• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 6:55 PM
CHAKISE; Nuru inayovumisha mawimbi ya Kiswahili Shuleni Stelurm Elite, jijini Nairobi

CHAKISE; Nuru inayovumisha mawimbi ya Kiswahili Shuleni Stelurm Elite, jijini Nairobi

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Stelurm Elite, Nairobi kimewawezesha wanafunzi kupiga hatua na kutia fora katika makuzi ya Kiswahili.

Shule hii kwa sasa imekuwa kati ya zile zinazofanya vyema zaidi katika masuala ya kiakademia na ukuzaji wa talanta mbalimbali miongoni mwa wanafunzi.

Chama hiki almaarufu CHAKISE kiliasisiwa mapema mwaka jana na Bw Samuel Wangila (Mwalimu Mkuu) ambaye sasa anashirikiana na Bi Judy Mwende, Bw Francis Kariuki na Bw David Tinega kusukuma gurudumu la Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Stelurm Elite.

Bw Wangila ni mtetezi mkubwa wa Kiswahili na msomaji kindakindaki wa gazeti hili la Taifa Leo. Amewaamshia wanafunzi wake ari ya kukipenda Kiswahili kiasi kwamba kila wazungumzapo, Kiswahili chao huvutia sana.

Lengo kuu la kuanzishwa kwa CHAKISE ni kuendeleza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya shule kwa kuwapa wanafunzi jukwaa mwafaka zaidi la kuhudhuria makongamano na kuzuru shule mbalimbali za msingi ili kuhamasishana na wanafunzi wenzao kuhusu umuhimu wa Kiswahili kama somo na pia kitega-uchumi.

Maazimio mengine ya chama ni kukuza vipaji vya usanii kupitia utambaji wa hadithi, uchoraji, uigizaji, utunzi wa mashairi na uandishi wa kazi nyinginezo bunilizi.

Isitoshe, chama huwaunganisha wanafunzi wote shuleni na kuwapa fursa ya kuelekezana katika baadhi ya mada zinazowatatiza madarasani.

CHAKISE pia kimeanza harakati za kuchapisha jarida la chama. Dhima kuu ya jarida hili ni kuzua mijadala muhimu katika taaluma ya Kiswahili na kuwapa wanafunzi nafasi ya kujieleza na kukuza vipaji vyao katika nyanja mbalimbali za sanaa.

Kupitia CHAKISE, walimu na wanafunzi shuleni Stelurm Elite kwa sasa wana jukwaa bora la kuzamia usomaji wa magazeti ya Taifa Leo kupitia mradi wa Newspapers in Education (NiE) unaoendeshwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG).

Kupitia mradi huu, NMG inayatumia magazeti ya Taifa Leo kuimarisha viwango vya kusomwa na kufundishwa kwa Kiswahili na masomo mengine katika shule za msingi na upili za humu nchini.

Kwa mujibu wa Bw Wangila, wengi wa wanafunzi wake wanaothamini na kuchangamkia usomaji wa Taifa Leo na kushiriki Shindano la Uandishi wa Insha katika gazeti hili, hudumisha umahiri wao katika lugha kwa kukwangura alama za juu zaidi hata katika mitihani ya kitaifa (KCPE).

Anaungama kwamba majaribio ya mitahini katika Taifa Leo ni daraja halisi la mafanikio kwa wengi wa wanafunzi wake ambao wamechochewa kutia fora katika somo la Kiswahili.

Miongoni mwa wanafunzi waliofaulu vyema zaidi katika KCPE 2020 kutoka Shule ya Msingi ya Stelurm Elite ni Daniel Opore (387), Cedrick Mwaura (376), John Kibiri (375), Brighton Odhiambo (375), Crinse Omollo (374) na Hillary Nathan (372).

You can share this post!

DONDOO: Madugu wageuka mbwa na paka

Rais wa Haiti auawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake