• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
Mchango: Familia ya mtandaoni yampa mtangazaji Kimani Mbugua bega la kuegemea

Mchango: Familia ya mtandaoni yampa mtangazaji Kimani Mbugua bega la kuegemea

NA MARY WANGARI

MWANAHABARI nyota wa zamani katika runinga ya Citizen amejitokeza kuomba msaada kwa Wakenya baada ya kupambana na maradhi ya akili (bipolar) kwa miaka miwili.

Kupitia video aliyorekodi na kuisambaza Jumapili kwenye mitandao ya kijamii na iliyofikia Taifa Leo, kijana Kimani Mbugua amefichua kwamba maisha yalianza kumwendea segemnege mnamo 2020 alipogunduliwa kuwa na matatizo ya akili.

Aidha, Mbugua aliyeruhusiwa kutoka hospitalini wiki iliyopita, alikiri kuwa hana mbele wala nyuma hata pa kuishi baada ya wahisani waliokuwa wakimsaidia “kumchoka.”

Katika video hiyo, Mbugua anaonekana akiwa na mkoba wake unaosheheni mali pekee aliyosalia nayo zikiwemo stakabadhi za pendekezo la biashara anayodhamiria kuanzisha huku akiomba Wakenya kumsaidia.

“Nimepoteza vitu vingi, nimepoteza marafiki wengi katika safari hii, watu walinichoka na sasa wengi hawataki kunisaidia wanasema wamechoka. Nilipotoka hospitali wiki iliyopita, nahisi akili yangu imerejea timamu na sitaki kurejea mahali nilipokuwa,” alisema.

“Nina mpango wa biashara niliyooweza kuandaa katika muda wa wiki moja baada ya kutoka hospitalini. Nina pendekezo langu la kwanza kwa mteja, mpangilio wa kampuni na kila kitu kiko tayari. Ninachohitaji tu ni mshirika atakayeleta pesa na kufanikisha mawazo yangu.”

Kulingana na mwanahabari huyo, aliamua kuchukua hatua hiyo ili kuepuka kuzama tena kwenye matatizo ya kiakili na kurejelea matumizi ya mihadarati.

“Niligundua ninaweza kuumia kisiri, nikose kuzungumza kisha nizame kwenye matatizo ya kiakili na kurejelea dawa za kulevya. Sitaki kurejelea mihadarati. Nimekaa kwa miezi miwili bila kuvuta sigara na bangi ambavyo ndivyo vitu pekee nilikuwa nikitumia,” akaeleza.

Alisimulia jinsi alivyopoteza mali yake yote hasa baada ya jamaa wake wa karibu kuuza gari alilochukua kwa mkopo na kumwacha akidaiwa mamilioni kiasi cha kuomba simu aliyotumia kuomba msaada.

Kufuatia kilio cha mwanahabari huyo Wakenya wakiongozwa na Roseline Ngolo almaarufu Nyako kupitia mtandao wake wa kijamii wa Tiktok walidhihirisha kwa mara nyingine ukarimu wao.

Kufikia Jumanne, Mbugua alikuwa amechangiwa kiasi cha nusu milioni na kupata mialiko ya kazi na makao katika muda wa saa moja na dakika 30 pekee baada ya kuomba usaidizi.

“Kaka njoo tufanye kazi. Tunaweza kutazama na kulinganisha pendekezo lako na letu. Huku tukifanya hivyo, tunaweza kukupa chumba bila malipo katika eneo la Tassia karibu na Nyayo Estate,” aliahidi Julius Apacha, ambaye ni mkurugenzi wa shirika moja nchini.

Mbugua aligonga vyombo vya habari kwa mara ya kwanza Oktoba 2022 alipochapisha ujumbe kupitia Twitter akiwalaumu wazazi wake kwa kumfungia katika Hospitali ya Mathari ili kumwadhibu.

“Ninaomba wote wanaonifahamu wawasihi wazazi wangu wanitoe katika Hospitali ya Mathari. Nilikuja hapa baada ya kukumbwa na kipindi kifupi cha matatizo ya akili Agosti 4, 2022, na nikaruhusiwa kuondoka Agosti 10, 2022,” alisema.

Hata hivyo, mamake Peris Wanjiku alikanusha madai hayo akisema mwanawe alikuwa anapokea ushauri nasaha kutokana na matumizi ya bangi kupita kiasi.

“Anapovuta bangi huwa anashikwa na kichaa. Hatujamtelekeza na tunahisi vibaya mno kwa sababu ya hali yake. Ni kama anafanya hivyo kutuumiza. Tumemsamehe na hatuna tatizo naye,” alisema Bi Wanjiku.

  • Tags

You can share this post!

Polisi wazima krusedi ya Pasta Ezekiel mjini Kilifi

Mbarak aonya kuhusu uwezekano wa maafisa wa umma kutumia El...

T L