• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
AKILIMALI: Unavyoweza kudumisha rutuba ya udongo kwa kutumia maharagwe na mimea ya aina hiyo

AKILIMALI: Unavyoweza kudumisha rutuba ya udongo kwa kutumia maharagwe na mimea ya aina hiyo

Na SAMMY WAWERU

WAKULIMA wengi wamekuwa mateka wa fatalaiza zenye kemikali kuimarisha rutuba ya udongo.

Wataalamu wa masuala ya kilimo wanaonya mazoea ya fatalaiza na dawa zenye kemikali, yanadhoofisha virutubisho vya udongo.

Ndio maana unapokodi shamba ambalo limezoeshwa pembejeo za aina hiyo, ukose kuzitumia kiwango cha mazao kitakuwa cha chini mno.

Udongo wenye rutuba unawekwa kwenye mizani kutokana na madini na virutubisho vilivyomo.

Madini ya Nitrojini ni kati ya yale muhimu zaidi katika shughuli za kilimo.

Watengenezaji wa fatalaiza huhakisha haikosi kiwango cha juu cha Nitrojini, kwa sababu ndiyo nguzo ya mazao bora.

Caroline Muriithi ambaye ni mkulima wa matunda kama vile ndizi, mapapai, karakara na avokado, anasema badala ya kutumia fatalaiza, kati ya mitunda hupanda mimea inayoorodheshwa katika familia ya Legumi.

Caroline Muriithi (kushoto)bakiwa katika eneo la shamba ambako anapanda migomba ya ndizi huko Ngariama Kusini, Mwea, ambapo pia kati ya migomba hukuza maharagwe na ndengu kuongeza Nitrojini na kuzuia kwekwe kumea. Picha/ Sammy Waweru

“Kwa mfano, eneo lenye migomba ya ndizi, hupanda maharagwe na ndengu,” adokeza.

Ni kundi la mimea ya familia ya Legumi iliyosheheni madini faafu ya Nitrojini.

Mfumo huo unapendekezwa na wataalamu wa kilimo.

“Ni mimea inayotambaa ardhini (cover crops), na kando na kuongeza Nitrojini kwenye udongo huzuia kwekwe kumea,” Daniel Mwenda, mtaalamu, asema.

Akihimiza wakulima kukumbatia ukuzaji wa maharagwe, hasa kati ya mimea na pia kuafikia kigezo cha mzunguko (crop rotation), mdau huyu anasema mimea ya familia ya Legumi husaidia kuboresha rutuba.

“Inasaidia kuongeza Nitrojini kwa kasi na kwa kiwango cha juu,” asema.

Mbali na maharagwe na ndengu, maharagwe asilia ya kijani maarufu kama minji pia yanapendekezwa.

“Ninapofanya mavuno ya viazi na mboga, hurejesha minji ili kuboresha rutuba kwenye udongo,” Timothy Mburu, mkulima Nyeri asema.

Mburu ni mkuzaji hodari wa viazimbatata, mboga kama vile kabichi, spinachi na sukuma wiki, na pia vitunguu.

Matumizi ya mbolea ya mboji pia vunde, husaidia kuongeza kiwango cha Nitrojini kwenye udongo.

Ni mbolea iliyotengenezwa kwa kuchanganya samadi ya mifugo, matawi na majani ya mimea tofauti, kisha inafunikwa kwa muda wa miezi kadhaa ili kuiva sambamba.

You can share this post!

WANGARI: Uhifadhi wanyamapori ni turathi kuu kwa vizazi...

NCIC yaonya wanasiasa wasiotaka kuona washindani ngomeni