• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 6:07 PM
Mapenzi jamani! Huyu unayempenda anampenda yule

Mapenzi jamani! Huyu unayempenda anampenda yule

NA JOHN KIMWERE

JOYLEEN Akware Emojong ni mmojawapo wa waigizaji wa kike wanaopania kutinga hadhi ya kimataifa miaka ijayo akifahamu fika kwamba penye nia pana njia.

Mwigizaji huyu anasema suala la mapenzi lishakuwa changamoto kwake. Kwa sasa amepiga breki uhusiano wa kimapenzi, akitumia muda wake kujikuza zaidi kiusanii.

“Kiukweli sina mpenzi wala sina mpango wa kumsaka maana niliyekuwa naye alinitenda,” akasema.

Anadokeza kuwa alihisi kudhalilishwa alipogundua kwamba aliyempenda kumbe alikuwa anampenda mwingine.

Kando na uigizaji alioanza mwaka 2021, ni mwanafunzi wa mwaka wa pili akilenga kuwa mwanahabari wa runinga.

Pia ni mwanamitindo anayekuja ambapo anajivunia kushiriki mashindano kadhaa.

”Katika uigizaji sijapata mashiko lakini nimepania kupambana mwanzo mwisho kuhakikisha ni taaluma itakayokuwa ajira yangu ndani ya miaka mitano ijayo,” anasema.

Anaongeza kuwa katika kipindi hicho analenga kuhakikisha ameshiriki filamu nyingi hapa nchini.

Msanii chipukizi Joyleen Akware Emojong. PICHA | JOHN KIMWERE

Anadokeza kuwa ingawa ndiyo ameanza kupiga ngoma, anafahamu bayana kwamba uigizaji ni ajira kwa wengi.

Pia anafunguka kuwa alitamani kujitosa katika uigizaji baada ya kutazama filamu ya ‘Sumu’ ya msanii Sasha iliyopeperushwa kupitia kituo cha runinga cha K24 miaka kadhaa iliyopita.

Anasema kuwa tangu akiwa mtoto, alipenda sana kutazama filamu kufikia wakati moja akatamani kuwa mwigizaji lakini alidhamiria kuhitimu kuwa mwanahabari, taaluma anayoisomea.

Binti huyu aliyetua duniani mwaka 2002 anajivunia kushiriki filamu mbili ‘Imposter’ na ‘Selina’ pia kipindi cha ‘Date my Family’ kilichorushwa kupitia runinga ya Maisha Magic East.

Katika mpango mzima, anatamani sana kufuata nyayo za watangulizi wao zaidi analenga kutinga hadhi ya mwigizaji mahiri duniani, raia wa Marekani, Jenniffer Lawrence, anayejivunia kushiriki filamu kama ‘Don’t Look Up’ kati ya nyingine.

Anasema duniani angependa sana kufanya kazi na mwigizaji shupavu Nadia Buari kutoka Ghana ambaye ameshiriki filamu nyingi tu ikiwamo ‘Hopefully Yours’ na ‘Slave to Lust’ kati ya nyingine. Mwingine akiwa mwigizaji mahiri wa filamu za Kinigeria (Nollywood), Luchy Donalds anayejivunia kushiriki filamu kama ‘Isabela’ na ‘Princess Clara’.

Hapa nchini anatamani kujikuta jukwaa moja na kina Sanaipei Tande na Brenda Wairimu. Tande ameshiriki filamu kama ‘Aziza,’ na ‘Kina’ nazo za Wairimu zikiwa ‘Monica’ na ‘Disconnect’ kwa kutaja tu baadhi ya kazi.

Anatoa wito kwa serikali za Kaunti ziweke mikakati kabambe kwenye jitihada za kupaisha tasnia ya uigizaji kwa kuzingatia taifa hili limefurika wasanii wengi tu wanaokuja, wavulana na wasichana.

  • Tags

You can share this post!

Vita vya maneno vyazuka kati ya Kang’ata na kamishna

TAHARIRI: Serikali, Azimio wajue hatima ya nchi ni kwao

T L