• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 8:09 PM
BAHARI YA MAPENZI: Mke asilazimishwe kuacha kazi ili kutekeleza majukumu ya nyumbani

BAHARI YA MAPENZI: Mke asilazimishwe kuacha kazi ili kutekeleza majukumu ya nyumbani

NA BENSON MATHEKA

KUNA watu wanaolazimisha wake wao kuacha kazi punde tu wanapowaoa na kutoa sababu mbali mbali za kuwataka kufanya hivyo.

Baadhi ya sababu huwa zina mantiki na zingine huwa hazina msingi. Zilizo na mantiki ni iwapo mume ana mpango wa kumwezesha mke kuwa na njia mbadala ya mapato kama vile kumwanzishia mradi au biashara.

Na hata kama ana mpango huo, haifai kumlazimisha kuacha kazi. Anafaa kumuomba kufanya hivyo, kujadiliana bila vitisho na kufikia uamuzi.

Uamuzi wa kuacha kazi ukifikiwa kupitia majadiliano, hakuna anayeweza kulaumu mwengine hali ikibadilika baadaye na mtu kutamani kazi aliyoacha.

Mtu anaweza pia kumuomba mkewe kuacha kazi iwapo kazi yenyewe ni hatari kwa maisha yake au kwa ndoa yao.

Hii pia inahitaji majadiliano ya kina na kupima kiwango cha hatari na kubaini iwapo kinaweza kufanya mke aache kazi.

Hali kama hizi zinakubalika mradi tu wanandoa wanajadiliana na sio kulazimisha mke kuacha kazi bila sababu maalumu.

Kuna wanaume waliojawa na wivu kiasi cha kudhani wake wao wanamezewa mate na wanaume wanakofanya kazi au wanaokutana nao katika shughuli za kikazi.

Mawazo kama haya yanaonyesha upungufu wa busara na hekima kwa kuwa kabla ya kukutana na mwanadada na kuanza kuchumbiana naye, huwa anafanya kazi na wanaume au kukutana nao na alichagua kuwa mkeo miongoni mwa wanaume wengi.

Kwa hakika, unaweza kumfanya kuwa na nafasi nzuri ya kupatana na wanaume unaodhani utamwepusha nao kwa kumlazimisha kuacha kazi.

Sisemi ni vibaya mwanamke kuacha kazi akiolewa na kuanza familia, ninachosema ni kuwa kuacha kazi kunafaa kuwa kwa hiari yake na pia baada ya kujadiliana na mumewe.

Ni tabia chwara kwa mwanamume kumshurutisha mkewe aliyekuwa akijitafutia hela zake na kuishi maisha mazuri aache kazi ili awe akimtegemea.

Lengo la mwanamume kama huyo huwa ni kukufanya mtumwa ili uwe ukimtegemea.

Hii pia huwa inapunguza mapato ya familia yenu. Japo kuna wanawake wanaobana mshahara wao wakiolewa na kutegemea mume kwa kila kitu, hakuna anayeweza kukosa kuokoa jahazi kwa ujira wake hata kama ni mdogo hali mbaya zaidi ikitokea.

Kwa hivyo, wanaume wanapaswa kukoma kuwa na hofu na kuruhusu wake wao kufanya kazi walizowapata wakifanya au wanazopata wakiwaoa.

Kupata kazi sio rahisi katika ulimwengu wa sasa na ni makosa kumlazimisha mkeo kuiacha kwa sababu ya wivu au kutaka kudhihirisha ubabe katika boma.

Kufanya kazi kunamfanya mke kupanua mawazo na kujifunza mambo mengi ya kuboresha maisha, na hivyo basi waume wanafaa kuwaunga mkono badala ya kuwavunja moyo.

Hata kama ni kwa hiari yake, mke hafai kuacha kazi bila mpango maalum wa maisha hata kama mumewe ni tajiri wa kupigiwa mfano.

Mke pia ana haki ya kutafuta mali yake sawa na mume, na zaidi ya yote si busara kumlazimisha mwanamke kuacha kazi aliyotumia pesa na miaka mingi kuwekeza au kusomea kwa sababu unataka akuhudumie kama mkeo.

Kuna wanawake wanaofanya kazi zinazowafunga zaidi lakini wanajua jinsi ya kusawazisha muda wao wa kikazi na wa nyumbani.

  • Tags

You can share this post!

PENZI LA KIJANJA: Kuchagua mchumba kunahitaji hekima si...

Manchester City kunusia taji leo Jumapili ikikomoa Everton

T L