• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Eric Omondi na mpenziwe watarajia mtoto baada ya kupoteza wa kwanza

Eric Omondi na mpenziwe watarajia mtoto baada ya kupoteza wa kwanza

NA MERCY KOSKEI

MCHEKESHAJI Eric Omondi ametangaza kuwa anatarajia mtoto wake wa kwanza na mpenzi wake Lynne, miezi saba baada ya kupoteza ujauzito.

Kupitia mitandao ya kijamii mnamo Alhamisi Juni 8, 2023, Erick alisema kuwa hata ingawa imemchukua miaka 41 kupata mtoto wake, anatazamia kuanza safari ya uzazi.

Kwa furaha, Erick alitoa shukrani zake kwa Mungu kwa baraka na pia alimshukuru mchumba wake, Lynne, kwa kumfanya baba kwa mara nyingine baada ya kufiwa na mtoto wao wa kwanza.

Mcheshi huyo alilinganisha baraka yake na ile wa Sarah katika Bibilia, ambaye alisubiri muda mrefu kabla kupata mtoto.

Msanii huyo alishukuru Mwenyezi Mungu kwa kumrejeshea mtoto wao, akisisitiza umuhimu wa baraka hii.

“Imenichukua miaka 41 lakini hatimaye Mungu amejibu maombi na amenibariki na mtoto wangu. Nahisi kama Sarah – mke wa Ibrahimu wa Biblia, alisubiri mtoto wake mwenyewe kwa muda mrefu,” alisema.

Akipitisha ujumbe kwa wafuasi wake kupitia mitandao ya kijamii, Lynne alifichua kuwa simu yake imekuwa ikivuma kwa jumbe za heri njema kutoka kwa marafiki waliopata habari hii.

Lynne aliongeza kuwa amekuwa akificha ujauzito huo kimakusudi.

Septemba 2022, Lynne alichapisha video akiwa pamoja na Eric wakiwa kwenye mashua, huku akikiri kuwa alipenda kufurahia maisha na Eric.

Baadaye kupitia makala ya maswali na majibu na mashabiki wake kwenye mtandao wa Instagram, Lynne alifichua kuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Omondi.

Hata hivyo, miezi miwili baadaye, Erick alichapisha video mtandaoni, Lynne akionekana akilia kando ya kitanda cha hospitali na baadaye akatangaza kwamba walipoteza ujauzito.

“Jana usiku ulikuwa mojawapo ya usiku mrefu zaidi maishani mwangu. Tulipigana kwa zaidi ya saa 5 ili kujaribu kuokoa Malaika wetu mdogo, lakini Mungu alikuwa na mipango mingine,” Eric aliandika.

 

  • Tags

You can share this post!

KRA yamezea mate mapato ya mama mboga, bodaboda

Rais wa Uganda Yoweri Museveni asimulia kuhusu hali yake ya...

T L