• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 6:55 PM
Bila kuzingatia muktadha, neno ‘hakika’ halipaswi kubadilishwa

Bila kuzingatia muktadha, neno ‘hakika’ halipaswi kubadilishwa

Nitaanza makala haya kwa kuuliza swali lifuatalo: Je, mtu huwa na uhakika wa jambo au hakika ya jambo? Vipo baadhi ya vielezi ambavyo aghalabu hukosewa katika matumizi.

Hivi ni vile ambavyo vimeundwa kutokana na aina nyingine za maneno kwa mfano nomino au vivumishi. Kabla ya kutaja mifano michache ya vielezi hivyo, ni muhimu kufafanua kuwa kielezi ni neno ambalo hutoa maelezo zaidi kuhusu kitenzi, kivumishi au kielezi kingine na kwa namna hiyo kuarifu kitendo kilitendeka wapi, lini,mara ngapi na vipi.

Kutokana na maelezo haya, kielezi hutekeleza dhima tatu muhimu ambazo ni kufafanua kitendo, kivumishi na kielezi kingine. Nitatoa mifano mitatu inayoonyesha dhima hizi katika mtawalia tulioutaja hapo juu bila kujikita katika ukina.

Alimwadhibu kupindukia(kinafafanua kitenzi ‘alimwadhibu’); Yeye ni mwanamume mbaya sana(kinafafanua kivumishi ‘mbaya’); Usiku wa manane, mbwa walibweka vikali sana(kinafafanua kielezi ‘vikali’).

Sasa tugeukie mifano michache ya vielezi tulivyoahidi hapo juu. Hii ni pamoja na “rahisi”, vigumu na hakika. Neno “rahisi” ni la kategoria mbili ambazo ni kivumishi na kitenzi. Kielezi ambacho huundwa kutokana na mojawapo ya kategoria hizi ni “kwa urahisi”.

Hata hivyo, kosa ambalo hufanywa na baadhi ya watumizi wa lugha ya Kiswahili ni kuligagamizia neno rahisi kiambishi {vi} kisha kulitumia kama kielezi.

Ni vyema kufahamu kuwa vielezi vilivyohimiliwa katika mizizi {ki} na {vi} ni vichache navyo huelezewa kuwa ni vya namna mfanano. Huitwa vielezi vya namna mfanano kwa sababu hufananisha vitendo na nomino au vivumishi.

Kwa mfano, tunaposema kuwa fulani hutembea kike,kielezi hiki kinatokana na nomino mke. Kauli “Ulifanya vizuri kumsaidia” ina kielezi ‘vizuri’ ambacho kinatokana na kivumishi {-zuri}. Kutokana na kivumishi {-gumu} tunapata kielezi vigumu.

Kwa hivyo, usemi “Itakuwa ngumu kukusaidia” si sahihi kisarufi. Sahihi ni:“Itakuwa vigumu kukusaidia”. Tofauti na mzizi -gumu ambao huongezewa {u} ili kupata nomino ugumu, neno hakika haliongezewi viambishi vyovyote.

Neno hilo la pili ni la kategoria mbili – nomino na kielezi. Kama kielezi, hutoa hakikisho la kitendo. Kama nomino, huibua dhana ya ukweli halisi.

Alhasili, tunapaswa kusema “Sina hakika ya unayoyasema”; Sina hakika atakuja lini; Nina hakika ya jibu nililompa n.k. Ni kosa kubadili umbo la hakika. Kwa hivyo, ni kosa kisarufi kusema: “*Sina uhakika wa mambo unayoyasema”.

You can share this post!

Sindwele amtoroka dereva wake kutokana na ‘uchochole’

DONDOO: Madugu wageuka mbwa na paka