• Nairobi
  • Last Updated December 6th, 2023 9:00 PM
Anavyovuna katika biashara ya kuchoma nyama   

Anavyovuna katika biashara ya kuchoma nyama  

NA SAMMY WAWERU

IDADI ya watu ulimwenguni ikikadiriwa kuongezeka kwa kasi ifikapo 2050, ulaji nyama unatarajiwa kuongezeka mara dufu.

Ni ongezeko ambalo linapaniwa kujiri na maendeleo hasa katika sekta ya ufugaji.

“Ufugaji ni mojawapo ya sekta inayotarajiwa kuimarika pakubwa, wafugaji wazidi kukaza kamba kuwekeza kwa kiwango cha juu,” asema Harry Kimtai, aliyekuwa Katibu katika Wizara ya Mifugo.

Kimtai kwa sasa ndiye katibu mpya Wizara ya Afya, kufuatia mageuzi ya majuzi ya Rais William Ruto katika baraza lake la mawaziri yaliyolenga makatibu.

Mfanyabiashara John Njuguna, akichoma nyama. Picha / SAMMY WAWERU

Kabla mabadiliko hayo, Akilimali Dijitali ilikuwa imefanya mahojiano ya kipekee na afisa huyo wa ngazi ya juu serikalini ambapo aliarifu kuhusu mianya tele iliyopo katika sekta ya ufugaji.

Amekuwa katika Wizara ya Mifugo, tangu serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Kulingana na Kimtai, uongezaji nyama thamani ndio mtandao mwingine wenye mapato ya haraka.

“Ni mwanya unaoweza kuinua wafugaji na washirika katika mtandao wa ufugaji nchini.”

John Njuguna, mfanyabiashara wa nyama Nairobi anaungama kauli ya Katibu huyo akikiri usindikaji nyama (processing) kama wenye wenye mapato chungu nzima.

Nyama choma iliyoandaliwa na John Njuguna, mwasisi wa Ruai Kikopey Choma Zone. Picha / SAMMY WAWERU

Mwasisi huyo wa Ruai Kikopey Choma Zone katika barabara ya Kangundo, huchoma, kukaanga kwa viungo mbalimbali nyama ikiwemo kuweka dhania, pilipili hoho (zile kali), vitunguu saumu na viazi na anasema hatua hiyo inateka soko lenye ushindani mkuu.

Hata ingawa bucha yake huuza nyama mbichi, uongezaji thamani anasisitiza faida yake ni ya kuridhisha.

“Kilo moja ya nyama mbichi ni Sh700, na inapoongezwa thamani huchezea zaidi ya Sh900,” aelezea.

Mfanyabiashara huyo ameegemea uuzaji wa viungo maalum vya mifugo kama vile shingo, bega, miguu, loin, flank, breaks na shank.

Aidha, nyama na mifugo anaojishughulisha nao ni mbuzi, nguruwe, kuku na samaki.

John Njuguna, akihudumia wateja wakati wa Maonyesho ya Nyama Kenya 2023, katika Ukumbi wa KICC, Nairobi. Picha / SAMMY WAWERU

Njuguna hutoa nyama zake kutoka kichinjio cha Thika, Kiamaiko na Kiserian.

Mfanyabiashara huyo hata hivyo, analalamikia kupata hasara nguvu za umeme zinapopotea.

Hajawekeza katika mashine na mitambo ya kisasa kuhifadhi nyama kama vile jokofu.

John Njuguna alikuwa miongoni mwa washirika katika mtandao wa nyama nchini waliohudhuria Maonyesho ya Nyama Kenya 2023, katika Ukumbi wa KICC, Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

Viva, Miguna Miguna amsuta Rais Museveni kwa pendekezo...

Magavana walia serikali yaua ugatuzi

T L