• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 3:17 PM
BAHARI YA MAPENZI: Ubunifu wahitajika kudumisha mvuto

BAHARI YA MAPENZI: Ubunifu wahitajika kudumisha mvuto

SIZARINA HAMISI Na BENSON MATHEKA

MARA nyingi maisha ya ndoa huchosha, hupoteza mvuto na wakati mwingine hupoteza ladha ya mahaba.

Katika hali kama hiyo kunakuwa na umuhimu wa kuweka juhudi za pamoja kwa wanandoa kuongeza ubunifu ili kuweza kuleta ladha katika maisha yao ya pamoja.

Wapo ambao baada ya muda wanachoka aina ya mahaba ambayo yamekuwa kawaida baina yao na huenda mmoja akataka kumueleza ama kumuonyesha mwenzake yale ambayo anaona yanaweza kuleta mabadiliko mazuri katika uhusiano wao.

Wapo ambao wanahofia kuchukua hatua wakihofia kueleweka vibaya na wenzao, kwani wakati mwingine unaweza kupata mume ana hasira za kifaru, mbishi na wivu wake ni wa kuua mtu.

Msomaji mmoja wa safu hii aliwahi kunieleza shida anayopitia wakati ule wa faragha na mumewe, kwamba anapojaribu kumbusu mumewe, anafungua mdomo wote na meno yanabaki nje. Matokeo yake huyu dada anakosa hamu ya kuendelea na busu. Akafungua roho yake zaidi kwamba mumewe hataki watumie mitindo tofauti kwenye shughuli.

Mawasiliano ni kiungo muhimu katika ndoa na hatua ya kwanza ni kuwa wazi kwa mwenzako. Iwapo ni mke, zungumza na mumeo kwa upendo.

Vilevile unaweza kumfundisha kwa kuweka mazingira ya “tujaribu” na sio kumwonyesha wazi unamfundisha. Mfano unaweza kumwambia tujaribu kubusu katika mitindo tofauti kama vile kwaheri, nakutamani, nakutaka, nasikia raha, nimechoka, nakupenda na mingine mingi.

Suala la muhimu kuzingatia ni kwamba hakuna anayeweza kuokoa ndoa yako isipokuwa wewe na mumeo. Je, mtaiboreshaje ndoa?

Kwa kujaribu kuboresha yaliyopo na wala sio kumbadili mwenzako.

Naamini hadi wapenzi wanapofikia uamuzi wa kufunga ndoa wanakuwa wamezoeana na wako huru kufanya chochote au kufanyiana lolote iwe kiutani ama kwa makini.

Hivyo nafasi hiyo inaweza kutumika katika kuweka wazi zile kero ambazo wote wawili huenda wanazipitia wanapokuwa faragha na kuwa tayari kujaribu mbinu mbalimbali kwa mujibu wa walivyozungumza na kuelewana. Bila kusahau suala zima la kutumia muda wa kutosha kutayarishana na kufurahishana.

Tatizo la wanawake na hata wanaume ni kushindwa kuwa huru katika mapenzi.

Wapo wanaume ambao wakishafunga ndoa, huwa wanadhani kazi imekwisha na jukumu la kuboresha mapenzi na uhusiano nalo limeisha na kusahau kwamba ndoa ni hatua ya kwanza ya kuweza kudumisha uhusiano na ukaribu na mke, kwamba baada ya ndoa, inafuata kazi ya ziada ya kubuni njia mbalimbali za kuchochea penzi lisichoke na mke pia asikuchoke.

Kuelewa yale ambayo yalimvutia kwa mkewe na kuhakikisha yanaendelea hata baada ya ndoa. Zile juhudi zilizowekwa katika kumtongoza zinatakiwa ziendelee hata baada ya ndoa.

Halikadhalika kwa wanawake, wakishaolewa na kuwekwa ndani, hudhani kwamba jukumu lao la kumvutia mume limefika tamat, bila kutambua kwamba hapo ndipo kazi inapoanza.

