• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
DINI: Mstari kati ya wema na ubaya ni mwembamba

DINI: Mstari kati ya wema na ubaya ni mwembamba

NA PADRE FAUSTINE KAMUGISHA

WEMA na ubaya vipo kila mahali. Ubaya utashinda kama watu wema hawafanyi chochote kizuri.

“Ubaya hauna nguvu kama watu wema hawana hofu,” alisema rais Ronald Reagan.

Ubaya haufukuzi ubaya. Wema unafukuza ubaya. Mstari kati ya wema na ubaya ni mwembamba. Kwanza mstari huo ni chakula cha akili. Mzee mmoja alimwambia mjukuu wake, “Mtoto wangu, kuna vita kati ya mbwa mwitu wawili ndani yetu sote. Mmoja ni Ubaya. Ni hasira, husuda, uchoyo, chuki, kujidharau, uongo na ubinafsi. Na mwingine ni Wema. Ni furaha, amani, upendo, unyenyekevu, wema, na ukweli.”

Mvulana alitafakari kidogo na kumuuliza babu yake, “Babu, mbwa mwitu gani anayeshinda?”

Babu alijibu, “Unayemlisha.”

Ukiwaza mabaya unamlisha mbwa mwitu anayeitwa Ubaya. Ukiwaza mazuri unamlisha mbwa mwitu anayeitwa Wema.

Mstari mwembamba kati ya wema na ubaya ni chakula unacholisha akili yako. Mawazo ni chakula cha akili. Mtume Paulo anatuasa, “Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema” (Warumi 12:21).

Mstari wa pili mwembamba kati ya ubaya na wema ni upokeaji.

Mtu mmoja alinunua gazeti toka kwa muuza gazeti kwenye kibanda cha magazeti.

Muuza magazeti alitoa huduma isiyo na heshima na yenye malalamishi.

Mnunuzi wa gazeti alipokea gazeti alililotupiwa usoni kwa tabasamu. Alimtakia muuza gazeti wikendi njema.

Rafiki yake mteja alitazama mambo yote kwa mshangao mkubwa. Alimuuliza mnunuzi wa magazeti, “Anakutendea hivi bila heshima kila mara?”

“Ndiyo, anafanya hivyo kila mara,” mnunuzi wa gazeti alijibu.

“Na kila mara unamtendea kwa upole na heshima?” akahoji rafiki wa mnunuzi.

“Ndiyo,” alijibu mnunuzi.

“Kwa nini unakuwa mwema kwake wakati yeye haonyeshi adabu na heshima?” alihoji rafiki wa mnunuzi wa gazeti.

“Ni kwa sababu sitaki aniamlie namna ya kupokea anavyonitendea na jinsi ya kutenda.”

Mtu akikufanyia ubaya nawe ukamtendea jambo baya, panakuwepo watu wabaya wawili.

Mstari wa tatu mwembamba kati ya wema na ubaya ni subira.

Mdhambi wa leo anaweza kuwa mtakatifu wa kesho. Mtu mbaya wa leo anaweza kuwa mwema kesho. Dharau ya leo ni heshima ya kesho.

Tunapata mwanga wa subira katika mfano wa magugu ya ndago kati ya ngano.

“Ufalme wa mbingu umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika shamba lake. Lakini usiku, adui yake akaja, akapanda ndago kati ya ngano, akaenda zake. Miche ilipomea na kuchanua, ndago pia zikaonekana. Hapo watumishi wa mwenye shamba wakamwendea na kumwambia, “Bwana hukupanda mbegu njema katika shamba lako? Basi limepataje ndago?

Akawaambia, “Adui amefanya haya. “Watumishi wakamuuliza, ‘Je, wataka twende kuyakusanya? Akasema, “La, sivyo, msije mkang’oa ngano pamoja na ndago mnayotaka kukusanya. Acheni mbegu zote mbili zikue pamoja mpaka wakati wa mavuno” (Mathayo 13: 24- 30).

Tunajifunza mambo matano. Kwanza, ni somo la subira na uvumilivu. Mpe muda.

Mungu ni mvumilivu kwa watu wote “Yeye huvumilia, maana hapendi mtu yeyote apotee.”

Pili, “ Wema unaweza kuwepo bila ubaya, ubaya hauwezi kuwepo bila wema,” alisema Mt. Thomas Aquinas.Ubaya ni kimelea. Ubaya ni kama kupe unakula kutoka kwa wema. Tatu, mwisho wema utashinda.

Juu ya jambo hili Margaret Thatcher aliyekuwa waziri wa Uingereza wakati fulani alisema, “Niko katika siasa kwa sababu ya mgogoro kati ya wema na ubaya, na ninaamini mwishowe wema utashinda.”

Tujitahidi kushinda ubaya kwa wema. Nne, kila mahali kuna mbinu zake za kuangamiza uovu. Wanafunzi wa Yesu ambao wengi walikuwa wavuvi walifikiri wanajua mambo ya magugu na ngano.

Walizoea kuosha nyavu, kuvua samaki na kuuza samaki. Ni kama waliuliza Bwana huwezi kuangamiza waovu kama tunavyoangamiza samaki waliooza? Huwezi kutumia mbinu za ziwani shambani. Yote yakiishasemwa, tuushinde ubaya kwa wema.

You can share this post!

Sonko aacha Kalonzo mataani, ajiunga na Ruto

HUKU USWAHILINI: Jamani ndoa zimekuwa ngumu huku kwetu,...

T L