• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:15 PM
Kwani unatumia simu ya ‘katululu’? DJ Mo azushia polisi waliokamata dereva wake

Kwani unatumia simu ya ‘katululu’? DJ Mo azushia polisi waliokamata dereva wake

Na FRIDAH OKACHI

MTUMBUIZAJI wa muziki wa Injili alifanya fujo Alhamisi jioni kwenye kituo cha polisi cha Muthangari akitaka dereva wake aliyekamatwa kwa kosa la kuendesha gari bila leseni, aachiliwe.

Samuel Muraya almaarufu Dj Mo, aliandamana na mkewe Size 8 hadi katika kituo hicho, eneo la Dagoretti Kaskazini, kufahamu kosa alilofanya dereva wao.

Kupitia video iliyochapishwa kwenye ukurasa wa BNN Instagram, Oktoba 19, 2023, Dj Mo anaonekana akimsukuma afisa wa polisi ambaye alikuwa anamzuia kuingia.

“Kwani hunijui? Angalia leseni ya dereva kwa mtandao. Kwani unatumia simu ya katululu?” Alifoka Dj Mo.

Naye Size 8 alionekana kukasirishwa na malumbano kati ya Dj Mo na maafisa hao.

“Ni makosa kumkamata bila kuangalia iwapo ni dereva halali. Mjue sisi ni Wakenya na tunahitaji kuhudumiwa vilivyo,”alisema Size 8.

Dj Mo aliambia Taifa Leo sababu kuu ya kufika kwenye kituo hicho, ni kukasirishwa na hatua ya polisi kumkamata dereva wake bila kuangalia mtandaoni iwapo amehitimu kuwa dereva au la.

“Nilikuwa nimekasirika. Dereva wangu aliwaambia waangalie kwa simu zao lakini wakachukua hatua ya kumshika. Sasa dereva wetu ako huru,”alisema Dj Mo.

Maelezo yake ni kinyume na habari zilizokuwa zimechapishwa kuwa ni yeye aliyekuwa ametiwa mbaroni kwa kosa la kutokuwa na leseni. Polisi wanasema maafisa wao wa trafiki walimkamata dereva wala si Dj Mo.

Mapema wiki, wawili hao wakihojiwa na kituo cha Getu Fm, walihimiza wanandoa wengine wasitegemee teknolojia kusuluhisha mizozo. Size 8 alionya wanandoa kutoangalia simu za wapenzi wao.

Lakini akiwa katika kituo cha polisi Muthangari alionekana kuwakosoa polisi kwa kutotegemea teknolojia.

  • Tags

You can share this post!

Wakulima na wakazi wa Nyeri washerehekea mvua

Aliua mwanawe ili apate nafasi ya kuyoyomea Uarabuni lakini...

T L