• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 5:50 AM
Fahali anayeenda haja chooni kama binadamu azua hofu kwa wakazi wa kijiji cha Nanjeho

Fahali anayeenda haja chooni kama binadamu azua hofu kwa wakazi wa kijiji cha Nanjeho

Na SAMMY WAWERU

WAKAZI wa kijiji cha Nanjeho, eneobunge la Matayos, Kaunti ya Busia wanaishi kwa wasiwasi kutokana na ng’ombe mwenye sifa na hulka za binadamu.

Kulingana na wenyeji, fahali huyo ameonekana akiingia kwenye choo kujisaidia sawa na afanyavyo binadamu.

Bw Shaban Wandera ameiambia runinga ya NTV kwamba ng’ombe huyo anaingia chooni kwa sehemu ya nyuma.

“Sijawahi kuona ng’ombe ambaye huenda ndani ya choo… Halafu anaenda na nyuma kisha anakaa chooni kujisaidia,” Wandera akasimulia.

Isitoshe, mbali na hulka hizo za kushangaza, fahali huyo anasemekana kusikiliza anayozungumza binadamu na kukaa mbali.

“Ni kama anaskia watu wakiongea anaelewa yanayozungumziwa. Anakaa mbali, haeleweki,” akasema.

Ikizingatiwa kuwa mafahali katika eneo la Magharibi mwa Kenya wanathaminiwa, fahali huyo ametajwa kuwa mnyama hatari kwa wakazi, jambo ambalo linaendelea kuzua hofu huku wakiepuka kutangamana naye.

Wanasema wanamtazama kwa umbali, hasa baada ya kujeruhi watu kadha.

“Alirusha teke mtu akiwa umbali wa karibu mita 50, akamvunja mbavu,” Bw Wandera akadokeza.

Bi Priscilla Barasa alithibitisha kuwa fahali huyo hatari alijeruhi jirani yake.

“Aliumiza jirani yangu ambaye kwa sasa anaendelea kupata matibabu,” Priscilla akasema, akieleza kwamba alijeruhiwa mabegani.

Ng’ombe ni wanyama wenye manufaa chungu nzima kwa binadamu kwa kuwa hutoa maziwa na kuchinjwa nyama, ila kwa wakazi wa kijiji cha Nanjeho ng’ombe dume huyo amekuwa kero.

Wanaiomba serikali kuingilia kati na kuwasaidia ili isisababishe hasara zaidi.

“Ni ng’ombe ambaye hashikiki na hata hawezi kufungwa kwa kamba,” Jackline Masiga akalalamika, Bw Shaban Wandera akisema “watu wanaona huenda akawa jini ama mwenye ng’ombe (anakotoka) alimtakasa kwa kumganga au labda ni mnyama aliyeibwa”.

Eneo la Pwani ndilo hushuhudia visa vya aina hiyo, hasa vinavyohusishwa na paka, ila fahali huyo anaendelea kuzua maswali tele na hofu kwa wenyeji Matayos.

You can share this post!

Havi akaa ngumu

Mwanasoka mstaafu Ronald Okoth ni balozi mpya wa kituo cha...