NA SAMMY WAWERU
DAIICHI Farm Ltd ni kampuni inayojishughulisha na usindikaji (processing) wa nyama za nguruwe katika Kaunti ya Meru.
Kabla kuingilia uongezaji thamani, ilianza kama ‘shamba’ la ufugaji wa nguruwe.
“Tuliingilia ufugaji wa nguruwe mwaka wa 2014,” afichua Philip Ndeng’era, mtaalamu wa Habari na Mawasiliano (IT) na Mauzo katika shirika hilo.
Huku nguruwe wakiwa kati ya mifugo walioathirika pakubwa kutokana na mfumko wa bei ya chakula, kampuni hiyo 2020 ilipata mwanya mpya kuteka mapato zaidi.
Mwaka huo ambao Kenya ilithibitisha kuwa mwenyeji wa janga la Covid-19, ndio ilianza uongezaji thamani nyama za nguruwe.
“Homa ya corona ilitufumbua macho, tukatambua mbinu kuteka mapato na faida,” Ndeng’era asema.
Malisho ya mifugo ya madukani, bei yake haikamatiki kufuatia gharama ya juu ya malighafi kuyatengeneza.
Baadhi ya wafugaji wamelazimika kuasi ufugaji.
Kulingana na Ndeng’era, hatua kuingilia mtandao wa uongezaji thamani ilishawishiwa na matamanio ya wateja kupata bidhaa zilizosindikwa (processed products).
Tunaunda soseji za kawaida, soseji motomoto na soseji za mwananchi, afisa huyo aelezea.
Daiichi Farms Ltd pia ni wataalamu wa viungo na sehemu maalum za nguruwe kama vile miguu, mbavu na loin chops.
“Bidhaa za nyama za nguruwe zilizoongezwa thamani zinateka soko lenye ushindani mkuu.”
Kando na mapato ya kuridhisha, Ndeng’era anataja nafasi tele za ajira zinazotokana na mtandao huo, kuanzia wafugaji wa nguruwe, wahudumu wa bucha (maarufu kama buchari), wanaounda na kuzalisha soseji.
Kwa sasa, Daiichi Farms Ltd ina nguruwe wapatao 1, 500 na pia ina kandarasi na wafugaji wengine ili kuziba gapu ya bidhaa zake sokoni.
Kampuni hiyo ilikuwa miongoni mwa wahusika katika uzalishaji nyama nchini walioshiriki Maonyesho ya Nyama Kenya 2023, katika Ukumbi wa KICC, Nairobi.