• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Ezekiel Odero atua jijini Nairobi kuhubiri injili

Ezekiel Odero atua jijini Nairobi kuhubiri injili

NA SAMMY WAWERU

SIKU chache baada ya kuachiliwa na mahakama, Mhubiri Ezekiel Odero amesafiri jijini Nairobi ‘kuhubiri injili’.

Taifa Leo Dijitali imebaini kuwa mchungaji huyo wa Kanisa la New Life Prayer Centre Kilifi, amezuru jiji Jumatano, Mei 17, 2023 kufuatia mwaliko wa pasta mwenzake Pius Muiru wa Maximum Miracle Centre.

Msongamano katika mazingira ya kanisa la Bw Muiru, tayari umeanza kushuhudiwa washirika na waumini wakifurika.

Duru zinaarifu, ndani ya kanisa mabango na maua yamewekwa kulipamba, Mhubiri Odero akitarajiwa kueneza injili na ‘kutakasa’.

Inasemekana mtumishi huyo wa Mungu amelazimika kusitisha kwa muda mahubiri kufuatia idadi kubwa ya watu waliojitokeza.

“Ninaomba kwa unyenyekevu wale walio nje mtoke kwa mlango, mtasaidiwa na polisi na wasaidizi wetu kanisani muingie kwa utaratibu. Nitakatiza ibada kwa sababu siwezi kubali watu waumie,” Bw Odero akanukuliwa.

Pasta huyo alisema usalama ni jambo la muhimu sana na kwamba anaheshimu serikali, akihoji kuwa anadhamini uhai wa kila mtu.

Odero alikuwa amekamatwa akihusishwa na mchungaji mwenza Paul Mackenzie anayeandamwa na kesi za mauaji yanatajwa kuchangiwa na mafunzo na dini potovu.

Aidha, ilidaiwa kuwa Odero ni rafiki wa pasta huyo tata ambaye angali kizuizini kufuatia maafa ya halaiki ya washirika wake Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Mhubiri Odero, hata hivyo, aliachiliwa kwa dhamana ya bondi ya Sh3 milioni au Sh1.5 pesa tasilimu.

Aliwakilishwa na mawakili Danstan Omari na Cliff Ombeta.

Akaunti zake za benki na M-Pesa, hata hivyo, zimefungwa.

 

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Aliyejifanya askari na kutapeli dereva kizimbani

Washtakiwa kwa wizi wa mitungi ya gesi wakati wa maandamano...

T L