• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Dorcas Gachagua: Ufukara katika familia nusra usababishe nijitie kitanzi

Dorcas Gachagua: Ufukara katika familia nusra usababishe nijitie kitanzi

NA SAMMY WAWERU

MKE wa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Bi Dorcas Gachagua, amesimulia jinsi nusra ajitie kitanzi kufuatia mahangaiko yaliyozingira familia yake.

Akihutubia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Daystar jijini Nairobi mnamo Septemba 19, 2023, Bi Gachagua alifichua kwamba akiwa mwanafunzi karibu ajiondoe uhai.

Aidha alidokeza kwamba jaribio hilo lilichochewa na ufukara uliozingira familia yake wakati akisoma.

“Nikiwa Mama wa Pili wa Jamhuri ya Kenya, ninawaambia kwamba wakati mmoja nikiwa katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU), kwa sababu ya hali (akimaanisha changamoto) iliyokuwa nyumbani karibu nijitie kitanzi,” Bi Gachagua alielezea.

Matamshi hayo, yaliashiria tatizo la afya ya kiakili alilopambana nalo, ambalo kulingana naye lilimsababishia msongo wa mawazo.

Bi Gachagua anaendeleza kampeni kuokoa vijana, hasa waliolemewa na kero ya matumizi ya dawa za kulevya, mihadarati na pombe haramu na hatari.

Kwa sababu ya mila, itikadi na maono ya jamii za Kiafrika kuhusu tatizo la afya ya akili, Pasta Dorcas alisema suala hilo linaendelea kupuuzwa jambo ambalo linazidi kuchangia wengi kuhangaika.

Alitoa mfano wa mama aliyesheheni ugomvi, mzazi mwenye hasira au dada anayerusha cheche za maneno kwa kupiga kelele, wengi wakidhania wamepagawa au ni wendawazimu, ila kulingana na Bi Dorcas Gachagua baadhi yao wanaugua tatizo la afya ya akili.

“Hupaswi kujibadilisha, ila unapaswa kubadilisha unavyofanya mambo…Tafuta mtu na uzungumze naye, mwaga yaliyo moyoni… Na ufahamu kuwa si wewe pekee unayepitia changamoto za maisha. Ni wengi wana shida ya afya ya akili. Ninawaahidi kama mama kuna matumaini. Usife moyo kwa sababu kuna uwezekano uwe kwenye hali hiyo na ushinde,” Bi Gachagua akaelezea.

Visa vya matatizo ya afya ya kiakili nchini vinazidi kuongezeka, hali ngumu ya maisha na uchumi ikitajwa kuchangia pakubwa.

Baadhi ya wahusika, wamejipata kujitia kitanzi.

Wasio na ajira, na pia maafisa wa polisi ni miongoni mwa makundi yaliyoandikisha visa vya juu.

Bi Gachagua anaendeleza kampeni kuangazia changamoto hiyo, akilenga vijana na taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu.

  • Tags

You can share this post!

Maandalizi ya Maonyesho ya ASK Nairobi 2023 yakamilika

Wakazi waachwa gizani kwa saa 4 Al-Shabaab wakiharibu mnara...

T L