• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Richie Spice kutumbuiza na kula ngege Kisumu

Richie Spice kutumbuiza na kula ngege Kisumu

RUSHDIE OUDIA Na ALI JUMANNE

MWANAMUZIKI Richell Bonner almaarufu Richie Spice ambaye tayari yuko jijini Nairobi anatarajiwa pia kuzuru Kisumu ambapo atapata fursa ya kutumbuiza mashabiki wa Reggae na kujionea jiji hilo lenye sifa ya kipekee.

Gavana wa Kisumu Prof Anyang Nyong’o ametangaza kwamba Spice ambaye ni raia wa Jamaica atatembezwa ajionee Ziwa Victoria, miundomsingi ya jiji hilo na kutangamana na wenyeji. Mwanamuziki huyo na kikosi chake cha watumbuizaji watapata fursa adimu ya kula vyakula vya kiasili vya Waluo miongoni mwa vyakula hivyo ikiwa ni samaki aina ya ngege na mboga za kienyeji kama osuga.

“Ni fursa nzuri kwetu hapa kujitangaza kuwa Kisumu ni kivutio cha utalii na vilevile kitovu cha utangamano na sehemu yenye fursa za kuvutia wawekezaji,” amesema Gavana Nyong’o.

Nyong’o amesema serikali ya kaunti inashirikiano na Ziva Empire kuhakikisha kwamba Spice anapiga shoo ya uhakika Jumapili.

Kulingana na mpangilio ni kwamba mwanamuziki huyo atamtembelea gavana na baraza lake la mawaziri, wawahutubie wanahabari kabla ya kuingia katika hoteli ya Imperial Sarova. Baadaye mwanamuziki huyo atatumbuiza katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta ulioko Mambo Leo.

Mwanamuziki huyo amejizolea umaarufu kutokana na nyimbo zake zenye mdundo wa kipekee kwa mashabiki wa muziki. Baadhi ya vibao vyake vya Reggae ni “Brown Skin”, “Youth Dem Cold Rel Bad”, “Grooving’ My Girl”, “Earth a Run Red”, “Marijuana”, “The Plane Land” na “King and Queen”.

Spice aliwahi kutumbuiza humu nchini mnamo Februari 16, 2019 ambapo aliwatumbuiza wapenzi wa muziki waliokongamana katika ukumbi wa KICC jijini Nairobi kwenye shoo aliyopiga wakati wa tamasha ya Nobody can Stop Reggae.

Ndugu zake watatu – Pliers, Spanner Banner na Snatcha Lion – nao ni wanamuziki wanaotambulika ulimwenguni kote.

  • Tags

You can share this post!

Akiri kuua mwanawe kutokana na msongo wa mawazo

Waliokamatwa kwenye msako mkali Mukuru kufikishwa kortini...

T L