• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
Askari aangushiwa kichapo kwa madai ya wizi wa ng’ombe  

Askari aangushiwa kichapo kwa madai ya wizi wa ng’ombe  

NA JESSE CHENGE

HALI ya mshikemshike ilishuhudiwa eneo la Lugari, Kakamega askari na raia walipokabiliana, wakazi wakilalamikia afisa ‘kuiba ng’ombe’.

Mtafaruku ulijiri, baada ya wananchi Lumakanda kuvamia afisa huyo na kumuangushia kichapo wakimhusisha na wizi wa mifugo.

Inasemekana fujo zilitokea mmoja wa wenyeji alipokosa ng’ombe wake zizini, hatua iliyomshawishi kufahamisha wanakijiji wenza.

Mmoja wa wanaoosha magari, alipuliza kipenga gari la polisi alilopelekewa kung’arisha lilipoonyesha dalili kutumika kusafirisha ng’ombe.

“Gari hili la askari nimekuwa nikiletewa mara nyingi kuliosha, ila leo nimepata kinyesi kikubwa cha ng’ombe jambo linaloibua maswali,” alisema Luka Kasuku, muosha magari Lumakanda.

Huku tukio hilo likiibua maswali chungu nzima kuhusu mienendo na maadili ya polisi eneo hilo, Benson Somek, mhudumu wa bodaboda na Boaz Mugunda, mkazi walidai askari Lumakanda wamekuwa wakihusishwa na uhalifu, ikiwemo wizi wa mifugo.

Kulingana na Samson Maiyo na Timothy Mahindi wamiliki wa ng’ombe huyo, alitoweka usiku na kusfirishwa eneo lisilojulikana.

Kamanda wa Polisi eneo hilo, Bernard Ngung’u alihimiza wananchi wenye ushahidi kujitokeza ili kusaidia katika uchunguzi.

“Jukumu la askari ni kulinda wananchi na kuboresha usalama. Hata hivyo, tutafanya uchunguzi kubaini ukweli wa madai ya wananchi,” Bw Ndung’u alisema.

Afisa huyo aliahidi kwamba endapo polisi husika atapatikana na hatia, sharia haitakuwa na budi ila kuchukua mkondo wake.

“Suala hili litachunguzwa na makachero wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI),” alisema, akikashifu vikali hatua ya gari la polisi kutumika kusafirisha ng’ombe.

Baadaye, ng’ombe huyo alipatikana akiwa amefichwa katika kaunti jirani ya Bungoma.

  • Tags

You can share this post!

Elimu ilivyochangia katika ustawi wa nchi tangu 1963

KRA yamezea mate mapato ya mama mboga, bodaboda

T L