Jukumu la mke baada ya ndoa pia litakuwa ni kuendelea kumvutia mumewe kwa yale anayopenda na kuhakikisha anampatia huduma zile anazotegemea kutoka kwake.

[email protected]

RAFIKI yangu mmoja alifananisha ndoa na nyumba inayopaswa kupakwa rangi upya baada ya muda fulani.

Alisema rangi ya nyumba huwa inapata vumbi au kufifia miaka inaposonga na hivyo wanaoishi ndani au wamiliki wake wanapaswa kuifanya upya ili kuitia nakshi kwa kuwa hakuna anayefurahia kuishi katika mazingira yasiyopendeza.

Rafiki yangu huyo alikuwa sahihi, ndoa inahitaji ubunifu wa wahusika wote ili izidi kunawiri na hii sio tafadhali.
Mtu anapofanyiwa jambo kwa muda mrefu huwa linachoshwa na kudumaza ndoa ambayo kwa hakika inafaa kukua na kupata nguvu miaka inaposonga.

Ndoa ambayo wahusika wanakosa ubunifu huwa inakuwa dhaifu miaka inaposonga. Masuala ya ndoa sio tofauti na mlo ambao unaongezwa ladha kupitia ubunifu wa mpishi.

Githeri haiwezi kuchosha ikiongezwa viungo tofauti kila siku lakini ikiwa mpishi atazoea kupakulia mahindi na maharagwe kavu miaka nenda miaka rudi, afya ya anayepika na kupikiwa itadhoofika.

Ubunifu katika ndoa ni mpana sana na wanaoukumbatia wameshuhudia manufaa yake.

Unanogesha ndoa na kuleta wahusika karibu zaidi.

Nazungumzia ubunifu wa chochote kinachohusiana na kujenga ndoa imara; mawasiliano, masuala ya faragha, kuzawadi mtu wako, unavyomdekeza na kumtunza kwa nyakati na vipindi tofauti vya ndoa yenu.

Hautarajii mke au mumeo awe jinsi alivyokuwa mlipokutana mara ya kwanza au mama na baba wa watoto watatu awe alivyokuwa kabla hamjapata watoto.

Mahitaji hubadilika pia, ya kimwili, hisia na akili. Mke na mume mzuri ni anayebadilika na wakati huku akibuni mambo au mbinu mpya za kuhakikisha ndoa inakuwa imara.

Kinachofanya ndoa kuchosha ni lugha na vitendo vya mtu kwa mume au mkewe kuhusu masuala fulani yenye umuhimu kwa ndoa au kwa mtu wake.

Hivyo basi ni muhimu kujua jinsi ya kuzungumzia mtu wako kwa lugha isiyoleta maudhi na kumfanyia kinachostahili kwa wakati na kukinogesha uwezavyo hadi akutambue.

Inasemwa maneno matamu humtoa nyoka pangoni na ndivyo ilivyo katika ndoa, ubunifu katika kutumia lugha hata wakati wa shughuli muhimu ya tendo la ndoa.

Aidha, unachangia pakubwa kuimarisha uhusiano hasa panapotokea hali ya kutoelewana kati ya mume na mke. Katika ndoa nyingi, unapata ni ubunifu wa mwanandoa mmoja unaofanya ndoa kunawiri.

Hivyo basi, usisubiri mume au mkeo afanye mambo unayoweza kuanza au kumfunza yanayoweza kunufaisha ndoa yenu.

Hata hivyo, kama nilivyosema hapo juu itategemea lugha na mbinu unatakayotumia kumfunza au kumdhirishia kwamba unanuia mema kwa mawazo, mipango au vitendo vyako.

Kila hatua ya ubunifu katika ndoa inafaa kuwa kwa kiasi na ndani ya uwezo wa wahusika na kwa nia njema. Haifai kuwa ya siri. Kwa hakika, katika ubunifu wa masuala ya ndoa huwa hakuna siri kabisa.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Orengo aponda wabunge ‘waasi’ Azimio akisema...

Maelfu waaga mtumishi wa umma aliyefaa wengi

T L