Na SINDA MATIKO
VITU vingi vimesemwa kumhusu soshiolaiti Hamisa Mobetto na kati yavyo ambavyo anakanusha, ni kufanyiwa upasuaji wa uso ili kunogesha mvuto wake.
Lakini mwanamitindo huyo wa zamani ambaye kwa sasa shughuli zake ni za uinfluensa, kakanusha kufanyia uso wake ukarabati.
Aidha aliweka wazi kwa nini tofauti na mastaa wengi, hajawahi kuchora tatoo mwilini wake.
“Mimi sina tatoo hata moja kwenye mwili wangu. Sipendi tu lakini napenda kuziona kwenye miili ya watu wengine lakini sio wa kwangu. Pia mimi sijawahi kufanya upasuaji wowote kwenye uso wangu. Uso wangu upo kama nilivyozaliwa,” alifunguka juzi kati akiwa kwenye Insta Live alikojibu maswali kibao ya mashabiki wake.
Hata hivyo, mama huyo wa watoto wawili alikosa kubainisha tetesi zinazodai kuwa kafanya upasuaji kunogesha shepu na makalio yake.
***
SUPASTAA wa Bongo fleva, Diamond Platnumz ameweka wazi kuwa atapambana sana kuhakikisha kuwa binti yake Tiffah hatakuwa msanii.
Platnumz anasema uamuzi huu umechangiwa na mengi aliyoweza kuyaona kwa zaidi ya miaka 10 akiwa kama msanii hivyo hangependa kabisa kumwona binti yake wa pekee aliyezaa na soshiolaiti Zari Hassan akifuata nyayo zake.
“Msanii wa kike kuna mambo mengi lazima apitie kama anataka kuwa msanii. Ni changamoto kubwa sana kiasi cha kuuza mpaka utu lakini ndio mfumo ulivyo. Sitokubali na sitaki hata kidogo mwanangu wa kike kuwa msanii.”
Diamond anasema kwa sasa anatengeneza mifumo ya kumwandaa Tiffah kuwa meneja wa wasanii lakini sio kuwa msanii.