• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
Dj Fatxo ‘awasamehe’ waliomhusisha na mauaji ya Jeff Mwathi baada ya kuondolewa mashtaka

Dj Fatxo ‘awasamehe’ waliomhusisha na mauaji ya Jeff Mwathi baada ya kuondolewa mashtaka

NA SAMMY WAWERU

MCHEZA santuri Lawrence Wagura Njuguna maarufu kama Dj Fatxo ametangaza kusamehe waliomhusisha na mauaji ya mwanafasheni Jeff Mwathi.

Kupitia chapisho katika ukurasa wake rasmi wa Facebook Jumatano, Mei 17, 2023, Bw Wagura amesema tetesi za kuhusishwa na maafa ya Jeff, 23, zilimkosesha amani kwa kile ametaja kama ‘kusulubishwa bila hatia’.

“Ninakumbusha kila mmoja umuhimu wa kutofanya maamuzi au kuhangaisha mtu kupitia mitandao kwa msingi wa taarifa za uongo ama fitina. Wengi wenu mnajua machungu na mazito ambayo nimepitia kutokana na mambo ya uongo,” aliandika.

Msanii huyo ambaye pia ni mwimbaji wa nyimbo za Mugithi, alivunja kimya chake baada ya Idara ya Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI) na Afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kumuondolewa mashtaka yaliyomhusisha na kifo cha Jeff.

Hata ingawa kesi hiyo haikuwa imewasilishwa rasmi kortini, duru zinaarifu mahakama pia imemuondolea lawama.

Kijana huyo alifariki akiwa katika nyumba ya Dj Fatxo, mtaani Kasarani, Nairobi mapema 2023.

Katika chapisho la Dj Fatxo, alikiri kuwa Jeff alikuwa rafiki yake.

“Sote tutathmini jinsi ya kuwa wakweli, wanaolewa na kuheshimiana. Ninaelewa kuwa hali hiyo (Jeff kufariki) haikuwa rahisi kwa baadhi yenu, ila ninawahimiza kuegemea ukweli…” alielezea.

Dj Fatxo pia alitumia jukwaa la chapisho hilo kufariji familia ya Jeff, marafiki zake na wanaohusiana naye kwa njia moja ama nyingine.

Kisa cha mvulana huyo kuuawa kiliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Kasarani, na kufuatia malalamiko ya umma mitandaoni afisi ya DCI Amin Mohamed ilitwaa kesi hiyo na kufanya uchunguzi upya.

Uchunguzi wa Kituo cha Kasarani, ulibainisha kuwa Jeff alifariki kwa kujitia kitanzi makao makuu ya DCI yakifutilia mbali taarifa hiyo.

Baada ya uchunguzi mpya kufanyika, ikiwemo mwili wa marehemu kufukuliwa kukaguliwa na Mwanapatholojia wa Serikali Dkt Johansen Oduor, DCI na DPP hawajaweka paruwanja kiini cha maafa ya kijana huyo.

Familia yake ingali inataka haki kutendeka, ikishikilia kwamba mwana wao aliuawa bali si kujitia kitanzi kama inavyosemekana.

  • Tags

You can share this post!

BORESHA AFYA: Faida na madhara ya ulaji wa nyama

Si uamuzi wa busara kuzoea ‘snacks na fastfood’

T L