• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
FATAKI: Usitoe huduma za mke wa ndoa kwa dume ambalo wala halijakuoa

FATAKI: Usitoe huduma za mke wa ndoa kwa dume ambalo wala halijakuoa

NA PAULINE ONGAJI

MAPEMA wiki hii nilikutana na picha fulani iliyochapishwa na binti mmoja mtandaoni, ambapo ilioonyesha vyakula vilivyopakiwa vizuri kwenye vifaa vya plastiki na kuwekwa kwenye friji.

Chini yake kulikuwa na maandishi “kila wiki ninapomtembelea mpenzi wangu, lazima nihakikishe kuwa nampikia na kumhifadhia chakula cha kumtosha juma nzima,” alisema.

Chapisho hili lilisababisha hisia mseto kutoka kwa wanamitandao huku wengi wakionekana kumdhihaki binti huyu.

Nakumbuka maoni fulani ya kudhihaki kutoka kwa binti fulani “juma lililopita uliweka chumvi nyingi” yaliyoonekana kuashiria kwamba pia yeye alikuwa mpenzi wa huyo kaka aliyekuwa akiandaliwa minofu kila juma.

Japo naamini kwamba ulikuwa utani, yaliakisi hali halisi ya yanayowakumba mabinti wanaojitoa kijasho kwa kuyashughulikia mahitaji ya madume ambao hawajawaoa wala kuwachumbia rasmi wakidhani kwamba hayo ni mapenzi.

Hii yanikumbusha kisa cha kaka mmoja miaka kadhaa iliyopita ambapo alikuwa akinung’unika kwa sababu binti mmoja alikuwa “amevamia” nyumba yake na kutaga mayai. Yaani kipusa huyo alikuwa amejileta nyumbani mwa kaka huyo na kwa wiki tatu mfululizo hakuwa anaonyesha dalili za kurejea alikotoka.

Naelezwa kwamba mojawapo ya sababu kuu ambazo zimewafanya akina kaka wengi siku hizi kuzembea inapowadia wakati wa kufuata utaratibu unaohitajika kabla ya kupata mke, ni haya mazoea ya kunyweshwa maziwa ilhali hawammliki ng’ombe.

Nasikia kwamba madume siku hizi hufurahia kila wanapotembelewa na vipusa wakati wa wikendi kwani wanafahamu kwamba mbali na kufanyiwa usafi na kupikiwa, watapata ile huduma nyingine muhimu bila malipo.

Dhana hii ni sababu tosha ya kuonyesha jinsi kuna baadhi ya mabinti wanaojishusha thamani wakidhani kwamba hii ni ishara ya mwanamke bora. Ya nini uchubue mikono yako ukimfulia na kumpikia kaka ambaye huna uhakika kwamba atakuoa?

Ya nini kumpa kaka ambaye hata hajathibitisha uhusiano wenu?

Najua wanasema sehemu hiyo sio sabuni inayoweza kuisha lakini je kwa nini utatize kwa kumpa mtu asiyestahili?

Ujumbe huu ni kwa wale warembo unaowapata kila wikendi wakiharibu kucha zao kuwafulia nguo madume ilhali wanafahamu vyema kwamba sio wao pekee mpangoni.

Kumbuka kuwa wengine hawapewi hata nauli ya kuja wala kurejea wakishawahudumia wanaume hawa.

Japo ni makosa wanavyofanya baadhi ya akina kaka hawa, utawalaumu vipi? Wengi wao hujiuliza, ya nini nimnunue ng’ombe ilhali naweza pata maziwa ya bure?

  • Tags

You can share this post!

PENZI LA KIJANJA: Anaweza kukwama kwako na hakupendi

Orengo aponda wabunge ‘waasi’ Azimio akisema...

T L