• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
Empower Smart yabuni apu ya kudhibiti ‘pocket money’

Empower Smart yabuni apu ya kudhibiti ‘pocket money’

Na MAGDALENE WANJA

KUKIDHI mahitaji ya mwanafunzi chuoni sio jambo rahisi kwa mzazi mwenye watoto zaidi ya mmoja.

Changamoto kuu huwa ni matumizi mabaya ya hela ambazo mwanafunzi anapokea kutoka kwa mzazi ili kukidhi mahitaji yake ya kila siku.

Hata hivyo, jambo hili limerahisishwa na uvumbuzi mpya ambao utawasaidia wanafunzi kutumia kiwango fulani cha pesa kila siku, na wala sio zaidi.

Apu hiyo kwa jina “Super Pay” ambayo imetengenezwa na kampuni ya Empower Smart, inatumika na wazazi pamoja na wanafunzi kwa kuhakikisha kuwa inaachilia kiwango fulani cha pesa kila siku.

Mwanzilishi wa kampuni ya Empower Smart Peter Muraya. PICHA | MAGDALENE WANJA

Mzazi akiwa mbali na mwanafunzi anaweza kukiona kiwango cha pesa ambacho mwanafunzi – mwanawe – anatumia kila siku.

Mwanzilishi wa kampuni ya Empower Smart Peter Muraya anasema kuwa uvumbuzi huo unatoa suluhisho kwa changamoto ambazo zimekuwa zikiwakumba wazazi.

“Kwa kutumia teknolojia hii, hali ya maisha shuleni itakuwa nzuri ikilinganishwa na hapo awali kwani wazazi sasa wataweza kutuma viwango vya pesa wanavyotaka bila hofu ya matumizi mabaya,” akasema Bw Peter Muraya.

Kwa kutumia njia hii, anayetuma pesa, ambaye kwa mara nyingi huwa ni mzazi, ana uhuru wa kuweka kiasi ambacho angetaka kimfikie mwanafunzi kila siku.

Bw Muraya anaongeza kuwa uvumbuzi huu ulitokana na changamoto alizopitia yeye binafsi alipokuwa akisoma katika chuo kikuu cha Kenyatta.

“Sikuwa na nidhamu katika matumizi ya pesa nilizopewa na mzazi , na mara nyingi nilijipata bila chochote ata wakati mwingine kukosa chakula ilhali mzazi wangu alikuwa amenipa pesa,” anasimulia Muraya.

Anaongeza kuwa uvumbuzi huo unampa mzazi nafasi kuamua iwapo mtoto atapokea hela kila baada ya siku, wiki au mwezi.

  • Tags

You can share this post!

Kampuni ya Thiwasco yapanda miti 1,500 Kang’oki...

Baadhi ya vyanzo vya furaha maishani mwako

T L