• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 3:45 PM
Mwanamuziki Dennis Mutara hatimaye aruhusiwa kuondoka hospitalini

Mwanamuziki Dennis Mutara hatimaye aruhusiwa kuondoka hospitalini

NA WANDERI KAMAU

MWANAMUZIKI maarufu wa nyimbo za injili, Dennis Mutara, hatimaye ameruhusiwa kuondoka hospitalini, baada ya kulazwa kwa karibu wiki mbili, kutokana na kile kilitajwa kuwa uraibu wa vileo.

Bw Mutara ni miongoni mwa wanamuziki waliovuma katika ukanda wa Mlima Kenya katika miaka ya hapo nyuma, kutokana na nyimbo zake maarufu kama ‘Tigana na Andu’ (Achana na Watu) kati ya nyingine.

Kwenye taarifa katika mitandao ya kijamii, Alhamisi, Septemba 21, 2022, mwanamuziki Karangu Muraya na Gavana Mutahi Kahiga wa Kaunti ya Nyeri—ambao ni miongoni mwa watu waliogharimia matibabu yake—walitoa jumbe za kumshukuru Mungu kwa kumwezesha msanii huyo kuimarika tena kiafya.

“Tunamshukuru Mungu kuwa ndugu yetu Dennis Mutara ameruhusiwa kuondoka hospitalini. Tunawashukuru wote waliojitokeza kumsaidia kwa namna yoyote ile kutokana na matatizo aliyokuwa nayo,” akasema Bw Muraya.

Masaibu ya mwanamuziki huyo yaliangaziwa na Taifa Leo wiki mbili zilizopita, baada ya kulazwa hospitalini, akionekana kuzidiwa na maumivu.

Bw Mutara alilazwa katika hospitali moja Kaunti ya Murang’a, Jumatatu, Septemba 11, 2023, na Wasamaria Wema waliofika nyumbani kwake katika eneo la Maragua.

Ijapokuwa watu walio karibu naye hawakueleza sababu halisi iliyomfanya kulazwa hospitalini, Taifa Leo ilithibitisha kwamba mwanamuziki huyo alikuwa amezama tena kwenye uraibu wa matumizi ya vileo.

“Tunataka kumpa nafasi (Dennis) kupona. Tunampeleka hospitalini kwanza na baadaye katika kituo cha kurekebishia tabia (rehab). Anaonekana kuzidiwa na matumizi ya vileo,” akasema mmoja wa watu walio karibu na mwanamuziki huyo.

  • Tags

You can share this post!

Mume ameniruhusu nitafute madume wa kumsaidia kazi, demu...

Boda ‘fisi’ wa kubeba vipusa bure aacha kazi...

T L