hayo yote kwa pamoja, nitakujibu kuwa nilikuwa na njaa ya mafanikio na nilifahamu mafanikio yoyote huja kwa jitihada na kuwa na mipango sahihi,” anasema.

“Nililima matunda, mboga na maharagwe. Niliuza mazao yangu sokoni na niliajiri vijana 10 ambao walikuwa wakinisaidia kazi za shamba na biashara zangu za mitumba,” anasema.

Mbae anasifia Serikali kwa kubadilisha mtaala wa elimu kutoka ile ya nadharia wa 8-4-4 kwenda katika mtaala wa vitendo yaani CBC.

Anasema kinachowatatiza wahitimu wengi ni kwa sababu hawajaandaliwa kupambana na changamoto za kimaisha, hivyo wengi wanasubiri kuajiriwa.

“Nyanya yangu alinifundisha kushona viatu tangu nikiwa mdogo, nilijifunza elimu ya kujitegemea kutoka kwa wazazi wangu na leo hii sitateseka kutafuta kazi kama wenzangu,” anaeleza.

Anasema ni aibu kwa mwanafunzi kuhitimu chuo kikuu ikiwa hajui hata kushona nguo yake iliyochanika.

You can share this post!

Makala ya Dimba – Beach Bay FC

AKILIMALI: Hakujua sabuni, mafuta kutoka kwa maziwa ya...